Serikali yabisha hodi rasmi mashamba ya Shambarai Burka na Bwawani

NA ANTHONY ISHENGOMA
WANMM

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) zimesaini mkataba wa makubaliano wa uendelezaji na utekelezaji wa mpango wa matumizi ya shamba lenye ukubwa wa ekari 6176.5 lililopo katika Wilaya za Arusha na Arumeru mkoani Arusha.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga na Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, Bw.Wilson Charles wakisaini mkataba wa mpango wa utekelezeji wa matumizi ya Shamba la Bwawani na Shambarai Burka liloko Wilaya ya Arusha na Arumeru Mkoani Arusha.

Utiaji sahihi makubaliano ya Shamba la Shambarai Burka na Bwawani ambalo awali lilimilikiwa na Tanzania Plantations Limited umefanyika Agosti 29,2023 jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga.

Sambamba na Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, Wilson Charles na kushuhudiwa na Wakurugenzi wa Halmshauri za Arusha na Arumeru.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga na Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, Bw. Wilson Charles wakikata utepe kuashiria kusainiwa kwa mkataba wa mpango wa utekelezeji wa matumizi ya Shamba la Bwawani na Shambarai Burka liloko Wilaya ya Arusha na Arumeru mkoani Arusha.

Akiongea kabla ya zoezi la utiaji sahihi wa makubaliano ya mpango wa utekelezaji na mgawanyo wa shamba hilo, Katibu Mkuu Sanga amesema, shamba hilo lilikuwa na mgogoro kati ya Wizara ya Ardhi na Kampuni ya Tanzania Plantations na makubaliano haya yanafanyika baada ya mahakama kuridhia ombi la Wizara ya Ardhi la kukatatua mgogoro nje ya Mahakama.

Mhandisi Sanga ameongeza kuwa, baada ya Serikali kulipa fidia kama ilivyokubaliana na mmiliki wa awali serikali iliweka utekelezaji wa mpango wa uendelezaji na usimamizi wa shamba hilo ambapo eneo la ekari 3,076.5 lilitengwa kwa ajili ya zao la mkonge.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga akiongea na baadhi ya wajumbe waliofika katika hafla fupi ya kusainiwa kwa mkataba wa mpango wa utekelezeji wa matumizi ya Shamba la Bwawani na Shambarai Burka liloko Wilaya ya Arusha na Arumeru mkoani Arusha.

Aidha, Kiongozi huyo wa Wizara ya Ardhi aliwaambia mashuhuda wa utiaji sahihi makubaliano hayo kuwa eneo la ekari 1,355 zimetengwa kama ardhi ya akiba na ekari 1,745 zilitengwa kwa ajili wananchi na mpango kina wa matumizi anwai ikiwemo ekari 673 zenye mashamba 513 yenye ukubwa wa ekari moja moja Shambarai Burka wilayani Meru.

Naye Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, Wilson Charles ameitaka Bodi ya Mkonge nchini pamoja na uendelezaji wa shamba hilo hususani eneo nla Bwawani kuangalia namna bora ya kuwezesha na kuinua hali ya wananchi akiwataja vijana kuwa walengwa muhimu katika ukuaji na uendelezaji uchumi katika Taifa.

Wakati huo huo Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Missaile Musa aliwataka watendaji wa halmashauri zote mbili kuhakikisha wanatenda haki wakati wa ugawaji ma maeneo ya makazi na mashamba ili kuepuka manunguniko na migogoro kati ya wananchi na Serikali.
Mkurugenzi wa Wilaya ya Arumeru, Mwalimu Zainabu Makwinya akisaini mkataba wa mpango wa utekelezeji wa matumizi ya Shamba la Bwawani na Shambarai Burka liloko Wilaya ya Arusha na Arumeru mkoani Arusha.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Ojugu Salekwa katika mchango wake juuu ya matumizi ya shamba hilo ameiomba Wizara ya Ardhi kuweka mpango bora wa matumizi ya ardhi iliyotengwa kama ardhi ya akiba ili wananchi wasivamie maeneo hayo na kuepusha usumbufu kwa wanasiasa na watendaji wa Mkoa wa Arusha.

Shamba hilo ambalo awali lilimilikiwa na Kampuni ya Tanzania Plantations Ltd lilikabidhiwa rasmi kwa Serikali tarehe 29, Aprili 2022 baada ya Serikali na kampuni hiyo kukamilisha taratibu za kisheria na baadae serikali kulipangia matumizi kwa ajili ya wananchi na sehemu ya shamba hilo kubaki kama ardhi ya akiba. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news