NA RAYMOND MUSHUMBUSI
WMJJWM
SERIKALI imewaonya wamiliki wa Makao ya kulea watoto nchini waliogeuza Makao hayo kujinufaisha kwa misaada mbalimbali inayotolewa hasa ya fedha.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu akisalimiana na baadhi ya Watoto wanaolelewa katika Makao ya kulea watoto ya Kijiji cha Matumaini mara baada ya ziara yake katika Makao hayo jijini Dodoma.
Onyo hilo limetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu alipotembelea Kijiji cha Matumaini kinacholea watoto jijini Dodoma Agosti 23, 2023.
Dkt. Jingu amesema kuwa baadhi ya wamiliki wa Makao ya kulea watoto wamekuwa wakifanya hivyo na hata kupiga picha za watoto kwa ajili ya kupata misaada ambayo haiwafikii wahusika na fedha zinazotolewa na wafadhili wenye mapenzi mema huzitumia kujinufaisha.
"Mnaotumia Makao ya Watoto kujinufasha tunawamulika, tutawafuatilia na tutawachukulia hatua kali kwa sababu mnakiuka Sheria na taratibu zilizopo. Huu ni wizi na ukatili dhidi ya Watoto na tunawahujumu waliotoka hiyo misaada,"alisisitiza Dkt. Jingu.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt.John Jingu akisikiliza maelezo kutoka kwa Msimamizi wa Makao ya kulea watoto ya Kijiji cha Matumaini,Sister Euphrasia Julius alipofanya ziara katika Makao hayo yaliyopo jijini Dodoma.
Dkt. Jingu ameongeza kuwa mtoto anatakiwa kulelewa na kutunzwa katika familia na jamii ila ikitokea mtoto amepata changamoto za maisha na kujikuta yupo katika mazingira ambao anakosa Malezi katika familia ndipo Makao yanatumika kuwalea.
"Mpaka sasa kuna jumla ya Makao ya kulea watoto 341 ambayo yanatoa huduma ya kulea watoto waliopatwa na changamoto zilizosababisha kutolelewa katika familia,"alisema Dkt. Jingu
Pia ameyataka Makao ya kulea Watoto nchini kuzingatia suala la Malezi hasa katika tamaduni na maadili ya kitanzania ili kujenga watoto walio na maadili mema hivyo kujenga taifa lenye maadili.
"Makao ya watoto sio biashara bali ni sehemu ya kuwasaidia watoto ambao hawajapata fursa za kulelewa katika familia, ni njia mbalada ya malezi kwa watoto wetu,"alisema Dkt.Jingu.
Vilevile amewataka wamiliki wa Makao ya Watoto ambao wameshindwa kuendesha Makao hayo wasing'ang'anie kukaa na watoto bali watoe taarifa kwa Maafisa Ustawi wa Jamii walipo katika maeneo yao ili watoto hao wapate sehemu nyingine watakazopata malezi.
Aidha, Dkt. Jingu ameupongeza uongozi wa Makao ya kulea watoto ya Kijiji cha Matumaini kwa kazi nzuri ya kuwalea na kuwatunza watoto waliopo katika Makao hayo kama watoto walio katika familia zao kwa kufuata Sheria na taratibu za uendeshaji wa Makao ya kuelea Watoto nchini.
Akisoma taarifa ya Kijiji cha Matumaini mmoja wa walezi wa Makao hayo, Sister Euphrasia Julius amesema kuwa Malezi ya Watoto katika Makao hayo ni ya Wana ndoa na kifamilia wa kujitolea kuwalea watoto bila kuwaasili kwa muda wakakaopenda ili watoto hao waweze kupata Malezi ya Baba na Mama kama watoto wengine katika familia.
Awali akimkaribisha Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Nandera Mhando amesema lengo ya kutembelea Makao ya Watoto ni kuangalia utendaji kazi wake na mazingira wanayolelewa Watoto kama yanakidhi vigezo, kanuni, miongozo, Sheria na madhumuni ya uanzishaji wa Makao ya kulea watoto.
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ipo katika ufuatiliaji wa Makao ya kulea watoto ambayo hayafuati Sheria na taratibu za uendeshaji wa Makao hayo nchini na itachukua Sheria kwa wamiliki wote ambao watabainika kufanya vitendo hivyo.