Serikali yazidi kuunga mkono maendeleo Musoma Vijijini

NA FRESHA KINASA

SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa fedha nyingi kutekeleza miradi mbalimbali ya elimu katika Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara ikiwemo kuchangia ujenzi wa Shule Shikizi ya Kitongoji cha Nyasaenge kilichopo katika halmashauri hiyo.

Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa Agosti 17,2023 na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, ambapo taarifa hiyo imeeleza jinsi wananchi wanavyoshukuru Serikali ya Awamu ya Sita na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Muhongo katika kuimarisha sekta ya elimu jimboni humo na kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali.

"Kitongoji cha Nyasaenge ni moja ya vitongoji sita vya Kijiji cha Kataryo. Kijiji hicho ni moja ya vijiji vitatu vya Kata ya Tegeruka ya Musoma Vijijini.

"Mwaka 2017, wananchi wakazi wa Kitongoji cha Nyasaenge waliamua kushirikiana na Mbunge wao, Prof.Sospeter Muhongo kujenga Shule Shikizi ili kutatua tatizo la watoto wao kutembea mwendo wa takribani kilomita 6-8 kwenda na kurudi kutoka masomoni kwenye Shule ya Msingi Kataryo,"imeeleza sehemu ya taarifa hiyo na kufafanua,

"Ujenzi wa awali wa gharama ya shilingi 49,086,500 (milioni 49.01) ulikuwa wa vyumba vya madarasa viwili, Ofisi ya Walimu moja, choo chenye matundu manne.

"Michango na nguvukazi ilitolewa na wana-Kitongoji cha Nyasaenge. Mbunge wao wa Jimbo alichangia saruji mifuko 100 na mabati 108."

"Baadae, Serikali ilitoa michango kama ifuatavyo: Mwaka 2021: EP4R: Tsh 46,600,000. Mwaka 2023: BOOST: Tsh 81,300,000. Tsh 50,000,000 (nyumba ya mwalimu)"

"Shule Shikizi Nyasaenge imetimiza vigezo vyote vya kuandikishwa kuwa shule ya msingi kamili- ombi liko kwenye Halmashauri yetu (Musoma DC)."imeeleza taarifa hiyo.

Rhoda Alex amesema, hatua ya Serikali kuchangia ujenzi wa shule hiyo utakuwa na manufaa makubwa kwa watoto ambao walikuwa wakitembea umbali mrefu hapo awali, watasoma karibu na kuondokana na changamoto hiyo huku akisema mchango wa Prof. Muhongo kusaidia ujenzi wa shule hiyo ni mkubwa sana.

"Tuna Mbunge ambaye dhamira yake ni kuifanya Musoma Vijijini iwe na taswira ya kipee hapa nchini, na ndio maana juhudi nyingi ameziweka kwenye kuimarisha maendeleo anatoa pesa na kuwashirikisha wananchi kushiriki katika maendeleo harambee nyingi anafanya na Serikali inatupenda imekuwa ikituunga mkono kutuletea fedha za maendeleo,"amesema Paul Faustine.

ZIARA YA CHAMA NA MBUNGE

"Jumatano ya Agosti 16,2023 Mwenyekiti wa CCM Wilaya, ndugu Denis Ekwabi aliongoza Kamati ya Siasa ya Wilaya kushirikiana na Mbunge wa Jimbo kukagua mradi huu wa ujenzi kwenye Shule Shikizi Nyasaenge."

"Vilevile, wananchi walipewa muda mwingi wa kuwasilisha kero na matatizo yao kwa viongozi hao walipewa majibu yaliyowaridhisha sana."imeeleza taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news