Serikali:Kwa mpango huu hakuna atakayeachwa nyuma

NA GODFREY NNKO

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imesema kuwa, huduma jumuishi za fedha ni miongoni mwa vipaumbele vya nchi katika kuinua uchumi na kuondoa umaskini kwa Watanzania .
Hayo yamesemwa leo Agosti 3, 2023 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Philip Mpango wakati akizindua Mpango wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa 2023 hadi 2028.

Ni kupitia hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) makao makuu ndogo jijini Dar es Salaam. 

Mheshimiwa Dkt.Mpango amesema, huduma jumuishi za fedha ni nguzo muhimu inayopaswa kuzingatiwa kwa kuhakikisha watu wa makundi yote wanafikiwa.

Pia ametoa wito kwa wataalam na wadau wa huduma jumuishi za fedha kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhakikisha wanaongeza kasi ya upatikanaji wa vitambulisho vya taifa ili kusaidia katika upatikanaji wa huduma rasmi za kifedha hususani kwa vijana. 

Makamu wa Rais amesema, watalaam hao wanapaswa kuhakikisha malengo yaliowekwa katika mpango huo wa tatu wa huduma jumuishi za fedha yanafikiwa kikamilifu ifikapo mwaka 2028.

Amesema, ni vema kuendelea na jitihada za kuimarisha ulinzi wa watumiaji wa huduma za kifedha dhidi ya uhalifu wa mtandaoni ili kuwajengea wateja imani ya kuendelea kutumia huduma hizo. 

Wakati huo huo, Makamu wa Rais Dkt.Mpango ametoa rai ya kupunguzwa kwa gharama za kutumia huduma rasmi za kifedha pamoja na kuongeza wigo wa dhamana ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo.
Makamu wa Rais ametoa wito wa kuongezwa na kurahisishwa kwa miundombinu ya malipo ya pamoja ili kuchochea matumizi ya huduma rasmi za fedha. 

Aidha amesema ni muhimu kuhakikisha upatikanaji wa mawasiliano kwa wote ili kupunguza matumizi ya fedha taslimu.

Utekelezaji wa mpango huo ambao umeanza leo unaenda sambamba na lengo muhimu la Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano ili kuhakikisha makundi ambayo hayajafikiwa wakiwemo vijana, wanawake, wajasiriamali, wakulima wadogo, wavuvi na makundi maalum wanafikiwa.

Waziri wa Fedha

Naye Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Nchemba amesema, Mpango wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha umeandaliwa kwa lengo la kuunganisha sekta binafsi na serikali ili kutatua changamoto za huduma jumuishi za fedha nchini. 

"Pongezi zimuendee Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan aliyeelekeza kukamilishwa kwa Mpango wa Tatu wa Huduma Jumuishi za Kifedha ambapo kama mlivyoona malengo yake yanalenga sekta za uzalishaji na makundi ambayo ni nguvu kazi katika kukuza uchumi wa nchi yetu.

"Mpango huu unalenga vijana na wanawake ambao ni nguvu kazi katika uzalishaji, lakini pia unalenga sekta zile za uzalishaji ambazo zinaajiri vijana wengi na zinaajiri watu wengi wa nchi yetu kuanzia kwenye kilimo, mifugo, uvuvi ambazo ni sekta zetu kuu kwenye uzalishaji.

"Lakini, pia makundi haya ambayo yametajwa ndiyo makundi ambayo ni nguvu kazi kubwa sana kwenye sekta binafsi katika nchi yetu,kwa maana hiyo mpango huu utaenda kuleta mabadiliko makubwa katika kukuza uchumi na kuondoa umaskini kwa Watanzania."

Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba amesema, mpango huo utasaidia kuongeza uelewa wa masuala ya huduma za fedha na kuongeza matumizi ya simu janja sambamba na kuhakikisha usalama wa wateja.

Pia, ametoa wito kwa wadau wa huduma jumuishi za fedha wa ndani na nje ya nchi kushirikiana wakati wa utekelezaji wa mpango huo wa tatu wa taifa ili kusaidia nchi iweze kupiga hatua katika kufikia malengo ya huduma jumuishi za fedha.

Gavana Tutuba

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Huduma Jumuishi za Fedha ambaye ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema, utekelezaji wa mpango huo utaongeza upatikanaji wa vituo vya utoaji huduma za fedha katika maeneo ya vijijini.

Pia amesema, mpango huo utapanua wigo mkubwa wa matumzi ya huduma za fedha kwa kuongeza machaguo na kuimarisha masuluhisho ya huduma kulingana na mahitaji ya wateja nchini.
"Leo umekuwa ni uzinduzi wa Mpango huu wa Tatu wa Huduma Jumuishi za Kifedha ambao umezinduliwa na Mheshimiwa Makamu wa Rais, Dkt.Philip Isdor Mpango kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, katika uzinduzi huu,kama mlivyoona ulikuwepo mpango wa kwanza, mpango wa pili, ambayo imetekelezwa kwa kiwango cha juu.

"Na wakati tunafanya maandalizi ya kuandaa mpango huu wa tatu, tulifanya kwanza tafiti na katika utafiti ule ulizinduliwa mwezi uliopita ulithibitisha kwamba, kiwango cha upatikanaji wa huduma rasmi za kifedha umefikia sasa asilimia 76.

"Ikiwa ni asilimia moja zaidi ya lengo lilokuwa limewekwa la asilimia 75 ifikapo 2023. Kwa hiyo, tumefikia malengo na tumeyapita kwa asilimia moja, ikiwa ni jitihda za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kufanya ujumuishi wa huduma hizi katika maeneo mbalimbali.

"Unapoongelea huduma hizi za kifedha ambazo ni moja wapo ya utekelezaji wa ile Financial Sector Development Plan ambayo ilianza kutekelezwa mwaka 2020 na itaishia mwaka 2030, lakini katika maeneo mbalimbali yaliyoainishwa kuna maeneo makubwa kama sita ambayo yamegusia sekta ndogo ya fedha au ya mabenki.

"Unaongelea pia, upande wa Bureau de Change, microfinance,masoko ya mitaji na hisa, bima, na pia tunaongelea upande wa mifuko ya hifadhi za jamii. 

Kwa hiyo ukiangalia maeneo yote yanaleta fursa kwa wananchi kuhakikisha kwamba katika utekelezaji wa shughuli zao, kila mmoja anaweza kuzifikia fedha au akazipata na kuendelea kufanya majukumu yake ili kujipatia kipato, lakini kuongeza ukuaji wa uchumi.
"Sasa, katika utekelezaji wa ule mpango wa kwanza, na mpango wa pili, tumekuwa zaidi tukijielekeza katika namna ya kuwafikia watu, tunasema access katika ufikiaji wa au utoaji wa huduma rasmi.

"Lakini, suala jingine tunalojaribu kuangalia ni namna sasa ya kupanua wigo ili kila mmoja aweze kufikiwa, sasa kwenye suala la kuwafikia watu, mmeona kuna changamoto mbalimbali licha ya kwamba tumefikia mafanikio yale ya asilimia 706 ikiwa ni asilimia moja juu ya lengo la asilimia 75 lilikuwa limepangwa.

"Sasa, katika utekelezaji kuna maeneo ambayo yanagusa vikundi kama sita ambavyo Mheshimiwa Waziri amevigusia na ukiangalia katika makundi yote kila watu kuna changamoto zao, lakini kwa ujumla zile changamoto zinataka kama kufanana.

"Suala kama la dhamana limeongelewa karibu na makundi yote, suala la usajili kuwa na zile nyenzo za kufikia usajili wenyewe tumeona kuna changamoto zimejitokeza, na katika mpango huu tumejipanga kuona namna ambavyo tutaweza kufikia wananchi wote kwa pamoja.

"Ndiyo maana tunapoongelea suala la ujumuishi, tunatazama namna tutakavyofanya mikakati yetu ili tuwafikie wananchi wote, na tumejiwekea sasa lengo kwamba kuanzia sasa 2023 kwa kipindi cha miaka mitano mpaka mwaka 2028 tuwe tumewafikia wananchi katika zile huduma rasmi.

"Tuongeze kiwango kutoka zile asilimia 76 za sasa mpaka asilimia 85 ifikapo mwaka 2028, sasa namna gani ya kuwafikia?. 

"Ukiangalia mpango huu, umebainisha changamoto katika makundi mfano kuna kundi kama la wanawake, katika wasilisho tumesikia mikakati mbalimbali na namna ambavyo wizara zinazohusika na kufungua fursa kwa wanawake zimebainisha na sisi kama sekta ya fedha tutahakikisha kwamba tutashirikiana nao.

"Kuna eneo kama la shughuli za vijana, wameonesha namna ambavyo Serikali itaendelea kuweka mifumop rasmi ya kuwasajili ili watu waweze kupata hizo huduma za kifedha licha ya changamoto zilizoongelewa,katika uzinduzi huu wa leo tumeona shuhuda ambazo zimetolewa na vijana, lakini katika mawasilisho ya wadau nao wameonesha mikakati namna watakavyoweza kuwafikia.

"Kuna kundi labda la wajasiriamali, kweli kuna changamoto mbalimbali, lakini pia mpango huu umeainisha namna ambavyo wajasirimali pia watafikiwa na zile huduma rasmi ili waweze hata kurasimisha shughuli au huduma zao, kwa sababu kuna wajasiriamali ambao wanafanya biashara katika mazingira ambayo si rasmi.

"Kwa hiyo, kama wataweka mifumo rasmi basi wataweza pia kupata hizo huduma za kifedha katika mifumo ambayo ni rasmi, kuna labda wavuvi na wakulima tumeona kwa upande wa wavuvi walikuwa na changamoto zao.

"Lakini wameonesha namna ambavyo hata katika uchumi wa buluu ambao labda shughuli ao wanakwenda kufanya katikati ya maji ili waje na vitoweo wamekuwa hawaaminiki, kwa hiyo tutaweka mifumo rasmi itakayoweza kuwabainisha, na kuwapa taarifa ili waweze kufikiwa na huduma hizo.

"Kwa hiyo, katika makundi yote aliyokuwa ametaja Mheshimiwa Waziri makundi yale sita kila kundi litatafutiwa namna ambavyo litapewa fursa ya kufikiwa na hizo huduma. 
"Kwa ujumla niseme kwamba, mpango huu ambao umeanza leo mpaka mwaka 2028 sisi kama kamati au kama Baraza la Kitaifa linalosimamia Huduma Jumuishi za Kifedha tutaendelea kushirikiana na wadau wote wa sekta ya umma na sekta binafsi pamoja na washirika wa maendeleo na wananchi wote kwa ujumla ili kila mmoja tumuwekee namna ambavyo kulingana na majukumu yao au kulingana na fursa zilizopo aweze kufikiwa.

"Kwa hiyo, nitoe wito kwa Watanzania wote kila mmoja kwa namna yake aweze kufahamu kwamba kuna hizi huduma za kifedha, atafute namna ambavyo atazifanya ziwe rasmi ili hatimaye ziweze kumfikia na kila mmoja awe tayari ili huduma hizi ziweze kumfikia.

"Kwa sababu asipokuwa tayari mwenyewe inawezekana hizo fursa zikampita pembeni. Kwa hiyo kila mmoja ajiandae, arudi kwenye mifumo rasmi ajue fursa zilizopo na aweze kuzifikia katika mifumo hiyo iliyo rasmi,"amefafanua kwa kina Gavana Tutuba huku akisisitiza kuwa, hakuna atakayeachwa nyuma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news