Sheikh Mwaipopo atoboa siri kuhusu Dkt.Slaa na wenzake

DAR ES SALAAM-Sheikh Said Mwaipopo amewataka Watanzania kutambua kuwa, kukamatwa kwa Balozi mstaafu, Dkt.Willbroad Slaa,Wakili Boniface Mwambukusi na Mdude Nyangali hakuna uhusiano wowote na misimamo yao kuhusu uwekezaji wa bandari nchini.

Mwaipopo ambaye ni Katibu wa Baraza la Habari la Kiislamu (BAHAKITA) ameyabainisha hayo leo Agosti 17,2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. 

"Wamekamatwa na baada ya kukamatwa, kumekuwa na maneno ambayo yamekuwa yakitengenezwa, ninataka nizungumze wazi na Dunia ijue na Watanzania tujifunze sana kusimamia haki na kusimamia ukweli. 

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Mwabukusi na Mdude waliokamatwa Agosti 12,2023 Mikumi mkoani Morogoro na wanashikiliwa kwa tuhuma za kutoa kauli za uchochezi, huku Dkt. Slaa aliyekamatwa Agosti 13,2023 jijini Dar es Salaam akishikiliwa kwa tuhuma hizo.

"Nimesikia juzi chombo kimoja au Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba,dada yangu Nkya na baadhi ya wataalamu wengi wa kisheria kupitia Kituo cha Haki za Binadamu, wanasema kwamba Dkt.Slaa, Mwambukusi na Mdude wamedhulumiwa na wamekamatwa kwa sababu ya misimamo yao ya kutetea suala la uwekezaji.

"Maneno haya ndugu zangu kama ninyi viongozi ambao mnasema na kila siku mnazungumzia sheria, haya maneno ni ya uongo, si ya ukweli.

"Tuzungumze tu ukweli,halafu tutawaachia Watanzania watachuja na wataamua,hawa watu hawakukamatwa kwa sababu ya kuzungumzia masuala ya bandari,mikataba ya DP(DP World), hawakukamatwa kwa sababu hiyo, tufike mahali Watanzania tuwe wakweli.

"Ipo clip humu kwenye simu yangu, anazungumza Mheshimiwa Dkt.Willbroad Slaa (ninaweza kuwapa ushaidi). Wilbroad Slaa ambaye ni mtu mzima amekuwa Balozi anazungumza anasema sasa wanataka walihamshe dude,kufanya maandamano.

"Na anasema wazi kwamnba tutaipindua Serikali,tutaiwajibisha Serikali na baadae kuna clip ya pili ya ndugu yetu Mdude amekwenda mbali amezungumza wazi kwamba anakuja Dar es Salaam kuandaa mikakati maalumu ya kufanya maandamano.

"Maandamano hayo atahakikisha yanaanzia Dodoma, Dar es Salaam yatakwenda kwenye ofisi za Serikali ambao ni wezi, amesema hivyo na mimi ninajua anayethibitisha wizi wa mtu ni Mahakama.

"Yeye alisema, ataingiza maandamano kwa viongozi wa Serikali ambao ni wezi na baada ya hapo amesema, wavamie vituo vya polisi wapige moto, waue watu.

"Amesema, wavamie ofisi za CCM, bahati nzuri mimi si msemaji wa chama,ninanukuu maneno aliyoyasema, hata kama atasema angevamia hoteli, au atavamia nyumba ya kulala wageni-guest house au atavamia mgahawa wowote, bado ni kosa linabaki kuwa kosa.

"Kwa maneno haya tu aliyoyasema,Nyangali Mdude akiyatoa ndani ya kinywa chake kama mwanasiasa na akihamasisha watu wafanye uhalifu huo wa kupindua Serikali kwa njia ya maandamano, inatosha wazi kuwa mhalifu na inatosha wazi hata Jenerali wa Polisi kuwakamata, kwa sababu nchi hii ina vyombo vya kisheria, ina vyombo vya ulinzi na usalama.

"Ina vyombo vya dola, na Jeshi la Polisi kazi yake ni kukamata, kuhoji, kupekuwa na kufikisha mahakamani.

"Sasa nimeanza kupata wasiwasi kwamba, nimemsikia dada yangu Nkya pale anasema yeye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, lakini Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba huyu na watu wa haki za binadamu wanasema wao wanasimamia haki za binadamu, Serikali imekosea kuwakamata.

"Lakini, hiyo haki ya binadamu inakuwa kwa wale wahalifu tu, haki ya binadamu haiko kwa upande mwingine? Kama kweli ni suala la mkataba wa bandari,kwenda kuvamia vituo vya polisi na kuhamasisha watu kulikuwa kunahusiana vipi na mambo ya uwekezaji.

"Uwekezaji wa bandari hakuingia polisi, wala IJP (Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania),wala RPC wa Polisi, ni Serikali na DP.

"Haya polisi ulikuwa unawaingiza nini, na kazi ya polisi ni kutulinda mimi na wewe unayeandamana, haya CCM ambao ulisema utavamia ofisi zao upige moto, uue watu? Halafu unasema watu wameonewa.

"Vyombo vinavyotetea haki za binadamu vinapaswa kutambua kuwa, haki za binadamu hazipo kwa wahalifu tu, angalieni na upande wa pili, wangeleta hawa watu madhara gani.

"Kwa sababu wametamka wao kwamba wanataka waipindue Serikali,haya wanasema wanataka waandamane wakavamie vituo vya polisi, hivi kwa akili ya kawaida vituo vya polisi vina akiba ya silaa na hatujui watavamia vituo wakiwa wamejiandaa vipi, je? Wangetakiwa watu kuvamia vituo vya polisi wakapora silaa wangeleta madhara gani katika nchi?.

"Halafu wanasheria mnasimama mnasema kuna wanasheria 100 wanakwenda kuwatetea, hata wangewatetea haki itabaki ile ile kwamba wamefanya kosa, na kukamatwa ni haki yao.

"Niwaulizeni, hao wanasheria 100 watetea vipi hiyo kesi? Kwa sababu ni mambo ya kushangaza na ndiyo ujue kwamba watanzania tuna matatizo, wanasheria 100 wakatetee kesi moja, hiyo kesi wanaitetea vipi?

"Sasa msitufanye Watanzania kama ni watu wajinga, kutishiwatishiwa masuala ambayo hayaingii akilini, kwa hiyo ninataka niufahamishe ulimwengu na Dunia ijue hawa watu hawakukamatwa kwa sababu ya kupinga uwekezaji.

"Wamekamatwa kwa maneno yao machafu, ambayo hayavumiliki duniani kokote, Serikali yoyote hata iwe Serikali yangu, ni sawa na mtu kukaa nje ya nyumba yako anasema anafanya maandalizi ya kuvamia nyumba yako,nikifika nyumbani nitaua mkeo, watoto kwa mtu mwenye akili lazima umdhibiti kuingia nyumbani kwako kabla hajaleta madhara.

"Sasa, IJP lazima tumpongeze na vyombo vyote vya ulinzi na usalama kuwawahi hawa watu,hatujui walikuwa na lengo la mapinduzi ya namna gani,"amefafanua kwa kina Sheikh Mwaipopo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news