Shirika la Posta Tanzania (TPC) watembea kifua mbele

NA GODFREY NNKO

SHIRIKA la Posta Tanzania (TPC) limesema,mwaka uliopita wa 2022/2023 ulikuwa ni mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa mpango mkakati wao wa nane wa kibiashara (2022/2023-2025/2026).

Ni mkakati unaolenga kuifanya Posta ya Kidijitali kwa Biashara Endelevu katika uchumi wa kidijitali ifikapo mwaka 2025/2026.

Hayo yamebainishwa leo Agosti 14,2023 na Postamasta Mkuu,Macrice Daniel Mbodo katika kikao kazi baina ya shirika hilo na wahariri wa vyombo vya habari chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Kikao hicho kimefanyikia Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam ambapo ni mwendelezo wa vikao vinavyolenga kuyaleta pamoja mashirika na taasisi zinazosimamiwa na ofisi hiyo ili waeleze umma walipotoka,walipo na wanapoelekea.

Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu amekuwa akisisitiza kuwa, kiu yake kubwa ni kuona taasisi na mashirika hayo yanafanya kazi kwa ufanisi na kwa maslahi ya nchi.

Aidha,Postamasta Mkuu,Macrice Daniel Mbodo ameeleza kuwa,katika mwaka huu wa kwanza wa utekelezaji wa mpango mkakati wao wa kibiashara, wamepata mafanikio mengi katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Uzalishaji wa Mapato na Faida

Posta Mastamkuu amefafanua kuwa, mwaka 2022/2023 wamezalisha mapato ya jumla ya shilingi 33.7 bilioni.

Amebainisha kuwa, mapato hayo ni ongezeko la asilimia 3.4 ikilinganishwa na mapato halisi yaliyozalishwa mwaka 2021/22 ambayo yalikuwa shilingi 32.6. bilioni.

"Faida kabla ya kodi tuliyozalisha ni shilingi 2.08 bilioni sawa na ongezeko la asiilimia 16 ikilinganishwa na faida iliyozalishwa mwaka 2021/22 ambayo ilikuwa shilingi 1.79 Bilioni,"amefafanua.

Utoaji wa huduma kidigitali

Kwa upande huu, Posta Mastamkuu amefafanua kuwa,shirika hilo limefanikiwa kuanzisha na kuzindua mfumo na programu tumizi ya Posta Kiganjani.

Lengo likiwa ni kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma za posta na biashara kupitia simu janja ambapo program hii inapatikana kupitia google play store na app store.

Aidha, amesema wamewezesha maduka zaidi ya 1200 kuuza bidhaa mbalimbali ndani na nje ya nchi kupitia duka lao mtandaoni.

Sambamba na kutangaza vivutio mbalimbali vya Tanzania kupitia stempu maalum za vivutio vikuu vitano vya Tanzania (Big Five).

"Ni tulizozizindua na kuziweka kwenye duka letu mtandao la stempu linaloonekana na kupatikana nchi zote duniani ili kuunga mkono jitihada za Serikali yetu za kuwavutia watalii."

Usalama wa bidhaa za wateja

Postamasta Mkuu,Macrice Daniel Mbodo amesema, katika kipindi cha mwaka 2022/2023 shirika hilo limeendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa mali za wateja kwa kuongeza mitambo mitatu ya kisasa ya ukaguzi wa mizigo.

Pia,kuongeza kamera za kisasa (CCTV Camera) 200 kwenye ofisi mbalimbali za shirika Bara na Zanzibar. "Kamera 200 zimenunuliwa na zimeshafungwa ofisi mbalimbali nchini."

Sensa

Aidha, amesema shirika hilo lilishiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi 2022. "Shirika limefanikiwa kushiriki katika kufanikisha zoezi la sensa ya watu na makazi kwa kusafirisha na kusambaza vishikwambi na vifaa vingine vyote vya sensa nchi nzima (Tanzania Bara na visiwani).

Mbali na hayo amesema,shirika limefanikiwa kusafirisha sampuli za kibaiolojia nchi nzima kutoka vituo vya afya vya kuchukulia sampuli na kwenda maabara za vipimo na kisha kurejesha majibu kwa wananchi waliochukuliwa vipimo kwa wakati.

Posta Masta Mkuu amefafanua kuwa,pia shirika limeendelea kusimamia vituo viwili vya Huduma Pamoja (Dar es Salaam na Dodoma) na kuanzisha vituo vitatu vipya Tanga, Mbeya na Mwanza.

Amesema,kupitia vituo hivyo, kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 zaidi ya wananchi 100,000 wamehudumiwa huduma mbalimbali ikiwemo huduma za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA).

Nyingine ni Uhamiaji Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA),Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Mfuko wa PSSF,Jeshi la Polisi Tanzania na wengineo.

Pia amesema, wamefanikiwa kuimarishaji wa mtandao wa usafirishaji kwa njia ya posta. "Ili kuhakikisha tunakidhi vionjo vya wateja wetu, tumeimarisha mtandao wetu wa usafirishaji kwa kuongeza magari 14 kwa njia ya barabara,

"Kuingia mikataba ya usafirishaji na kampuni mbalimbali za meli na ndege ndani na nje ya nchi kama vile Azam Link, Zan Fast Feries, ATCL, KLM na wengineo."

Wakati huo huo, Posta Mastamkuu amefafanua kuwa, kutokana na ufanisi wao wamepata uwezeshaji kutoka Umoja wa Posta Duniani.

"Shirika limepata fedha jumla ya dola 120,000 kutoka Umoja wa Posta Duniani kwa ajili ya kutengeneza mfumo wa utumaji na upokeaji fedha ndani na nje ya nchi kwa njia ya kielektroniki (posta cash ewallet) ambapo ujenzi wa mfumo huu unaendelea."

Aidha, amebainisha kuwa, Umoja wa Posta Duniani umeliamini shirika kwa kuanzisha ofisi zake mbili ndani ya jengo la makao makuu ya Posta ya Tanzania.

Ofisi ya kwanza, Posta Masta Mkuu amesema ni Ofisi ya Umoja wa Posta Duniani ya kutegemeza Teknolojia ya Mifumo ya Umoja wa Posta Duniani kwa nchi zote Afrika zinazoongea Kiingereza na Msumbiji.

Amesema,mkuu wa ofisi hiyo ni Mtanzania na ni mtumishi wa Shirika la Posta,Aicha Nangawe. "Kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 Posta ya Tanzania kupitia ofisi hii imesapoti nchi 15 za Afrika."

Ofisi ya pili amesema, ni ofisi ya Umoja wa Posta Duniani ya kusimamia miradi yote ya Umoja wa Posta Duniani kwa ukanda wote wa Afrika Mashariki ambapo mkuu wa ofisi hii pia ni Mtanzania na mtumishi wa shirika hilo,Tumaini Nguto.

Wakati huo huo, Posta Mastamkuu amesema, msimamizi wa miradi ya Umoja wa Posta Duniani hapa nchini ni Mtanzania,Selemani Mwarabu.

Shirika la Posta Tanzania lilianzishwa kwa Sheria Na.19 ya mwaka 1993 baada ya kuvunjwa kwa lililokuwa Shirika la Posta na Simu Tanzania na lilianza kazi rasmi Januari Mosi, 1994.

Aidha,Shirika la Posta linamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100, hivyo ni shirika la watanzania kwa asilimia zote 100.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news