NA VERONICA MWAFISI
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewataka Makatibu Tawala wa Wilaya kutekeleza majukumu yao kikamilifu ikiwepo kusimamia suala la nidhamu ili kutenda haki na kuondoa changamoto za kiutumishi.
Mhe. Simbachawene amesema hayo alipokuwa akizungumza na watumishi wa umma wa Wilaya ya Kwimba, Mkoa wa Mwanza wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji na kutatua kero na changamoto zinazowakabili watumishi wa umma katika Wilaya hiyo.
“Makatibu Tawala, msidhani ya kuwa mamlaka ya nidhamu hayapo kwenu, mmechaguliwa kuwa viongozi kwa lengo la kuondoa changamoto kati ya waajiri na waajiriwa, hivyo mna jukumu kubwa la kusimamia suala hilo,” amesisitiza Mhe. Simbachawene.
Aidha, Mhe. Simbachawene amesema ni vema viongozi wa Wilaya wakafahamu changamoto mbalimbali za watumishi na wananchi na kuzishughulikia ili kuondoa tabia ya baadhi ya watumishi kutaka kuchukua majukumu ambayo hawahusiki nayo.
Akitoa neno la shukrani, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Mhe. Ng’wilabuzu Ludigija amemshukuru Waziri Simbachawene kwa kufanya ziara ya kikazi katika Wilaya yake na kuzungumza na watumishi kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji ambapo ameahidi kwa kushirikiana na watumishi wa wilaya hiyo watatekeleza maelekezo yote ambayo amewaagiza.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene yupo katika ziara ya kikazi mkoani Mwanza yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Miradi ya TASAF.