NA FRESHA KINASA
KUFUATIA juhudi kubwa za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Suluhu Hassan katika Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara wananchi wa Kijiji cha Kigera Etuma ambao ni wachimbaji na wafugaji wameishuru Serikali kwa kuwajengea shule ili wanafunzi wasome karibu na makazi yao.
Hatua hiyo, imemuibua pia Mzee Kiunya ambaye ni mkazi na mzaliwa wa Kitongoji cha Kusenyi kwa furaha tele baadaya ya kupata shule kwenye kitongoji chao jambo ambalo pia wananchi wamelipokea kwa shangwe na wamemuombea baraka na neema Rais Dkt.Samia, Mwenyezi Mungu amjalie katika uongozi wake.
Ambapo mzee huyo amemtuma Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo ampeleke Katika Kitongoji hicho Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akafungue shule hiyo inayokamilishwa ujenzi wake aweze kumuona kwa macho yake kabla hajafa.
Kwa upande wao wananchi wa kijiji hicho wamesema kuwa, katika kipindi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan maendeleo makubwa yamefanyika jimboni humo ikiwemo ujenzi wa shule hiyo ambayo itawasaidia wanafunzi kusoma karibu na hivyo kuongeza ufanisi wa masomo yao.
Magreth Lugembe ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kigera 'B' amesema, kujengwa kwa shule hiyo kutainua ufaulu wa wanafunzi Kupanda na kuimarisha mahudhurio yao.
Pia, Mwalimu huyo amemshukuru Rais Dkt.Samia na Mbunge wa Jimbo hilo kwa kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo hilo kwani mbali na kuimarisha sekta ya elimu, maendeleo katika Nyanja mbalimbali yameendelea kufanywa.
Malele John Diwani wa Kata ya Nyakatende amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imeupiga mwingi kwa kutoa fedha nyingi za maendeleo ambazo zimeleta mageuzi chanya kwa wananchi na hivyo amemshukuru Prof.Muhongo na Rais Dkt.Samia kwa kuwapa heshima wananchi kupitia miradi inayogusa maisha yao.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Vijijini, Denis Ekwabi amemshukuru Prof.Sospeter Muhongo kwa jinsi anavyotekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kuwatumikia wananchi jimboni humo kwa moyo wa dhati na kuchapa kazi kwa bidii akishirikiana na chama na wananchi.
"Tumejenga shule,zahanati na vituo vya afya tulikuwa na kituo kimoja cha afya tarafa ya nyanja. Tumejenga Hospitali ya Wilaya Kwikonero Suguti ndugu zangu Prof. Muhongo atupe nini."amesema Ekwambi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini iliyotolewa Agosti 23, 2023 imesema kuwa,"Kijiji cha Kigera cha Musoma Vijijini kimepokea shilingi 348,500,000 kutoka serikalini.
"Fedha hizo ni kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi mpya (Mradi wa BOOST) ambayo itakuwa ya pili, na inajengwa kwenye Kitongoji cha Kusenyi,"imeeleza taarifa hiyo na kusema.
"Mzee Kiunya, mzaliwa na mkazi wa Kitongoji cha Kusenyi, kwa furaha tele ya kupata shule kwenye kitongoji chao, amemtuma Mbunge Prof Muhongo ampelekee hapo kitongojini Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akafungue shule hiyo inayokamilishwa ujenzi. Mzee huyo ameongea kwa lugha ya Kikwaya."