DAR ES SALAAM-Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe Albert Chalamila, Agosti 17,2023 amevunja uongozi wa Soko la Mabibo na kuagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi wa kina katika soko hilo na watakaobainika hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
RC Chalamila ametoa agizo hilo alipofika katika soko hilo kutatua mgogoro baina ya wafanyabishara biashara wasiowaaminifu wakiongozwa na Uongozi wa Soko hilo na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.
Aidha,RC Chalamila amekemea watu wachache, wabinafsi, katika soko hilo kukwamisha jitihada za serikali na kamwe wasijaribu hata kidogo kwani masoko lazima yaboreshwe Serikali ikusanye mapato yake na wafanyabishara wafanye biashara zao sehemu rafiki.
"Hatuwezi kuacha watu wachache wanajinufaishe na Serikali inakosa mapato, Mkurugenzi wa Manispaa anza kazi leo,"alisema Chalamila.
Hata hivyo, RC Chalamila amebainisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan dhamira yake ni kuboresha masoko tayari kiasi cha milioni 600 kimetengwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kwa ajili ya kuanza kazi ya kuboresha soko hilo.
Vilevile Mkuu wa Mkoa amesema, uongozi uliokuwepo ulikuwa ukikusanya fedha nyingi, lakini zilikuwa zikiishia katika matumbo ya watu wachache badala ya kuwanufaisha walio wengi.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Hashim Komba ameweka bayana Changamoto zilizoko katika soko hilo na kuonyesha dhamira ya wilaya yake kutaka maboresho ya soko hilo muhimu kwa masilahi mapana ya Umma.