ALGIERS-Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria zimesaini Hati nane za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta za umeme, gesi, biashara, viwanda na kilimo, utamaduni na sanaa, kumbukumbu na nyaraka, mafunzo katika vyuo vya diplomasia na ushirikiano katika taaluma na teknolojia.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf wakisaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika mafunzo ya diplomasia kati ya Chuo cha Diplomasia cha Tanzania (CFR) na Chuo cha Diplomasia cha Algeria wakati wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria uliofanyika tarehe 30 Julai 2023 hadi 1 Agosti 2023 jijini Algiers, Algeria.
Utiaji saini wa makubaliano hayo umeshuhudia na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria wakati wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Algeria.
Mkutano wa Mawaziri ulitanguliwa na Mkutano Ngazi ya Maafisa Waandamizi uliofanyika tarehe 30 hadi 31 Julai 2023.
Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huu umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax. Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe na Naibu Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mambo ya Ndani ya Nchi, na Nishati
Madhumuni ya mkutano huo ni kutathmini hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa masuala mbalimbali ya ushirikiano yaliyokubaliwa kwenye Mkutano wa Nne uliofanyika mwaka 2010 jijini Dar es Salaam.
Akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Waziri Tax ameleza kuwa mkutano huu ni kielezo cha dhamira ya dhati kati ya Tanzania na Algeria kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo na kuweka mfumo rasmi wa kujitathimini katika masuala mbalimbali yaliyokubalika.
‘’Ni imani yangu kuwa wataalam wetu wamefanya kazi kubwa katika majadiliano kwa kuangalia maeneo muhimu na ya kipaumbele ili kuendelea kukuza ushirikiano kwa maslahi ya nchi zote mbili,"alisema Dkt.Tax.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf katika hotuba yake ameeleza kuwa mkutano huo umetoa fursa ya kujadili na kukubaliana maeneo ya kipaumbele kwa maslahi ya pande mbili.
Pia ameeleza kuwa kusainiwa kwa makubaliano ni ishara ya wazi kuwa nchi hizi zitaendelea kudumisha uhusiano mzuri uliopo sanjari na kukuza ushirikiano kwenye maeneo mapya yenye tija.
Matukio katika picha juu yakionesha viongozi kutoka sekta za ushirikiano kati ya Tanzania na Algeria wakisaini Hati za Makubaliano na Mikataba ya Ushirikiano wakati Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria uliofanyika tarehe 30 Julai 2023 hadi 1 Agosti 2023 jijini Algiers, Algeria.
‘’Serikali ya Algeria itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya kazi pamoja ili kufikia malengo tuliyojiwekea katika sekta mahsusi za ushirikiano,’’ alisema Mhe. Attaf.
Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Attaf wamewashukuru Wakuu wa Nchi wa pande zote mbili kwa utayari na jitihada zao wanazozifanya katika kuhakikisha ushirikiano uliopo unaimarishwa zaidi kwa maslahi mapana ya nchi mbili.
Mkutano huo umejadili na kutathimini utekelezaji wa maeneo ya ushirikiano katika Siasa na Diplomasia, Ulinzi na Usalama, Fedha na Uchumi, Nishati, Habari na Mawasiliano, Kilimo, Elimu na Mafunzo, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Utalii, Kilimo na Uvuvi na Afya, na Sanaa na Utamaduni.
Katika kuendelea kuhakikisha kwamba Tanzania na Algeria zinatekeleza maazimio ya mkutano husika, nchi hizi mbili zimekubaliana kuitisha mkutano wa sita utakaofanyika nchini Tanzania mwaka 2025.