DAR ES SALAAM-Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)imeupongeza uongozi wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini TARURA kwa kukamilisha miradi kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora.
Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI ilipo kagua miradi inayotekelezwa na TARURA katika Mkoa wa Dar Es Salaam.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa kamati ya TAMISEMI Mhe. Dennis Londo ameeleza kuwa miradi iliyotembelewa imekamilika kwa wakati na kwa ubora na kwamba itasaidia kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi.
"TARURA Mkoa wa Dar Es Salaam
wanafanya kazi nzuri, miradi imekamilika kwa wakati na itasaidia
kurahisisha shughuli za wananchi kiuchumi na Kijamii,"amesema Mhe.
Londo.
Kuhusu Halmashauri zenye mapato ya ndani yanayozidi
Billioni tano kutakiwa kuchangia asilimia kumi ya fedha za maendeleo
katika ujenzi wa Barabara,Kamati hiyo imeonesha kuridhishwa na
Halmashauri za Mkoa wa Dar Salaam kwani tayari zote zimetekeleza agizo
hilo la Serikali na tayari zimetoa fedha hizo kwaajili ya ujenzi wa
Barabara.
Kwa upande wake Mhe. Salome
Makamba (Mb) ambaye pia ni mjumbe wa Kamati hiyo ameeleza kufurahishwa
na kazi zinazofanywa na TARURA huku akitoa wito kwa wananchi kuhakikisha
wanaitunza miundombinu iliyojengwa ili iweze kutumika kwa muda
uliokusudiwa.
"Kazi iliyofanyika chini ya TARURA ni kubwa lakini
niwasihi wananchi kuhakikisha wanaitunza miundombinu hii ili iweze
kutumika kwa muda uliokusudiwa na kuleta tija katika nchi kiuchumi na
Kijamii."
Naye Mkurugenzi wa Barabara kutoka TARURA mhandisi Venanti Komba amesema kuwa ushauri wa Kamati hiyo umechukuliwa na utafanyiwa kazi ili kuendelea kuboresha na kuwapatia huduma ya usafiri na usafirishaji wananchi.