NJOMBE-Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ((Tanzania Forest Services (TFS) Agency) wataendelea kutunza na kuendeleza utamaduni kupitia Utalii wa Ikolojia nchini.
Hayo yamebainishwa Agosti 25, 2023 na Waziri wa Sanaa,Utamaduni na Michezo,Mheshimiwa Balozi Dkt.Pindi Chana katika ufunguzi wa Tamasha la Pili la Taifa la Utamaduni katika viwanja vya Stendi ya Zamani mkoani Njombe.
Akizungumza katika ufunguzi wa tamasha hilo,Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kuwa, lengo kuu la tamasha hilo ni kuhakikisha kwamba kama watanzania tunao wajibu wa kuzilinda na kuziendeleza tamaduni za nchi yetu na hata Afrika kwa ni ndio njia pekee ya utambulisho wa utanzania.
"Watu kutoka nchi mbalimbali wamekua wakiuliza kwa nini watanzania tumekuwa tunaishi kwa amani lakini majibu ya haya yote ni kutokana na utamaduni tuliojiwekea na ambao tunaendelea kuuihifadhi," alisema Waziri Balozi Dkt.Chana.
Amesisitiza pia watanzania kuendelea kutunza na kutumia tamaduni ambazo tumejiwekea zinazosisitiza maadili mema katika jamii ili kuitunza amani tuliyonayo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Wakala Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania inashiriki katika Tamasha hili la utamaduni la kitaifa la kuonyesha pia ni kwa jinsi gani inashiriki katika kukuza na kihifadhi utamaduni zilizopo Tanzania hasa katika jamii mbalimbali .
Akizungumza na baadhi wananchi waliotembelea katika banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania - TFS, Mhifadhi Mwandamizi Kelvin Fella amesema kuwa utamaduni unaelezea maisha ya ujumla ya mwanadamu na kazi zote anazozifanya kila siku.
Amesema kuwa, kama TFS yapo maeneo ambayo ambayo yanahifadhi utamaduni wa watanzania na waafrika kwa ujumla kama vile maeneo ya Malikale ambayo yanaelezea tamaduni mbalimbali ambazo jamii huzifanya.
"Tunayo maeneo ya hifadhi za malikale katika vituo vya mji mkongwe Bagamoyo, Kaole pamoja na Kondoa Irangi ambazo zote hizi zinahifadhi utamaduni wa Watanzania ambapo imekuwa ni sehemu ya kukumbusha maadili yayotakiwa katika jamii zetu,"amesema Mhifadhi Mwandamizi.
Ameongeza kuwa,katika misitu inayosimamiwa na TFS zipo shughuli za kiutamaduni zilizowahi kufanyika na zipo zinazoendelea kufanyika ndani ya misitu hiyo ikiwemo mapango ya kuabudia, maeneo ya asilia yaliyotumika na machifu katika utawala wao na maeneo ya matambiko ambayo wananchi hutumia kuabudia katika mila zao.
Aidha, amewaomba Watanzania kutembelea katika hifadhi hizo ili kuweza kujionea historia mbalimbali zilizotunzwa katika hifadhi hizo. ikiwa ni pamoja na kujikumbusha historia ya jamiii mbalimbali na maadili wanayotakiwa kutafuta.
Nao wananchi waliotembelea banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania wamepongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa katika utunzaji wa maeneo mbalimbali yanayodumisha Utalii Ikolojia katika kutunza na kuendeleza tamaduni za jamii mbalimbali.
"Nimefurahishwa sana na nimependezwa na namna tamaduni zetu zinavyohifadhiwa na hii inasaidia sana kukumbusha jamii zetu kufuata mila na tamaduni ili kuweka maadili mema katika jamii, wananchi watembelee maeneo haya kujua historia na tamaduni hasa jamii ya kizazi kipya,"amesema Editruda Sanga
Kauli mbiu ya Tamasha la Pili la Kitaifa Utamaduni 2023 ni " Utamaduni ni msingi wa maadili, Tuulinde na Kuundeleza".
Kuhusu TFS
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ulianzishwa kisheria kupitia Tangazo la Gazeti la Serikali (GN 269) la Julai 30,2010 na kuzinduliwa rasmi Julai 18,2011.
Kuanzishwa kwa Wakala wa Huduma za Misitu ni kwa mujibu wa Sheria ya Wakala “the Executive Agencies Act Cap. 245 (Revised Edition 2009)”, pamoja na Sera ya Misitu ya mwaka 1998, Sera ya Ufugaji Nyuki ya mwaka 1998, Sheria za Misitu na Nyuki Sura 323 na Sura 224 za mwaka 2002.
Aidha, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania uliundwa kwa kuzingatia Programu ya Serikali ya Maboresho katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2000 (Public Service Reforms Programme (PSRP 2000)).
Programu hii ililenga kuimarisha Idara na Wakala (Ministerial Departments & Agencies (MDAs)) katika kuhakikisha utoaji wa huduma bora na madhubuti katika utumishi wa umma, ambapo Wakala zinakuwa na uwezo, motisha na mbinu za mabadiliko yenye kuleta ufanisi na tija kiutendaji.
Tags
Habari
Maliasili na Utalii
Maliasili za Tanzania
Tanzania Forest Services (TFS)
TFS
Utamaduni na Sanaa