DAR ES SALAAM-Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka waendesha bodaboda na Watanzania kwa ujumla kuondoa wasiwasi na taharuki kuhusu taarifa iliyosema kuwa,madereva bodaboda wataanza kulipishwa kodi, kwani taarifa hiyo sio taarifa rasmi kutoka kwenye mamlaka hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyoonwa na DIRAMAKINI imefafanua kuwa, “TRA inapenda kuufahamisha umma kuwa taarifa zinazosambaa kuhusu bodaboda kutozwa kodi sio rasmi.

Ilidaiwa kuwa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika mabadiliko ya Sheria za kodi mwaka 2023, serikali imeweka kodi ya mapato kwa wasafirishaji wa abiria kwa kutumia pikipiki zenye magurudumu mawili (Bodaboda) ambapo watatakiwa kulipa kiasi cha sh. 65,000 kwa mwaka.
Hayo yalisemwa juzi na Afisa Mkuu wa Usimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Hamad Mterry, wakati akiwasilisha mada ya mabadiliko ya sheria mbalimbali za kodi kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu.
Mterry amesema kuwa, hiyo ni moja ya sheria ya kodi ambayo ni mpya na imewagusa bodaboda, ambapo watatakiwa kuichagia serikali kiasi cha sh.65,000 kwa mwaka, kuanzia mwaka huu wa fedha ambao tayari umeanza tangu Julai Mosi, 2023.
Afisa Mawasiliano na Elimu kwa Umma kutoka TRA Mkoa wa Simiyu, Benjamin John amesema kuwa, bodaboda anaweza kulipa kodi hiyo kwa awamu nne ndani ya mwaka, ambapo kila awamu atatakiwa kulipa sh.16,250.