TTCL:Sisi ni kitovu cha uchumi wa kidigitali nchini

NA GODFREY NNKO

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limesema kuwa, ndilo kitovu cha uchumi wa kidigitali nchini (digital economy), hivyo litahakikisha huduma ya mtandao mpaka nyumbani (Fiber Mlangoni) inaleta matokeo chanya kwa wananchi na Taifa.

Mkurugenzi Mtendaji wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga ameyaeleza hayo leo Agosti 24, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, kinachoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ambapo leo ilikuwa ni zamu ya TTCL kuelezea walipotoka, walipo na wanapokwenda.

"TTCL inaendesha Mkongo wa Taifa na vile vile inatoa huduma ya Fiber Mlangoni ambazo zitahakikisha wananchi wote wanapata high speed inaneti nchi nzima.

"Kwa hiyo, tumeanza kutoa huduma hizo, tumefanya kwanza upgrade ya Mkongo wa Taifa kuanzia gbt 200 kwenda 800, na tunatarajia ifikapo mwezi Januari itafika 2TB (2 terabytes-GB2) ambayo ni kubwa kabisa.

Wakati huo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TTCL, Mhandisi Ulanga amesema, wapo katika mpango mkakati wa kuzimaliza changamoto za kimawasiliano nchini na ili kufikia hilo wilaya 139 sasa zitafikiwa na huduma ya Mkongo wa Taifa.

"Lakini lengo kubwa ni kuhakikisha wananchi wanapotumia huduma za kimtandao ziwe za kupitia huduma za Fiber Mlangoni tutahakikisha wote wanapata high speed intaneti nchi nzima, ziwe za gharama nafuu, lakini vile vile ziwe zinafika kila mahali.

"Ifikapo mwezi Januari mwaka 2024 tutakuwa tumefikisha wilaya 100, lakini lengo ni ifikapo Desemba (mwaka kesho) tuwe tumefika wilaya zote 139.

"Tulikuwa tunakumbana na changamoto kwenye baadhi ya wilaya kama Wilaya ya Mafia ambayo ipo baharini, lakini tumeshapata suluhisho kuhakikisha nako tunafika katika kipindi kijacho cha miezi kama minne au mitano.

"Sisi, kama Shirika la Mawasiliano tunataka kuwaambia wananchi kwamba, mnapoona maendeleo makubwa ya kimawasiliano nchini, sisi ndiyo tupo katika kitengo hicho.

"Ndiyo muhimili mkuu wa mawasiliano ambao tunaamini kabisa kuwa, uendelevu wa TTCL ndiyo uendelevu wa uchumi wa kidigitali hapa nchini,"amefafanua Mhandisi Ulanga.

Kuhusu uchumi huo

"Tunapozungumzia uchumi wa kidigitali (digital economy) mambo mengi yatakuwa yanapita kwenye mitandao, sisi ni sekta wezeshi ya muhimu sana ambayo tunafanya kazi kwa karibu sana na sekta ya fedha.

"Na kuhakikisha kwamba tunaboresha matumizi ya digital financial services, kwa hiyo kwa upande mmoja, tunaona kama tunavyotumia hizi mobile money,

"Lakini tunakoelekea tuko katika mazungumzo ya kuhakikisha kwamba, chini ya usimamizi wa wizara yetu tunahakikisha kwamba tunaachana kabisa na matumizi ya fedha mkononi.

"Lakini, mzungumzaji mkubwa atakuwa ni sekta ya fedha, sisi tunaweka miundombinu wezeshi katika maeneo mbalimbali, moja ya kipingamizi kilikuwa ni kutopatikana kwa miundombinu ya mawasiliano ya uhakika.

"Lakini sisi tunahakikisha ikishakuwepo miundombinu ya mawasiliano ya uhakika tutaweza kuingia kwenye cashless economy kirahisi zaidi, kwa sababu hilo kwanza lina faida tatu kubwa katika uchumi.

"Moja linaweka rekodi sahihi za matumizi ya fedha maeneo mbalimbali, mbili litarahisisha uwezo wa kukopa na kupeleka miamala sehemu mbalimbali na la tatu litaweza kuweka huduma mbalimbali za kifedha nchini,"amefafanua Mhandisi Ulanga.

Mageuzi

"Kuna mengi ya ndani ambayo tunayafanyia kazi, hatuamini kwamba katika hali tuliyonayo shirika tunaweza kuyafikia hayo bila kufanya transformation.

"Tuna mpango mkakati ambao ni transformation, kuna mengi ambayo tunayafanya kama internal process ambazo tunaendelea nazo,tunaishukuru sana Ofisi ya Msajili wa Hazina katika mambo ambayo yalikuwa yanatubana wameweza kutusaidia.

"Lengo ni tuweze kujiendesha kibiashara zaidi na kujibu mahitaji ya wateja wetu na wadau wetu mbalimbali ambao tunawapatia huduma.

"Utakuta kuna nguzo ya TANESCO tunashirikiana nao na ushirikiano huo utakuta tunajenga nguzo TANESCO wanaweza wakatumia. Mambo mengine tunabadilisha shirika letu liweze kulingana na haya tunayoyatarajia kuyafanya.

"Na jambo kubwa kuliko yote ni kuongeza ukubwa wetu katika kuwahudumia wateja, ninaamini tuna malalamimo mengi upande wa huduma kwa wateja tumeyaainisha malalamiko hayo, tunayafanyia kazi kusudi yaweze kuisha kabisa.

"Tuna changamoto mbalimbali ambazo mwanzoni tulikuwa tunayumba kidogo katika kushindana kibiashara. Sasa hivi tumebadilika na tuna uwezo, tuko vizuri na wadau.

"Sasa hivi pia tumeweza kukaa vizuri na Msajili wa Hazina mtakumbuka vizuri tumefanya kikao wikiendi iliyopita kilifunguliwa na Mheshimiwa Rais, lengo ni kuhakikisha changamoto zinazotubana kama mashirika ya umma na taasisi za serikali zinaondolewa.

"Sote tunatambua kwamba tunaishi kwenye soko la aina moja, utakuta changamoto zinazonibana mimi, zinambana pia Tigo, Vodacom na kadhalika kwa namna nyingine.

"Kuna maamuzi ya kisera yameshafanyika na mdhibiti ambaye ni TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania) yamefanyika, tumeweza kufanikiwa vitu mbalimbali.

"Moja wapo ni kufikisha mawasilino sehemu mbalimbali nchini,tuna ushirikiano na mashirikia zikiwemo kampuni na benki mbalimbali ambao ni wateja wetu wakubwa na tunawahudumia vizuri sana."

Pia, Mhandisi Ulanga amefafanua kuwa,TTCL wanajiangalia kwa upana zaidi, sio kama shirika tu la ndani ya nchi bali shirika kubwa linaloweza kutoa huduma nje ya mipaka ya nchi.

"Na, tumepuguza gharama zetu na kupata wateja wengi zaidi wa Fiber Mlangoni zaidi ya wale ambao tuliwategemea, pia tunajenga miundombinu kusudi tuwaunganishie wateja.

"Sambamba na utelekezaji wa mifuno ambayo imeongeza ufanisi wetu. Mtazamo wa Mkongo wetu wa Taifa kuna maeneo ambayo sasa hivi yalikuwa hayana mkongo wa taifa, tutayafikishia huko.

"Lengo ni kufikisha mkongo kila wilaya na baadaye kila tarafa na kata na wananchi wote wapate mkongo. Na concern yetu kama shirika ni kama tumeweza kufika Mlima Kilimanjaro tukiwa na mawaziri na mimi pia na viongozi mbalimbali hakuna changamoto yoyote itakayotushinda kama shirika.

"Tunaamini kwamba,shirika hili ni kitovu cha kufikisha uchumi wa kidigitali wa nchi yetu na sisi tunawakaribisha wote,"amefafanua kwa kina Mhandisi Ulanga.

Mkurugenzi wa Biashara

Naye Mkurugenzi wa Biashara TTCL, Vedastus Mwita amesema, wanaendelea na ujenzi wa miundombinu huku lengo likuwa ni kufanya vizuri nchi nyingi za Afrika ifikiapo mwaka 2027.

"Kwa miundombinu tunayoiandaa tunatamani kufikia mwaka 2027 muione TTCL ikifanya vizuri nchi mbalimbali Afrika na iweze kushindana na kampuni nyingine zitakazokuwepo.

"Pia tunatoa huduma vijiji 365, hivi vilikuwa havina kabisa huduma ya mawasilino kutokana na vijiji hivi kuwa pembezini sana.

"Kwa hiyo, TTCL kwa sasa inafanya kazi katika mikoa ya kibiashara 24, lakini kwa mwaka huu wa fedha tutaongeza mikoa mingine sita, kwa hiyo tutakuwa na mikoa 30 na tuna vituo vya huduma kwa wateja 109.Market share yetu ni asilimia 97, kwa hiyo TTCL ndio mmliki mkubwa katika nchi hii.

Mkurugenzi huyo wa Biashara amefafanua kuwa, "Huduma zetu zimegawanyika katika makundi makubwa matatu kwa maana ya makundi ya huduma za mawasiliano.

"Tunatoa huduma za data kupangisha vifaa vya mawasilino na huduma za simu. Sasa huduma hizi zimechakatwa katika makundi mbalimbali kuwawezesha wanaopewa huduma wazipate kwa namna wanavyoweza kutumia.

"Kwa hiyo utaona tunahuduma za data, sauti, mobile voice kutoa maeneo ya miundombinu ya mawasilino na katika nchi nzima tuna data center na maeneo hayo oparetors wote wanaruhusiwa kuwa na vifaa vyao, mpaka sasa wanavifaa vyao, lakini pia tuna kituo kikubwa kabisa.

"Ni kituo ambacho kinajumuisha vituo vyote 24 na kimsingi sisi ni wafanyabiashara wakubwa wa miundombinu. Na mwisho ni layer mbalimbali ambazo ni huduma mtumiaji wa mwisho anazitumia mlaji wa mwisho. Masoko ili kuufungua uchumi wa kidigitali tumepanga masoko katika makundi manne.

"Kundi la kwanza tunaliita Consumer Level, kundi hili linawahusu watu binafsi ambao hawana makampuni, lakini wanatumia huduma hii na pia aina ya bidhaa ambazo tunawapatia wireless mobile service, lakini pia na huduma hizi zinawezeshwa sana kwa fiber kuyawezesha haya.

"Kundi la pili ni makampuni ya kati, madogo,makubwa na serikali, lakini kundi la tatu ni mobile network oparetors.TTCL ni telecommunication oparetor anayewezesha miundombinu ya aina zote za mawasiliano.

"Kwa hiyo sisi tunaendesha aina zote za miundombinu ya mawasilino, lakini eneo la mwisho TTCL ni mwezeshaji wa huduma za mawasiliano kwenye nchi mbalimbali.

"Kwa sasa ukitazama biashara yetu utaona eneo kubwa linalochangia biashara ya TTCL ni eneo linalojumuisha makampuni, mabenki, taasisi kubwa, serikali, miradi ya kimakakati lakini eneo la pili ambalo ni eneo la biashara ya kimataifa tunatoa huduma za mawasiliano katika nchi mbalimbali.

"TTCL ndio mtoa huduma za data katika mradi mkubwa wa Mwalimu Nyerere hadi manispaa,mwezeshaji wa mawasilino airport zote Tanzania hii.

"Ndege zinaweza kuongozwa vizuri kutoka na mawasiliano ya TTCL, pia Wawezeshi wa data zetu zote, data za hali ya hewa na kuongoza anga, lakini pia TTCL ndio mwezeshaji wa data transmission ya wilaya zote na tumeziunga zote nchi nzima.

"Na ndio maana Mheshimiwa Waziri mkuu amekuwa akitumia miundombinu hii kufanya vikao na wakuu wa mikoa akitokea aidha Dodoma au Dar es Salaam. Kwa hiyo sisi ni wawezeshi.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Biashara TTCL,Mwita ameendelea kufafanua kuwa, "Lakini vile vile TTCL ndio mwezeshaji wa benki zetu. Benki zote leo ukienda Musoma huko utaingia benki X utafanya transaction mtu wa makao makuu anaona.

"Na eneo hili tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa ndio maana kuna hali ya usalama, CRDB, NMB, NBC, TCB, na benki nyingine.

"Tunatoa huduma kwa zaidi ya benki 20, lakini pia tumewezesha mradi wa mahakama, mtagundua pia hata mlolongo wa kesi kuna baadhi ya kesi zinafanyika wahusika wakiwa magerezani.

"Na miundombinu hii imejengwa na TTCL na huu ni mwaka wa nne imekuwa na mafanikio makubwa sana, TTCL pia amekuwa akitoa huduma kwenye miradi ya vyuo vikuu kuwezesha research mbalimbali kufanikishwa. Na pia anashiriki kwenye mradi wa SGR.

"Na mawasiliano haya yanachangia kwa asilimia kubwa sana kuleta maendeleo katika nchi hii. Miundombinu hii isipofanya kazi hata kwa dakika moja itakuwa shida kubwa sana.

"Sekta zote muhimu zinazowezesha wananchi kupata huduma muhimu TTCL amehusika pia.Tunaposema kuwa TTCL ni mwezeshaji wa huduma za mawasiliano Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika hatukosei tuko sahihi.

"Focus yetu kibiashara ni kuhakikisha tunatoa huduma za ubora na zinazopatikana wakati wote na maneo yanayojengwa makampuni kutumia TTCL.

"Pia tunataka kuhakikisha tunatoa huduma na kukidhi matakwa ya walaji. Pia TTCL. kuingia katika ushindani mkubwa wa kutoa huduma ndani ya nchi yetu na nje ya nchi zetu, hivyo watu wasiwe na wasiwasi na hili pia teknolojia ya habari na mawasiliano iwe bora ili Serikali ikusanye kodi kwa kupitia teknolojia.

"Katika mwaka wa fedha uliopita,shirika lilikuwa limewasha huduma za 4G Mobile kwenye kwenye maeneo ya vijiji na kata 102 zilizokuwa zimepata huduma hiyo na kwa sasa tunazifikia kata 104 ambazo zitakuwa zimeweshwa kupata huduma ya hiyo ifikapo mwaka 2024.

"Lakini kuna maboresho mengine ambayo yanaleta chachu ya kuendelea kufanya maboresho ya huduma za intaneti kutokana na maboresho hayo uingizaji wa intaneti hapa nchini umeongeza kuboresha miundombinu yake.

"Lakini chini ya usimamizi mzuri wa serikali tumeendelea kutekeleza miundombinu wezeshi na kuhakikisha inakuwa na mapinduzi katika sekta zote za kiuchumi na sisi kama shirika tumebaki kuwa kama mhimili wa mawasiliano na uchumi wa kidigitali,"amefafanua kwa kina Mkurugenzi wa Biashara TTCL.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news