MOROGORO-Wajumbe wa Tume iliyoundwana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan wamekutana na kufanya mazungumzo na Taasisi ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine mkoani Morogoro.
Katika mazungumzo hayo,uongozi,wafanyakazi na wanafunzi wametoa mapendekezo yao kwa baadhi ya maeneo wanayoshauri kufanyiwa maboresho katika taasisi Tume ya Rais ya Haki Jinai.
Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu ambaye pia ni Mjumbe wa kuangalia Jinsi ya Kuimarisha Taasisi za Haki Jinai, Balozi Ernest Mangu amesema, endapo mapendekezo yanayotolewa yatatekelezwa vyema na Taasisi za Haki Jinai zikatengewa bajeti ya kutosha kutaimarisha na kuleta mabadiliko ya kiutendaji kazi na uchumi kwa Taasisi hizo na Taifa kwa ujumla.
Amesema moja ya eneo ambalo linapaswa kufanyiwa maboresho ni kuwepo mifumo ya utoaji mafunzo kwa watendaji pamoja na matumizi ya TEHAMA kwa Taasisi hizo ambazo zimekuwa zikikumbwa na changamoto ya upotevu na kuharibika kwa taarifa za watu wanaowahudumia kutokana na kutunza taarifa hizo kwa njia ya makaratasi.
“Ni lazima na sisi tuboreshe namna ya kutekeleza majukumu yetu hasa kwenye haya maeneo ambayo tunagusa haki za watu, ili tuweze kuwa katika viwango ambavyo mataifa mengine yameshafikia,"amesema Balozi Ernest Mangu.
Pia Balozi Ernest Mangu amesema, maboresho yatakayofanyika yatahusisha pia marekebisho ya Sheria, Kanuni na Sera zinazogusa Mfumo wa Haki Jinai ikiwa ni pamoja na kutungwa kwa sheria na sera mpya zikazowezesha kuwepo kwa Mfumo imara wa Haki Jinai.
Naye Mjumbe wa Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuimarisha Taasisi za Haki Jinai, Dkt. Laurean Ndumbaro, amesema wakati wa ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wananchi Jeshi la Polisi limelalamikiwa sana kwa kushindwa kukomesha uhalifu, matumizi ya nguvu kupita kiasi, kubambikia watu kesi, vitendo vya rushwa na mali za watuhumiwa kupotea vituoni.
Amesema, baada ya kupitia malalamiko hayo na maoni yaliyopendekezwa, Tume ikapendekeza Jeshi hilo kufanyiwa maboresho ya muundo wake na kuwa Huduma ya Taifa ya Polisi (Natonal Police Service) kwa msingi wa Jeshi hilo ni kuhudumia jamii.
"Kwa upande wa Taasisi, Jeshi la Polisi limelalamikiwa sana, Tume tumeyapitia malalamiko hayo na mapendekezo yaliyotolewa, tukapendekeza Jeshi la Polisi lifanyiwe maboresho makubwa, badala ya kuendelea kuwa Jeshi la Polisi litambulike kuwa National Police Service,
"Kwa msingi wake ni kuhudumia jamii, kulinda raia na mali zao, sambamba na kubadilishwa kwa mfumo wa mafunzo ya jeshi hilo,"amesema Dkt. Ndumbaro
Aidha, Dkt. Ndumbaro amesema Jeshi la Magereza nalo limelalamikiwa katika maoni ya wananchi kwa kutumia nguvu kupita kiasi na ukaguzi unaotweza utu, ukaguzi ambao unakinzana na kifungu cha sheria ya Utu wa mtu kuheshimiwa.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA),Prof. Raphael Chibunda amesema, Chuo hicho kitaendelea kushirikiana na Wajumbe wa Tume hiyo pamoja na serikali katika utoaji wa elimu ya masuala ya Haki Jinai kwa jamii.
Amesema, hatua hii itawawezesha wananchi kushirikiana kwa karibu na vyombo vya Haki Jinai, vilevile kuwafanya waliopewa dhamana ya kusimamia vyombo hivyo kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu kama zinavyoelekeza.
Meltus Rwezaula ni Msimamizi wa Kumbukumbu Daraja la Kwanza SUA, akatoa mchango wake kuhusiana na ukamataji wa watuhumiwa unavyofanywa na Jeshi la Polisi wakati mwingine usivyozingatia weledi kwa kazi zao, akisisitiza pia mabadiliko ya sheria za makaosa ya usalama barabarani.
Amesema, tume hiyo ikaangalie na kurekebisha adhabu za makosa ya barabarani ambayo imegeuka kuwa tatizo sugu kwa kushindwa kuleta suluhu, hasa kwa wanaofikishwa mahakamani kwa matukio ya ajali za uzembe wamekuwa wakipewa adhabu ambazo haziwafanyia kujutia kosa badala yake raia wamekuwa waathirika wa matukio hayo.