Tutafakari yanayotukuta

NA ADELADIUS MAKWEGA

WAKRISTO wameambiwa kuwa Mwenyezi Mungu hapatikani katika fujo, Mungu hawezi kupatikana kwa kumkimbia na wala hatuwezi kumpata Mungu wetu kwa kumuogopa.

Hayo yamesemwa na Padri Godian Sempige Msigala leo Agosti 13, 2023 katika mahubiri ya Dominika ya 19 ya Mwaka A wa Liturjia ya Kanisa, Parokiani Chamwino Ikulu, ndani ya misa iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria Imakulata, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.

“Kwa utume ambao Mungu anatupatia, unaweza kusema umeoa au umeolewa na mwenza wa ajabu, hata sisi watawa unaweza kusema kuwa hivi kweli mimi Mungu aliniita niwe Padri?.

"Kwa haya yote ninayopitia? Sasa jamani kila mmoja wetu naomba atambue kuwa huu ni wakati sahihi wa kwenda kukaa kwa ukimya na Mungu wetu.”

Akiendelea kuhubiri katika misa hiyo ya kwanza ya Jumapili hii iliyoanza saa 12.30 ya asubuhi, Padri Msigala alifafanua kuwa,

“Tuyatafakari yanayotukuta, ili tufahamu hapo Mungu anataka kutuambia nini? Mfano wa wazi ni wa Nabii Hosea, yeye alioa mwanamke muhuni, mkewe alikuwa mzuri, akawa na tabia chafu, huku akitembea na watu wa mataifa mbalimbali.

"Maana huo urembo wake uliwavutia wageni hao, tambua huyo ni mke wa nabii, mke muhuni. Nabii Hosea akasema,’Hivi Mungu! Kwelii mimi nabii wako.

"Lakini mke wagu yuko hivi kweli?’ Nawaombeni waamini wangu katika hali kama hii tutumie wasaa huo tuyatafakari tunayopitia ili tujue Mungu anataka kusema nini nasi?.”

Misa hiyo iliyofanyia katika hali ya utulivu mkubwa, huku juu ya kanisa hilo wakisikika ndege na mdudu nyenze lakini sauti hizo zilinaswa na mashine ya kurekodia ya mwandishi wa ripoti hii tu, wakati ilikuwa ngumu waamini kuzisikia kabisa sauti hizo mbili maana walizama katika tafakari kubwa ya mahubiri hayo yanayogusa maisha ya kila siku ya binadamu.

Padri Msigala aliongoza adhimisho la misa hiyo ikiwa na nia na maombi kadhaa, yaliyoongozwa na maelezo kuwa katika misukosuko ya bahari, Yesu alitokea na kujitambulisha kama mwokozi wa wafuasi waliokuwa na hofu ya kuzama katika maji,

“Utulize mawimbi na kutupa shwari na amani, wakati mashua ya maisha yetu inapoyumbishwa na matatizo na magumu ya maisha, Ee Bwana.”

Hadi misa hiyo inakamilika hali ya hewa ya Kijiji cha Chamwino Ikulu ilikuwa ya baridi kali, upepo kiasi huku ardhi ikipambwa na majani mengi yaliyokauka, lakini kijani kibichi kilionekana katika macho ya mwandishi wa ripoti hii, pale maeneo yanayomwagilia tu ambayo ni machache sana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news