ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema ujio wa nyota maarufu wa filamu nchini China, Jin Dong utaendelea kuifungulia Zanzibar soko la Utalii kutoka China.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika mazungumzo na mgeni wake Msanii Maarufu wa Sanaa ya Filamu kutoka nchini China, Jin Dong alipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar leo Agosti 10,2023 na kushoto kwa Rais ni Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi.(Picha na Ikulu).
Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Agosti 10,2023 Ikulu jijini Zanzibar alipotembelewa na msanii huyo ambaye yupo Zanzibar kwa kazi ya kutengeneza filamu.
Alisema, ujio wake ni fursa adhimu kwa Zanzibar kutangazwa kimataifa hasa kupitia Sekta ya Utalii ambayo ni sekta mama ya Uchumi wa Taifa.
Rais Dkt.Mwinyi alimueleza mgeni wake huyo kwamba, Zanzibar ina vivutio vingi vya utalii, ukiwemo utalii wa fukwe safi nyeupe zinazovutia wengi duniani,utalii wa utamaduni, utalii wa Mji mkongwe,utalii wa michezo, utalii wa visiwa pamoja na wa mikutano.
Aidha, alimkaribisha mgeni huyo kuitumia fursa ya kuwepo kwake Zanzibar kutembelea maeneo muhimu ya utalii likiwemo shamba la viungo vya Zanzibar, Kisiwa cha Mnemba, Kaskazini Unguja pamoja na Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Naye, nyota huyo wa filamu nchini China, Jin Dong alimueleza Rais Dkt.Mwinyi furaha yake ya kufika Afrika kwa mara ya kwanza tena ndani ya visiwa vya Zanzibar kwa nchi za Afrika Mashariki.
Alisema, mbali na safari ya sanaa hapa Zanzibar, lakini pia ujio wake unaimarisha uhusiano wa undugu na urafiki uliopo baina ya China na Tanzania ikiwemo Zanzibar.
Aliahidi kuwa, balozi mzuri wa kuitangaza Zanzibar kwa Utalii na alieleza imani yake ya kuwavutia Wachina wengi kuja kutalii visiwa vya Zanzibar.
Miongoni mwa maeneo ya utalii aliyotembezwa msanii huyo ni kisiwa cha Mnemba, Mji Mkongwe maeneo ya Forodhani na Ngome Kongwe.
Jin Dong ni nyota mkubwa China mwenye wafuasi wa mitandao ya kijamii zaidi ya milioni 15. Mbali na kazi za sanaa pia ni mwanasiasa na Naibu Mkurugenzi wa Kikundi cha Sanaa cha Serikali cha Utamaduni.