DODOMA-Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID), Craig Hart ameahidi kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya shirika hilo na Tanzania kuhakikisha ustawi wa watoto unaimarishwa.
Craig ameyasema hayo alipokutana na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt.Dorothy Gwajima jijini Dodoma Agosti 21, 2023 kwa lengo la kujitambulisha na kuanza majukumu yake nchini baada ya aliyekuwepo Cate Somvogsiri kumaliza muda wake.
Craig amesema suala la malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto linahitaji ushirikiano wa wadau wote hivyo kuahidi kuwaunganisha wadau kufanya kazi kwa pamoja.
Kwa upande wake Waziri Dkt. Gwajima amemueleza Mkurugenzi huyo kwamba katika kuhakikisha huduma bora za Ustawi hasa kwa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, Wizara inashirikiana na USAID tangu mwaka 2013 kupitia miradi mbalimbali.
Ameongeza kuwa, bado kuna changamoto kadhaa zinazohitaji ushirikiano ili kuzitatua baadhi zikiwa ni migogoro ya familia, uhaba wa Maafisa Ustawi wa Jamii na upungufu wa vitendea kazi kwa Maafisa hao.