Usiyoyafahamu kuhusu NHC, walituvusha je kutoka mapipa na makuti?

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Hamad Abdallah amesema, mapato ya shirika hilo yamekuwa yakiongezeka kila mwaka.

"Kwa hiyo Shirika la Nyumba la Taifa, mapato yetu yamekuwa yakiongezeka kila mwaka, ukiangalia mwaka 2022 mapato yetu yalikuwa bilioni 257.47 ukilinganisha na mapato ambayo ni ya mwaka 2021 ambayo yalikuwa ni bilioni 144.

"Kwa hiyo utaona kulikuwa na ongezeko kubwa sana, lakini vile vile mnafahamu mapato yetu yamekuwa yanategemea sana hizi nyumba ambazo tumekuwa tunapangisha ambapo mapato vile vile yaliongezeka.

"Kwa mwaka 2022 tulikuwa na mapato ya bilioni 90.79 ukilinganisha na mapato ya mwaka 2021 ambayo yalikuwa bilioni 80.923 lakini mauzo ya nyumba, na sisi mapato yetu yanapopatikana kwenye upangishaji wa nyumba, kwenye uuzaji wa nyumba, miradi ambayo tunajenga sisi asilimia kubwa huwa tunauza.

"Kwa hiyo mapato ambayo yalipatikana kwenye mauzo ya nyumba kwa mwaka huu wa fedha ilkuwa ni bilioni 121 na utaona kulikuwa na ongezeko kubwa la kutoka bilioni 29 ambazo tulikuwa tunapata awali.

"Nadhani mnalifahamu lile jengo la CRDB makao makuu, mmeliona lile jengo kubwa? Lile ni moja ya matunda ya National Housing.

"Lile jengo tulili-design National Housing, tumelijenga National Housing na tukawauzia CRDB kwa hiyo mapato yanayopatikana kwenye maeneo kama yale ndiyo mnaona faida yake hii.

"Lakini, vile vile sisi ni wakandarasi wa daraja la kwanza, kwenye mapato ambayo tumekuwa tukipata kupitia ukandarasi utaona mwaka 2021 tulikuwa tumepata bilioni 23.6 lakini mapato hayo yakaja kuongezeka 2021/22 mpaka bilioni 43.98 sasa huu mchanganuo ndiyo unakuja kutupatia mapato ya bilioni 257.47."

Mbali na hayo, Mkurugenzi Mkuu wa NHC ameainisha vipaumbele vya kukuza sekta ya nyumba nchini huku akisema shirika hilo litaishawishi Serikali kufanya nyumba kuwa ni kipaumbele cha Taifa.

Ameyaeleza hayo leo Agosti 3, 2023 wakati wa kikao kazi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, kinachoratibiwa na Msajili wa Hazina katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Pia, amesema kwa sasa juhudi zinafanyika kuwaruhusu Diaspora kununua nyumba na kuwekeza katika ardhi ya Tanzania.

Amesema, kasi ya ukuaji wa uchumi inazidi kuongezeka ambapo kwa sasa shirika lina nyumba za bei nafuu kila mkoa kwa ajili ya Watanzania wenye uhitaji wa nyumba za makazi.

Katika hatua nyingine, akizungumzia Sera ya Ubia kati ya NHIC na Sekta Binafsi amesema, kwa sasa imefungua milango ya uwekezaji kwenye sekta ya nyumba na kuendelea kuvutia wawekezaji nchini kupitia sekta binafsi ambayo ni injini ya kujenga uchumi imara.

Akizungumzia mpango wa matengenezo ya nyumba za shirika amesema, sambamba na ukusanyaji wa kodi shirika limetumia shilingi bilioni sita kukarabati nyumba 847 maeneo mbalimbali.

Pia amesema, bado ukarabati unaendelea pamoja na kuanzishwa kwa mradi mpya wa ujenzi wa nyumba za makazi ujulikanao kama Samia Housing Scheme utakaohusisha ujenzi wa nyumba 5000 nchini.

Wakati huo huo, amesema wanakuja na mpango wa kuwatangaza wadaiwa sugu kwenye vyombo vya habari na kuwataka wateja wao kuzingatia na kufata masharti na taratibu za upangaji wa nyumba za shirika hilo.

NHC nini?

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Hamad Abdallah amesema, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa historia, ni shirika ambalo lilianzishwa kwa Sheria Namba 45 ya 1962.

"Na lilikuwa ni shirika la kwanza kabisa kuanzishwa na Mwalimu Nyerere (Rais wa Kwanza, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere) najua kuna mashirika mengine ambayo yamekuja yameshafanya mawasilisho kama mashirika matano na wengine watakuja.

"Lakini, sisi tunajivunia kuwa ni shirika la kwanza kabisa kuanzishwa na Mwalimu Nyerere mwaka 1962, mwaka mmoja tu baada ya Uhuru, akaanzisha shirika la nyumba la Taifa.

"Na dhamira ninadhani ilikuwa ni kuweza kuwapatia Watanzania makazi bora,unafahamu baada ya Uhuru ukitoka tu Kariakoo ukienda Magomeni Mapipa, nadhani wengi wenu mnafahamu kwa nini iliitwa Magomeni Mapipa.

"Kwa sababu, mapaa ya nyumba zake zote zile zilikuwa yanakatwa mapipa yale kwa hiyo wanatengeneza mabati, hatukuwa na mabati wakati huo, lakini inawezekana mabati yalikuwepo kidogo,lakini kufuatana na hali za Watanzania wakati huo waliweza kumudu kuweka mapipa kama sehemu zao za kujistiri.

"Lakini, ukienda mbele kidogo unakutana na Magomeni Makuti, makuti kwa sababu nyumba zile ziliezekwa na makuti, na Mwalimu nadhani aliona umuhimu wa kuanzisha shirika ambalo sasa litatoa makazi bora kwa Watanzania.

"Kwa hiyo mwanzoni kwenye miaka ya 60 (Mwalimu Nyerere) akaja na Scheme ambayo ilikuwa inaitwa Operesheni Ondoa Makuti, nyumba nyingi za Dar es Salaam na mikoa mingine zilikuwa zimeezekwa na makuti.

"Kwa hiyo, kupitia kwenye ile operesheni Watanzania waliweza kupata makazi, sasa hiyo miradi ilikuwa inafanyika kwa namna gani? Serikali ilikuwa ikitoa fedha moja kwa moja asilimia 47, lakini vile vile tulikuwa na wahisani, Ujerumani Magharibi.

"Pamoja na Benki ya THB ambayo ilikuja kuanzishwa baada ya shirika kuanzishwa, ilikua ikitoa mikopo, kizazi hawakumbuki kama kulikuwa na Benki ya Nyumba ambayo inaitwa THB-Tanzania Housing Bank.

Kwa pamoja, walikuwa wakichangia takribani asilimia 47, lakini na asilimia 13 ya kipato ilikuwa inatokana na asilimia chache ya nyumba ambazo Shirika la Nyumba la Taifa lilikuwa linazimiki wakati huo.

"Sasa, kupitia Operesheni Ondoa Makuti, Watanzania waliweza kupata makazi, walipataje makazi, watu walikuwa na viwanja vyao, alichokifanya Mwalimu,nyumba zilikuwa zinajengwa, kulikuwa kuna nyumba za vyumba sita na vyumba vinne, kwa hiyo shirika linajenga zile nyumba na mtu anakopeshwa.

"Nyumba ya vyumba sita nadhani ilikuwa ni shilingi elfu 10,000 (kwa wakati huo) na nyumba ya vyumba vinne shilingi elfu 6,000 miaka ya sitini.

"Sasa, kilichotokea ni nini, Watanzania vile vile walikuwa hawana uwezo wa kurejesha hizo fedha, zile nyumba ukiziangalia mpaka leo, ukienda Magomeni kuna nyumba zilijengwa na Shirika la Nyumba la Taifa miaka hiyo.

"Nyingine zilijengwa Mwananyamala, zilijengwa Temeke, Ilala kulikuwa na pande mbili kulikuwa na design kwa jili ya kipangisha ili ziweze kumuwezesha yule mtu aweze kurejesha ule mkopo.

"Kwa hiyo, kulikuwa na utaratibu huo ambao tunauita tenancy pattern scheme maana yake unakuwa mpangaji mnunuzi,Watanzania wengi sana waliweza kuwezeshwa wakawa wamiliki wa nyumba.

"Na nyumba hizo ukienda Songea utazikuta, ukienda maeneo mbalimbali utazikuta, kwa hiyo utaona dhamira ya Mwalimu mwaka 1962 iliweza kulifanya shirika liweze kujiendesha vizuri.

"Na aliendelea hivyo, mpaka miaka ya 1978-9 tuliiingia kwenye vita na Uganda (historia), uwezo wa Serikali kuweza kutoa ruzuku ile asilimia 47 ikawa ndogo, ilikuwa na majukumu mengine sasa, lakini wakati huo huo bei ya mafuta mwaka 1979 iliongezeka sana kwenye soko la Dunia.

"Kwa hiyo, fedha nyingi sana zikawa zinatumika sasa kwenye mambo mengine ya muhimu.Kwa hiyo,uwezo wa Serikali kutoa ruzuku ulikuwa haupo, kwa hiyo ikasimamisha kutoa ruzuku nadhani ruzuku ya mwisho kabisa ilikuwa mwaka 1982.

"Kutoka serikalini kuja Shirika la Nyumba la Taifa, na baada ya hapo sasa NHC ikatakiwa ianze kujiendesha yenyewe, kwa bahati mbaya sana uwezo wa kujiendesha ikawa haina, wakati wa ubinafsishaji wa mashirika.

"Kilichofanyika sasa, mwaka 1990 Serikali iliona iweze kulikwamua (NHC) kwa hiyo ikaja na Sheria Na 2 ya mwaka 1990 ambayo sasa ilikuja kuunganisha iliyokuwa Msajili wa Majumba (Register of Building).

"Zamani ulikuwa ukipita mjini kote unakuta Msajili wa Majumba, zile nyumba zilikuja kuhamishwa kwa sheria ya mwaka 1990, kwa kuunganisha ilyokuwa Msajili wa Majumba na National Housing, na sababu ya kufanya hivyo ilikuwa ni kuifanya National Housing iweze kujiendesha.

"Lakini nayo bado haikuweza kuisaidia shirika kuweza kujiendesha kibiashara, kwa hiyo mwaka 2005 kukawa na mabadiliko ya sheria, kupitia Miscellaneous Amendments Laws No. 2, ambayo ilifanya mabadiliko ya sheria nyingi.

"Moja kuiondoa au kuifuta rent restriction act ambayo ilikuwa inaonekana kuwa, pamoja na kuunganisha Msajili na National Haousing, sheria hii ilikuwa inaibana National Housing kuweza kujiendesha, mambo machache kwenye sheria ambayo ilikuwa inaitwa rent restriction ulikuwa hauwezi kuongeza kiwango chochote cha kodi,bila kupitia kwenye mabaraza ya kodi, kulikuwa kuna mabaraza ya kodi.

"Na ili mabaraza ya kodi yaweze kupitisha hizo kodi, ni lazima wathamini wapite wafanye uthamini wa nyumba zote ili waweze kupata standard rent.

"Kodi ambazo zinatakiwa zitozwe kwa wapangaji, lakini vile vile kumtoa mpangaji ambaye ameshindwa kulipa kodi, kwa mfano ulikuwa ukitakiwa kwenda kuomba kibali mahakamani, bia hivyo hauwezi kumtoa mpangaji.

"Na, hii haikuwa sheria kwa ajili ya Nationa Housing tu, ilikuwa sheria kwa Watanzania wote, kwa makampuni yote ambayo yalikuwa yamewekeza kwenye real estates.

"Lakini unafahamu wengine walikuwa hawana utii wa hizo sheria, lakini Nationa Housing ni taasisi ya Serikali lazima ifuate hizo sheria, kwa hiyo sheria hii ilikuwa mwiba kidogo kwa National Housing.

"Ukitaka kuendeleza upya maeneo na kutaka kuwaondoa wapangaji, moja wakati huo ukishatoa tu notisi, ile kusimama halipi tena kodi, lakini vile vile kwenye sheria ilikuwa inaelekeza ukamtafutie makazi mbadala.

"Na ilikuwa inatoa vigezo makazi mbadala ni nini, kodi zake ziwe sawa sawa, maeneo ambayo kama watoto wanasoma Jangwani Sekondari na walikuwa wakitembea kilomita moja kwenda Jangwani Sekondari,basi wasitembee zaidi ya kilomita moja.

"Iliweka vigezo vingi sana, na hayo yote ilikuwa mwiba kwa Shirika la Nyumba kuweza kujiendesha, bahati nzuri sheria hiyo ikaja kuondolewa mwaka 2005.

"Sasa kuanzia hapo, Shirika la Nyumba likatakiwa lijiendeshe kibiashara,kuwa kulikuwa kuna vikwazo hivi na vile, vikwazo hivyo tumeshaviondoa, sasa mnatakiwa mjiendeshe kibiashara."

"Sasa, kufuatana na sheria namba mbili ikawa imetoa majukumu mbalimbali kwa shirika, kuwa ifanye majukumu gani.

"Moja wapo ilikuwa ni kujenga nyumba za makazi na biashara na kuzipangisha, ambapo jukumu hilo lilikuwepo toka sheria ya mwaka 1962.

"Sheria namba 45, lakini vile vile kujenga majengo kulingana na mipango maalum tunaita schemes. Lakini, nyingine ilikuwa ni kuzalisha vifaa vya ujenzi, wanaoifahamu National Housing vizuri wanakumbuka zamani tulikuwa na viwanda vya kutengeneza fenicha.

"Kiwanda kilikuwa kinaitwa TACONA, lakini vile vile tulikuwa na kiwanda kwa ajili ya kuzalisha matofali ya kuchoma, yalikuwa yanatoka Kisarawe.

"Kwa hiyo, moja ya majukumu ambayo tulikuwa tumepewa ilikuwa ni kuzalisha vifaa vya ujenzi, lakini vile vile kusimamia milki, milki nikizungumza ndiyo viwanja, majengo kwa Kiswahili (real estates) ya shirika.

"Nyumba ambazo za shirika tulikuwa tumeziridhi kutoka Msajili wa Majumba, lakini vile vile nyumba ambazo National Housing iwe ilikuwa ikijenga, huwa tunatakiwa tuziangalie hizo nyumba.

"Kukusanya kodi, tuweze kusimamia mikataba na wapangaji lakini vile vile tuweze kuzifanyia matengenezo.

"Lakini, jukumu lingine ambalo tuliongezewa ni ujenzi ambapo sisi wenyewe tuwe ni wakandarasi, lakini vile vile tuweze kutoa ushauri elekezi kwenye sekta ya ujenzi,"Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Hamad Abdallah ametoa historia ya shirika hilo kwa upana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news