Vyanzo vya ukatili wa kijinsia Bunda vyatajwa

NA FRESHA KINASA

MFUMO dume, utelekezaji familia, kucheza kamari na kutokuwajibika kuhudumia familia kwa wanaume wa Kata ya Chitengure katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara vimetajwa kuchangia vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Hali ambayo inarudisha nyuma juhudi za Serikali na wadau wanaopambana kutokomeza vitendo vya ukatili ndani na nje ya halmashauri ya wilaya hiyo mkoani Mara. 
Hayo yamebainishwa Agosti 18, 2023 na Wananchi Vinara wa mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia katika mjadala wa wazi uliofanyika katika Ofisi ya Kijiji cha Busambara.

Ambapo, umewakutanisha viongozi wa serikali, Wananchi na Shirika la VIFAFIO linalotekeleza mradi wa 'Funguka paza Sauti kutokomeza Ukatili' chini ya ufadhili wa Shirika la Foundation for Civil Society.

Kusekwa Masungwa amesema kuwa, wanaume wamekuwa wakishindwa kuhudumia familia zao na badala yake kuwaachia jumumu hilo wanawake kutokana na biashara ndogo ndogo wanazofanya ili wahudumie familia. 
"Wanaume wamekwepa jukumu la kuhudumia familia na wanatuachia jukumu hilo sisi wanawake kufanya biashara ndogo ndogo ili tuhudumie familia. 

"Hata mwanamke akipata pesa bado anaombwa na mwanaume kwa lazima eti akazimue (kunywa pombe) usipo mpa tu anapigwa au anatoa lugha chafu mara nitakufukuza kwangu (ukatili wa kisaikolojia),"amesema Kusekwa. 

Sarah Juma amesema kuwa, wanaume wamekuwa wakitumia mfumo dume katika familia zao akitolea mfano pale msimu wa mauzo ya zao la pamba wanaume hutumia fedha hizo pasipo kuishirikisha familia akiwemo mama na watoto ambao wameshiriki mwanzo mwisho katika Kilimo na hatua zote za uvunaji. 

"Mama na watoto wamelima, wamepanda, wamepalilia wamevuna na wakati mwingine baba alikuwa akienda shamba mara moja moja muda mwingi yeye anawaagiza nendeni shambani."amesema na kuongeza kuwa.

"Lakini siku ya kuuza yeye ndiye anashika pesa yote hataki ashirikishe familia kupanga mipango ya maendeleo anakwenda mjini kunywa pombe na Wanawake wengine akirudi hana pesa na mkali kweli kweli hataki kuulizwa chochote,"amesema Sarah Juma. 
"Upo mchezo wa kamari ambao baadhi ya wanaume wamekuwa wakiucheza, baba anatoka nyumbani asubuhi anakwenda huko. akirudi nyumbani mchana ama usiku kula. 

"Na asipokuta chakula nyumbani anamgombeza mwanamke wakati hakuacha pesa ya matumizi. Hajui mboga imenunuliwaje ama unga hajanunua japo si wote,"amesema Paul Yusuph. 

Judith Kajana amesema, baadhi ya wanaume kutelekeza familia imekuwa ikichangia kwa kiwango kikubwa mimba za utotoni ambapo baadhi ya watoto hujiingiza katika matendo yasiyofaa ikiwemo ngono na kupelekea mimba hizo kabla ya umri wao unaokubalika kisheria. 

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Fausta Gabriel amesema, ukatili wa kijinsia umegawanyika katika aina nne ukiwemo ukatili wa kisaikolojia, kiuchumi, kimwili na kingono.
Ameshauri kila mmoja kushiriki katika kutokomeza aina hizo, kwani kwa kiasi kikubwa aina zote hizo zinafanyika na madhara yake ni makubwa ikiwemo ulemavu wa kudumu, migogoro ya ndoa, madhara ya kisaikolojia, magonjwa ya kuambukiza, wanafunzi kushindwa kutimza ndoto zao na kuchangia umaskini katika jamii. 

Fausta amesema, katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mimba za utotoni zipo kwa kiwango kikubwa ambapo kila kata zaidi ya wasichana 50 wamepewa mimba wakiwa katika umri mdogo jambo ambalo linahitaji nguvu ya pamoja ya jamii kuweza kulimaza. 

Robinson Wangaso kutoka Shirika la VIFAFIO amesema kuwa, wamekuwa wakitekeleza mradi huo kuisaidia Serikali katika kuhakikisha jamii inakuwa salama kwa kuondokana na ukatili hasa kata kando kando ya ziwa na maeneo ya mialo lengo ni kuleta mabadiliko chanya ya kumaliza ukatili wa kijinsia. 

Mwenyekiti wa Kijiji cha Busambara, Reuben Myenjo amelishukuru Shirika la VIFAFIO kwa kutekeleza mradi huo wa kupinga ukatili kwani utaweza kusaidia kupunguza vitendo hivyo huku akisema jambo hilo litawekwa katika ajenda za vikao vya Serikali ya Kijiji na vitongoji ili kutoa elimu kwani ukatili upo unahitaji mkakati kuumaliza. 
Katika mjadala huo mapendekezo yametolewa yatakayosaidia kupunguza ukatili ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi wa kata hiyo, sheria zifuatwe kumaliza mchezo wa kamari kwa wanaume, waelimishwe kuhudumia familia zao na kuwaripoti wanaotekeleza familia zao kwa hatua za kisheria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news