NA GODFREY NNKO
WADAU mbalimbali nchini wameombwa kuendelea kujitolea kufanikisha huduma za hedhi salama shuleni ili kuwapa watoto wa kike nafasi ya kujisomea kwa furaha wanapofikia kipindi hicho.
Rai hiyo imetolewa leo Agosti 7,2023 katika Shule ya Msingi Mtoni iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam na Mlezi wa Kikundi cha Wake wa Viongozi cha Ladies of New Millenium Women Group, Mke wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mary Majaliwa.
Mama Majaliwa ametoa wito huo, ikiwa mwaka jana Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu alibainisha kuwa, asilimia 48 ya wanafunzi wa kike wanakosa masomo kutokana na kuwa katika mzunguko wa hedhi hali ambayo huathiri uwezo wa wanafunzi hao kujifunza kwa ufasaha.
Waziri Ummy aliyasema hayo jijini Dodoma wakati akifungua warsha ya usambazaji matokeo ya utafiti juu ya hedhi salama uliofanyika kwa wanafunzi wa kike katika mikoa 16 nchini.
Alisema, utafiti huo uliofanywa mwaka 2015 na shirika la SNV Netherlands Development pamoja na Tanzania Water and Sanitation Network (TAWASANET) katika halmashauri za Sengerema, Mufindi, Chato.
Sambamba na Temeke ulionesha kuwa, asilimia 48 ya wanafunzi wa kike hukosa masomo wanapokua kwenye hedhi asilimia 78 ya waliohojiwa walisema kipindi cha hedhi huathiri uwezo wao wa kujifunza.
Mbali na hayo, Mama Majaliwa akizungumza katika hafla hiyo ya kukabidhi jengo ambalo limekarabatiwa na Ladies of New Millenium Women Group mahususi kwa ajili ya kuwastiri watoto wa kike kipindi cha hedhi shuleni hapo amesema, hiyo ni hatua njema ambayo inapaswa kuunga mkono na wengine.
"Kwanza kabisa napenda kutoa shukurani zangu kwa akina mama wa Millenium (New Millennium Group) kwa ajili ya kuja kulikarabati hili jengo ili kuwasaidia watoto wetu wa kike ili kutimiza hedhi salama.
"Nimefurahi sana kuliona hili jengo, bahati nzuri nimepita huko ndani nimeliona, ni jengo nzuri na ninaamini litakuwa msaada mkubwa sana kwa watoto wetu wa kike kwa ajili ya kujihifadhi pale wanapoona sasa hali imekuwa mbaya na kuendelea vizuri na vipindi madarasani.
"Napenda pia nimshukuru mama yetu Mama Selina ambaye amejitoa kwa kupitia kipato chake, kutusaidia kuleta hizi taulo za watoto kike.
"Na kadri alivyoeleza, ameeleza kwamba ameshasaidia shule nyingi za hapa Dar es Salaam, kwa hiyo mama mimi ninakushukuru sana na ninaomba uendelee na moyo huo.
"Bahati nzuri umeahidi kuendelea kuleta tena hapa shuleni,tunaendelea kukushukuru, kwani kwa kuendelea kufanya hivyo,ninaamini watoto wetu wataendelea kujihifadhi vizuri siku zote na kusoma katika hali ya utulivu wakiwa darasani.
"Pale hali hiyo inapowakuta ghafla wakiwa katika siku zao za hedhi, naomba nitoe wito kwa wadau wengine wote yakiwemo mashirika binafsi mbalimbali ambao wanaweza kujitoa kusaidia watoto, kusaidia kama anavyofanya huyu mama, waendelee kutusaidia.
"Wanaweza kuja shuleni, wakaona mazingira yalivyo wakanona vyumba vilivyo wanaweza kupata chumba wakafanya ukarabati kama tulivyofanya sisi, lakini pia wanaweza kujenga chumba kikubwa zaidi.
"Ili kuweza kuwasaidia hawa watoto waweze kuendelea na masomo kama kawaida na waweze kujihifadhi kama inavyotakiwa."
DC Temeke
Naye Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam,Mheshimiwa Mobhare Holmes Matinyi amewashukuru wake wa viongozi kupitia asasi yao ya Millenium kwa moyo wao wa upendo.
"Tunawashukuru kwa moyo mzuri wa kujali, watoto wetu, binti zetu ambao wapo shuleni, hili ni jambo muhimu ambalo tulikuwa hatuliangalii.
"Lakini, wao wameliona na wamekwenda hatua kubwa zaidi wamekarabati vyoo kwa ajili ya watoto wa kike na kuviwekea mahitaji muhimu kwa ajili ya kuwasaidia katika kipindi ambacho ni muhimu katika maisha yao.
"Tungependa kutoa wito kwa watu wengine waunge mkono juhudi hizi ili shule zetu ziweze kuwaisaidia watoto huduma kama hizo.
"Pia, tunamshukuru sana Mama Selina kwa juhudi zake na kwa kujitoa kwa ajili ya kusaidia taulo, huu ni moyo wa utu na ndiyo moyo wa Utanzania. Na ninafurahi sana kwa kuwa, wana mpango wa kufanya hivyo katika shule zote za Temeke, kwa kweli litakuwa jambo la kuingwa kwa Tanzania,"ameeleza.
Mkuu wa Shule
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mtoni, Victor Kangati amesema, "Tunawashukuru sana Ladies of New Mellenium kwa kuwaletea watoto wetu wa Shule ya Msingi Mtoni taulo.
"Kwa kweli ni jambo kubwa ambalo litawasidia sana watoto wetu hasa wa kike kupunguza utoro, kwa sababu hapo nyuma, suala la utoro lilikuwa linachangiwa sana pale hawa watoto wetu wa kike wanapofikia hedhi.
"Kwa hiyo wanapokosa huduma hiyo wakati mwingine wanapopata hedhi wanabaki nyumbani, wanajua wakifika shuleni hakuna utaratibu wa kupata huduma hiyo, kwa hiyo kwa sasa kwa sababu, elimu inatolewa na huduma hii inatolewa itasaidia sana kuboresha taaluma shuleni kwa watoto wa kike.
"Na hii inajidhirisha kwa matokeo yetu ya miaka miwili ya kumaliza elimu ya msingi, watoto wa kike wamepata ufaulu mzuri kushinda watoto wa kiume.
"Kwa sababu huduma hii inapowafikia wanakuwa hawana wasiwasi, wakati wa masomo wanahudhuria, kwa hiyo mazingira hayo yanwafanya kufanya vizuri kwa upande wa taaluma.
"Kwa hiyo, niwashukuru sana akina mama wote walioguswa na hili na hasa kina mama ambao wametengeneza utaratibu wa kuweza kupanua hii huduma kwa shule zote za Manispaa ya Temeke ninaamini kwa kufanya hivyo itasaidia sana kuinua taaluma yetu ya Manispaa ya Temeke,"
HQ Tanzania
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HQ Tanzania ambao ni watengenezaji na wasambazaji wa pedi za HC,Selina Godfrey Letara amesema, "leo nimejisikia furaha sana kuwasaidia watoto wa kike kupata pedi.
"Kwa sababu, hizi taulo za kike zimekuwa ni changamoto kubwa sana kwenye shule nyingi, mimi nimeenda mpaka kwenye shule za vijijini mpaka Mwanza huko Misungwi, kwa hiyo mtoto akiingia darasani anakuwa hayuko huru, kwa sababu anakuwa labda amevaa kitambaa anaogopa atachafuka.
"Kwa hiyo, wanawake wa Millennium waliponiambia,nikawaambia nitawasaidia, ni siku mbili tu, kwa hiyo nikaongea na uongozi wa HQ Tanzania nikaomba fungu nikapata katoni 300.
"Ninashukuru sana kwa hawa wamama kitu ambacho wamekianzisha ni kikubwa sana, wameanzia kwa Shule ya Mtoni, lakini baadae watakwenda shule nyingine nami nitakuwa nao bega kwa bega,"amefafanua Letara.
Aidha, kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) juu ya masuala ya maji na usafi mazingira shuleni ya mwaka 2018 inaonesha asilimia 66.8 ya shule ndizo zina huduma ya hedhi salama.
Pia,kati ya hizo zilizobainika kuwa na viteketezi ni asilimia 24 huku asilimia 22.8 zinatupa taka kwenye mashimo na 19.5 zina vichomea taka visivyokidhi.
Licha ya jitihada za Serikali na wadau bado tatizo la hedhi salama shuleni ni pana na linahitaji mikakati endelevu ambayo ni jumuishi kwa watu wote ili kuweza kuwapa uhakika watoto wa kike kusoma salama wakiwa shuleni kipindi cha hedhi.