MBEYA-Wakulima wapatao 50 kutoka Makambako Mji wamenufaika na elimu ya matumizi sahihi ya mbolea mara baada ya kutembelea banda la Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) katika maonesho ya nanenene yanayoendelea katika viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.
Akizungumza na wakulima hao leo tarehe 6 Agosti, 2023 bandani hapo, Afisa Udhibiti Ubora wa TFRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Henerico Renatus aliwataka wakulima kutumia mbolea mara baada ya kupima afya ya udongo na kubaini aina ya virutubisho vinavyohitajika katika udongo huo.
Alisema, kutumia mbolea kwa mazoea kunapelekea kuweka mbolea isiyohitajika kwenye udongo huo na kusababisha mkulima kupoteza pesa kutokana na aina ya mbolea iliyotumika kutokuongeza tija kwenye zao husika.
Akizungumza kuhusu matumizi sahihi ya mbolea, Heneriko ameeleza kuwa, kuna kanuni nne za matumizi sahihi ya mbolea ikiwa ni kutumia mbolea sahihi kwa kiwango sahihi, wakati sahihi na sehemu sahihi.
Akifafanua kuhusu kanuni za matumizi sahihi ya mbolea, Heneriko amesema kila zao lina mahitaji yake ya mbolea ambayo hutofautiana kulingana na zao husika na kuwataka wakulima kuchagua mbolea sahihi kulingana na virutubisho vilivyopo kwenye mbolea husika na mahitaji ya zao husika pamoja na afya ya udongo.
Akielezea kuhusu kiwango cha mbolea kinachopaswa kutumika kulingana na zao, Henerico ameeleza kuwa, lazima mkulima azingatie hali ya udongoo na mahitaji ya zao kabla ya kuweka mbolea na kwa upande wa sehemu sahihi ya kuweka mbolea ameeleza kuwa, mkulima anatakiwa kuweka mbolea mahala ambako mizizi inaweza kufika na kufyonza virutubisho hivyo.
Aidha, Henerico amewaeleza wakulima kuhusu namna virutubisho vinavyopotea kwenye udogo na kueleza kuwa njia ya kwanza inayosababisha virutubisho kupotea kwenye udongo ni kuchujika ambapo virutubisho kwenye mbolea za madini huyeyuka na kunyonywa kwa urahisi na mmea pia huchujika kwenda chini zaidi ya mizizi hususan kirutubisho cha nitrojeni.
Ameeleza njia yingine ni mvuke na kuhama kwa virutubisho (Run off) kunakoweza kutokea wakati wa mvua kubwa au mafuriko.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima kutoka Makambako, mkulima Burton Sadaka Sanga wa tawi la Azimio Kata ya Mwembetogwa alisema amenufaika na elimu inayomtaka kuhakikisha anapima afya ya udongo kabla ya kutumia mbolea katika shamba lake, aidha kutokutumia mbolea wakati wa mvua ama jua kali na kuelezwa kuwa, wakati mzuri anaopaswa kutumia mbolea ni wakati udongo unapokuwa na unyevunyevu.
Sanga ameahidi kuelimisha wakulima wengine ambao hawakupata nafasi ya kuhudhuria kwenye maonesho ya nane nane mwaka huu ili na wao waweze kuongeza tija kwenye kilimo chao.
Naye mkulima Cleopa Lufumbe ameishukuru serikali kwa kuwakumbuka wakulima na kutoa mbolea za ruzuku zilizosaidia kuongeza tija katika kilimo chao na kuwataka wakulima kuhakikisha wanapima afya ya udongo kabla ya kutumia mbolea.