NA FRESHA KINASA
WANAKIJIJI katika Jimbo la Musoma Vijijini lililopo mkoani Mara wameamua kufufua mradi wa ujenzi wa zahanati yao huku Mbunge wa jimbo hilo, Mheshimiwa Prof. Sospeter Muhongo akichangia saruji mifumo 200.
Kijiji cha Chimati cha Musoma Vijijini ni moja ya vijiji vitatu vya Kata ya Makojo. Vijiji vingine ni Chitare na Makojo.Kwa muda wa miaka mingi,kata hii yenye vijiji vitatu ilikuwa inahudumiwa na zahanati moja tu ya Kijiji cha Chitare.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Agosti 12, 2023 na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini ambayo imefafanua kuwa, utoaji wa huduma za afya kwenye Kata ya Makojo inaenda kubadilika kwa maboresho makubwa.
"Kituo cha Afya cha kata hii kimejengwa kijijini Makojo. Kijiji cha Chimati kimeamua kufufua mradi wa ujenzi wa zahanati yao ulioanza mwaka 2018 na kusimama hadi leo.
"Mbunge wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo ameungana tena na Wana-Chimati kuendelea na ujenzi wa zahanati ya kijiji chao.Ujenzi ulipoanza mwaka 2018, Mbunge huyo alianza kutoa michango yake kwa kuchangia saruji mifuko 50."
"Jumatano ya Agosti 10,2023, Mbunge huyo akiambatana na Kamati ya Siasa ya CCM ya Wilaya ya Musoma Vijijini, aliendesha harambee kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho."
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, harambee hiyo katika Kijiji cha Chimati wanakijiji na wazaliwa wa hapo walitoa saruji mifuko 123,Kamati ya Siasa (CCM) ya Wilaya saruji mifuko 25,Mbunge wa Jimbo saruji mifuko 200.
Aidha,kero na matatizo yaliyowasilishwa na wananchi wa Kata ya Makojo,Mbunge wa Jimbo alipokea kero na matatizo yanayowakabili wananchi, na kuyatolea majibu.
Mwenyekiti wa chama wilaya,Denis Ekwabi na Katibu wa Chama Wilaya (CCM),Valentine Maganga walijibu maswali yaliyoelekezwa kwenye chama. Vlevile, walitoa elimu na ufafanuzi kwa masuala mengine yaliyoulizwa.
Jimbo la Musoma Vijijini linaendelea kuboresha utoaji wa Huduma za Afya na takwimu za sasa ni hizi hapa:Hospitali ya hadhi ya Wilaya:
1 (moja), imeanza kutoa huduma
Vituo vya Afya (6)
2 vinatoa huduma
2 vinatoa huduma kwa hadhi ya Zahanati
2 ni vipya vinasubiri kufunguliwa
Zahanati 42
24 zinatoa huduma (za Serikali)
14 zinajengwa (Wananchi & Serikali, baadhi)
4 ni za Binafsi
Picha zilizoambatanishwa hapa juu zinaonesha matukio mbalimbali ya tarehe Agosti 10, 2023 ya Harambee ya Kijiji cha Chimati ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini.
Mbali na hayo,tenki la maji la ujazo wa lita 75,000 (pichani) linakamilishwa ujenzi Kijiji cha Chimati kwa ajili ya maji ya bomba ya kijiji hicho.
Pia, wananchi na viongozi wote wa Jimbo la Musoma Vijijini wanaendelea kuishuruku Serikali chini ya uongozi mzuri wa Mhe. Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwapatia fedha za miradi mbalimbali ikiwemo ya Sekta ya Afya.