NA WITNESS MASALU
WMJJWM
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto.
Sambamba na Ajenda ya Taifa ya kuwekeza kwa vijana balehe na utekelezaji wa ahadi za nchi kwenye Jukwaa la Usawa wa Kijinsia ni baadhi ya maeneo yanayopewa kipaumbele katika utekelezaji wa afua mbalimbali kimkakati kutokana na umuhimu wake kwa jamii.
Waziri Gwajima ameyasema hayo jijini Dodoma leo Agosti 17, 2023 alipokutana kwa mazungumzo na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini, Elke Wisch.
“Serikali imekua mstari wa mbele katika kuboresha hali ya maisha kwa wananchi wake kwa kuja na afua mbalimbali za Kimaendeleo zinazogusa makundi yote katika Jamii kupitia Maafisa Maendeleo na Ustawi wa Jamii japokuwa changamoto ya upungufu wa maafisa bado ipo."
Amesema ili kuhakikisha tunakuwa na Taifa lililo bora ni lazima kuanza kuwekeza kwa watoto na kwamba Serikali imeshaanza kutekeleza afua ya malezi na Makuzi ya awali katika vituo kadhaa hivyo jitihada za kuongeza zinafanyika.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu amesema Serikali imeendelea kutengeneza mazingira salama kwa watoto katika kuwainua wanawake.
“Kuimarisha hali ya uchumi kwa wanawake ambao ni moja ya njia za kutengeneza mazingira bora na salama kabisa kwa ajili ya Watoto nchini kwani wao ndiyo washiriki wakubwa wa malezi katika Jamii,"amesema Dkt Jingu.
Naye, Elke Wisch ameahidi Shirika hilo litaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Serikali ili kuhakikisha Taifa linafikia malengo yake katika kuboresha maisha ya Wananchi wake.