NA MUNIR SHEMWETA
WANMM
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa soko la Madini ya Tanzaniate katika mji mdogo wa Mererani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula (katikati) akipata maelezo ya ujenzi wa mradi wa soko la Madini ya Tanzanite kutoka kwa mhandisi wa jengo hilo wakati wa kukagua mradi huo wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara tarehe 3 Agosti 2023.
Ujenzi wa mradi wa soko hilo unatekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) chini ya mshauri Chuo cha Ufundi Arusha kwa gharama ya shilingi bilioni 5.49.
Akizungumza alipotembelea mradi huo Agosti 3, 2023 wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara Dkt Mabula alisema, kuwepo kwa soko la madini nchini kutaifanya Tanzania kujulikana zaidi sambamba na kukaribisha watu kutoka nje ya nchi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt Angeline Mabula akipata maelezo ya Maendeleo ya ujenzi wa mradi wa soko la Madini ya Tanzanite alipokwenda kuukagua wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara tarehe 3 Agosti 2023.
”Tuna imani hata wafanyabiashara wa madini hayo kutoka tanzania sasa ili kuweza kulinda rasilimali ya nchi na kuhakikisha kwamba ‘exporter’ mkubwa wa madini ya tanzanite ni yule anayetoka kwenye nchi yake pamoja na kuwa na soko,”alisema Dkt. Mabula.
Alitoa rai kwa wamiliki wa soko hilo la madini ya Tanzanite kuona namna bora ya kujitangaza zaidi ikiwemo kutumia tovuti huku wakionesha kuwa soko hilo la madini liko Tanzania na Mererani ambapo ndiko madini yanakochimbwa.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt.Angeline Mabula (kushoto) akiwa katika stoo ya kuhifadhia vifaa vya ujenzi wakati alipofanya ukaguzi wa Maendeleo ya ujenzi wa Soko la Madini ya Tanzanite wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara tarehe 3 Agosti 2023.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, matangazo ya kulitangaza soko hilo yanaweza kuanza mapema wakati ujenzi ukiendelea ili ifahamike kuwa madini hayo yanapatiakana nchini na soko lake liko Mererani jambo alilolieleza litaongeza juhudi za kulinda rasilimali za nchi.
Alimpongeza mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro na timu yake kwa kuwa na wazo la kuwa na soko la madini ya Tanzanite katika mji mdogo wa Mererani ambapo alisema uamuzi huo unaenda kufungua fursa kwa watanzania lakini pia kwa nchi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt.Angeline Mabula (wa pili kushoto) akielekea kukagua Maendeleo ya ujenzi wa mradi wa soko la Madini ya Tanzanite alipofanya ziara katika mradi huo tarehe 3 Agosti 2023.
Awali Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mkoa wa Kilimanjaro Juma Kiaramba alimueleza Waziri wa Ardhi Dkt Mabula kuwa, ujenzi wa soko hilo ulianza rasmi tarehe 22 Mei 22, 2022 na unatarajia kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu wa 2023.
Muonekano wa ujenzi wa Soko la Madini ya Tanzanite lililopo katika mji mdogo wa Mererani wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).
Kiaramba alisema, ujenzi wa mradi huo unaendelea vizuri ingawa shirika lake linakabiliwa na changamoto kubwa ya kupanda kwa gharama za vifaa vya ujenzi.
Amesema, katika kukabiliana na hali hiyo shirika lake limekuwa likinunua vifaa vikubwa kutoka vyanzo vya uzalishaji na kutolea mfano wa nondo na saruji ili kuhakikisha gharama za ujenzi zinabakia kama ilivyo.