NA BENNY MWAIPAJA
Beijing-China
WAZIRI wa Fedha, Mhe. Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba, ametoa wito kwa Kampuni ya Mawasiliano ya Huawei ya China, kuisaidia Tanzania kuweka mifumo ya kisasa ya teknolojia ya mawasiliano.
Ni mifumo itakayowezesha nchi kuboresha ukusanyaji mapato yake ya ndani na kupunguza malalamiko ya watumiaji wa mifumo hiyo wakiwemo wafanyabiashara.
Waziri wa Fedha wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), na ujumbe wake wakisikiliza maelezo kutoka kwa mtaalam wa mambo ya utafiti na stratejia ya mifumo ya TEHAMA wa Kampuni ya Mawasiliano ya Huawei Bw. Chu Wantao, namna walivyofanikiwa kufunga mitambo inayozuia madereva kufanya makosa ya barabarani wanapoendesha vyombo vya usafiri vya moto, ikiwemo kuongea na simu, ulevi nk. walipotembelea Kampuni ya Huawei, Tawi la Beijing, China na kujadili masuala ya uwekezaji wa Kampuni hiyo nchini Tanzania.
Dkt. Nchemba ametoa Rai hiyo Beijing nchini China alipoongoza Ujumbe wa Tanzania kutembelea Kampuni hiyo Tawi la Beijing ambapo masuala kadhaa ya uwekezaji wa Kampuni hiyo nchini Tanzania, yalijadiliwa.
Alisema kuwa, mifumo iliyopo nchini ya kukusanya mapato ya ndani ya Serikali haisomani (haiwasiliani ipasavyo) na kuzua malalamiko kutoka kwa watumiaji lakini pia hali hiyo inaikosesha Serikali mapato.
Waziri wa Fedha wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), na ujumbe wake wakisikiliza maelezo kutoka kwa mtaalamu wa mambo ya utafiti na stratejia ya mifumo ya TEHAMA wa kampuni ya Mawasiliano ya Huwaei Bw. Chu Wantao, namna walivyofanikiwa kujenga mifumo ya kuboresha elimu kwa kutumia TEHAMA pamoja na matumizi ya nishati jadidifu, walipotembelea Kampuni ya Huawei, Tawi la Beijing, China na kujadili masuala ya uwekezaji wa Kampuni hiyo nchini Tanzania.
Dkt. Nchemba aliyeambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali Dkt. Natu Elimaamry Mwamba, Balozi wa Tazania nchini China Mhe. Mbelwa Kairuki na Viongozi wengine wakuu wa Taasisi za Serikali ikiwemo Tanroads na Shirika la Reli Tanzania TRC, alisema kuwa ujumbe wa Tanzania umejionea mageuzi makubwa ya Teknolijia ya Habari na Mawasiliano TEHAM iliyobuniwa na Kampuni hiyo.
Alisema kuwa miaka michache iliyopita Kampuni hiyo ilikuwa ni ya kawaidia lakini baada ya kuwekeza kwenye utafiti wa tenolojia janja, Huawei imekuwa Kamouni kubwa na inayoheshimika ulimwenguni na kwamba inaweza kuisaidia Tanzania kuboresha mifumo yake ya ukusanyaji mapato yake kwa njia ya kodi mbalimbali.
Waziri wa Fedha wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), na akizungumza jambo wakati akiongoza Ujumbe wa Tanzania walipotembelea na kufanya mazungumzo ya kiuwekezaji na uongozi wa Kampuni ya Mawasiliano ya Huawei ya China, alipofanya ziara ya kikazi katika kampuni hiyo Tawi la Beijing na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Huawei Bw. Zhang (Katikati). Aliyevaa nguo nyekundu ni Katibu Mkuu-Wizara ya Fedha Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa TRC Bw. Masanja Kadogosa na kulia ni Kamishna wa Idara ya Usimaizi wa Deni la Serikali, Bw. Japhet Justine.
Aidha, Dt. Nchemba ameuomba uongozi wa Kampuni hiyo ambao uliongozwa na Makamu wake wa Rais Bw. Zhang kwenye mazungumzo hayo, kutoa nafasi kwa vijana wa kitanzania za kuongeza ujuzi wa masuala ya TEHAMA kwa kuwapa nafasi ya kujifunza kwa vitendo kwenye Kampuni hiyo ili nchi iwe na vijana wabobezi kwenye masuala ya mawasiliani hivo kukuza ajira na kujiongezea kipato.
Aliiomba pia Kampuni hiyo kuwekeza nchini Tanzania kwa kujenga kiwanda cha kutengeneza simu janja ili wananchi hususan waishio vijijini wapate simu janja kwa bei nafuu na ziwasaidie katika kazi zao za kujipatia kipato na kwamba soko kubwa la ndani ya nchi na nchi jirani ni kivutio kikubwa cha uwekezaji huo.
Waziri wa Fedha wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), akipokelewa na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Mawasiliano ya Huawei Bw. Zhang, Alipoongoza ujumbe wa Tanzania kutembelea Kampuni hiyo mjini Beijing, China, na kujadili masuala ya uwekezaji wa Kampuni hiyo nchini Tanzania.
Katika ziara hiyo Mhe. Dkt. Nchemba aliambatana na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Balozi wa Tanzania-China- Balozi Mbelwa Kairuki, Mkurugenzi Mkuu wa Shirila la Reli Tanzania (TRC), Bw. Masanja Kadogosa, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, Kamishna Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali-Bw. Japhet Justine na Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Melkizedeck Mbise(Picha na Wizara ya Fedha-Beijing).
Akizungumza kwa niaba ya Makamu wa Rais wa HUWAEI Bw, Zhang, Meneja wa Huawei Tawi la Tanzania Bw. Russel Zhao, alisema kuwa Kampuni yake imepokea mamobi ya Serikali kupitia kwa Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba na kwamba itaangaza fursa mbalimbali zinazopatikana nchini Tanzania na kuwekeza mitaji na teknolojia.
Alisema kuwa uhusiano mzuri na wa muda mrefu uliopo kati ya China na Tanzania unaendelea kuleta hamasa na kwamba Kampuni hiyo itaangalia uwezekano wa kurejesha Ofsi yake Tanzania kwa hivi sasa wanafanya shughuli zao nchini Tanzania kutokea nchi Jirani ya Kenya.