Afya ya Profesa J imeimarika, shukurani kwa Rais Dkt.Samia

DAR ES SALAAM-Rais mstaafu wa Awamu ya Nne,Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete ameelezea kufarijika zaidi baada ya kutembelewa nyumbani kwake na msanii wa hip pop,Joseph Leonard Haule (Profesa J au Wa-Mitulinga).

"Leo nimetembelewa na Profesa J nyumbani kwangu Kawe. Ni furaha iliyoje kuona afya yake imeimarika. Hakika Mwenyezi Mungu ni mkubwa!,"ameandika Mheshimiwa Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete.

Februari 11, 2022 Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ilitangaza kugharamia matibabu ya Profesa J.

Ni baada ya Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu kumtembelea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa akipatiwa matibabu ili kumjulia hali.

"Nimefika kuleta salamu za Rais Samia Suluhu Hassan ambaye yupo safarini nje ya nchi, amesema kuwa, anatambua mchango wa Profesa J akiwa Mbunge wa Mikumi.

"Lakini, pia kazi zake za sanaa ambazo zimehamasisha vijana wengi kujiajiri kupitia muziki.Hivyo, kuanzia sasa, Serikali itagharamia matibabu yake hadi hapo atakaporuhusiwa kutoka hospitalini na ninauagiza uongozi wa hospitali kuleta bili zote wizarani kuanzia sasa,"alieleza Waziri Ummy.

Msanii huyo aliyevuma na kibao cha Hapo Vipi huku akiwa na albamu za Machozi Jasho Na Damu, Aluta Continua, Mapinduzi Halisi, J.O.S.E.P.H ni baba wa familia ambaye pia amewahi kuhudumu katika siasa, kwa siku za karibuni alikuwa akipigania afya yake.

Ugonjwa wa rapa huyo ambaye alihamia katika fani ya siasa ulikujia miaka miwili baada ya kupata pigo kubwa la kupoteza kiti chake cha Ubunge katika Jimbo la Mikumi mkoani Morogoro baada ya kuhudumu kwa muhula mmoja pekee.

Profesa J alibwagwa na Dennis Londo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye alipata kura 31,411 dhidi ya Profesa Jay aliyezoa kura 17,375.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news