AICC yatoa ahadi kwa BoT kusaidia kuimarisha akiba ya fedha za kigeni

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC),amemuahidi Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba kwamba, kituo hicho kitashiriki kikamilifu kusaidia kuimarisha akiba ya fedha za kigeni nchini.

Ametoa ahadi hiyo Septemba 14, 2023 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini ambavyo vinaratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Dhamira ya vikao hivyo ni kuwezesha umma kufahamu taasisi na mashirika yote ambayo yapo chini ya ofisi hiyo yalipotoka, yalipo na yanapokwenda ili kuyafahamu kwa kina kwa sababu wao ndiyo wamiliki wakuu.

"Kwa hiyo AICC inasema, Mheshimiwa Gavana hiki ndiyo kituo cha kukupa dola za Kimarekani.Tumejipanga kwa umakini mwaka huu tutaliingizia Taifa zaidi ya dola za Kimarekani milioni 48.

"Lakini, pia tuna mikakati tunayokwenda kuifanya, tunaamini tuna uwezo wa kufanya zaidi ndani ya miaka mitano ijayo, tumejiwekea malengo ya kuwa na mikutano 50 ya watu 2000, na iwapo wakikaa kwa siku nne ni dola za kimarekani milioni 160,"amefafanua Mafuru.

Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kilianzishwa chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma Na.17 ya mwaka 1969 kwa agizo la Rais kupitia tangazo la Serikali namba 115, lililochapishwa tarehe 25 Agosti 1978.

AICC kinamilikiwa na Serikali ya Tanzania na kinafanya kazi chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kinafanya kazi kama shirika kamili la kibiashara huku utoaji wa huduma za mkutano ndio biashara kuu.

Hata hivyo, AICC pia hukodisha ofisi katika majengo ya makao makuu na makazi katika Manispaa ya Arusha. Kituo kinatoa huduma za afya kupitia hospitali yake iliyopo Manispaa ya Arusha.

AICC pia inamiliki na kuendesha Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) kilichopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

JNICC ni Kituo cha Mikutano kilichojengwa kwa madhumuni mengi katika Jiji la Dar es Salaam, chenye teknolojia ya kisasa ya sauti-video, mawasiliano na habari.

"JNICC ni kituo ambacho tulikabidhiwa na Serikali miaka tisa iliyopita ili tuweze kukiendesha na chenyewe kiko chini ya AICC kwa hiyo makao makuu yako Arusha tunakiendesha pamoja kama entity moja.

"Tunaamini fursa zilizopo katika diplomasia ya uchumi ni kubwa, Dodoma inahitaji kuwa na kituo kikubwa pia tunahitaji kwenda Zanzibar, kwa hiyo itafika mahali tunaweza kusema tunaanzisha taasisi nyingine kwa hiyo vituo hivi vina mchango katika uchumi.

Utalii

"Arusha kama kitovu cha utalii, na sisi kama wenyeji wa uchumi wa mikutano, tunachangia pia katika Sekta ya Utalii. Kwa hiyo,sekta hii haifanyi kazi peke yake,kwa mwaka huu tukifanya mikutano 30 ikawa na watu 1000 tu,na wakakaa siku nne tu, na kila mmoja akatumia dola 400 tu, hizi ni sawa sawa na dola milioni 48.

"Kwa hiyo Kituo cha AICC na JNICC kwa mikutano 30 ambayo ninaamini tutafika, tutaingizia uchumi wa nchi hii dola milioni 48, hii ni sawa sawa na kama shilingi bilioni 120 za Kitanzania kwa exchange rate ya leo,"amefafanua Mafuru.

Mkurugenzi Mtendaji huyo anasema, kuwa inakadiriwa kwa wastani Afrika idadi ya watu 396 wanashiriki kwa mkutano mmoja, na katika hao watu wanakaa siku nne kwenye hiyo nchi wanayokwenda.

"Wanapokuwa katika hizo nchi ngoja nianzie hapa nchini. Kwamba wakiwa Afrika wanatumia dola 290 kwa siku, lakini watu hao hao wakiwa Tanzania wanatumia dola 423.

"Kwa hiyo mchango wa sekta hii kwa Afrika ni dola 459,360 (396x290x4), lakini kwa Tanzania ni 670,032 (396x423x4)."

Mikakati

Mafuru amesema, kwa kutambua mchango mkubwa katika uchumi kupitia Diplomasia ya Uchumi wamejiwekea mikakati mbalimbali ili kuimarisha huduma zao na waweze kuhudumia mikutano mingi zaidi ya ndani na nje ya nchi.

Amesema, licha ya maboresho makubwa ambayo wanaendelea kuyafanya katika vituo na miradi yao, pia wanatarajia kujenga kituo kikubwa zaidi jijini Arusha cha The Kilimanjaro International Convention Centre (KICC).

Pia, mikakati mingine ni kuongeza ushirikiano na wadau muhimu ikiwemo Bodi ya Utalii Tanzania (TTB),Shirika la Ndege la Air Tanzania, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania.

Sambamba na, watoa huduma za watalii wenye hoteli, wafanyabishara, balozi za nje, TANAPA, Ngorongoro Conservation, NHC na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Mafuru amesema,AICC wanamiliki nyumba na ofisi mbalimbali ambazo wanaendelea kuziboresha na kuziendeleza ili kuongeza kipato kwa taasisi na shirika.

Pia, amesema Hospitali ya AICC ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 90,000 kwa mwaka, hivyo licha ya kutoa huduma ya afya pia imekuwa sehemu ya kutengeneza mapato kwani inahudumia watu kutoka ndani na nje ya nchi.

"AICC ina nyumba za kupangisha mpaka leo asubuhi tuna vyumba vya kupangisha 624, lakini miongoni mwa hizo zina apartment 48, lakini pia pale AICC tuna ofisi zenye ukubwa wa square mita 23,000, ambazo huwa tunapangisha kwa taasisi kadhaa.

"Tunaendelea kuwekeza na kuboresha kuhakikisha kwamba tunapata mapato, pia tuna Hospitali AICC hii miaka ya nyuma ndio ilikuwa hospitali kubwa katika Kanda ya Kaskazini.

"Na kwa wastani inahudumia zaidi ya wagonjwa 7,500 kwa mwezi na kwa ujumla ina uwezo wa kuhudumia wageni 90,000, toka Kanda ya Kaskazini na wengine wanaokuja katika mikutano huwa tunawahudumia.

"Pia AICC imeshiriki katika matukio mengi na imekuwa kitovu cha vijana wanaoleta amani katika ukanda huu wa Afrika wapo wastaafu, kina Mkapa, Nelson Mandela wamefanya kazi kubwa kusaidia nchi nyingi za Afrika na hasa migogoro mikubwa kuitatua.

Mikutano

Mafuru amesema, miongoni mwa mikutano ya karibuni ambayo wameifanikisha kwa mafanikio makubwa ni pamoja na Africa Human Capital Heads of State Summit,The Africa Food Systems Forum na mingineyo.

"Mwezi wa sita tulikuwa na wageni 1200, lakini wanaotoka nje ni wageni 1000, hiki ni Chama cha Madaktari tulikuwa na EU wageni 800, kati yao 600 walitoka nje ya nchi.

"Human Capital Summit, Mheshimiwa Rais na viongozi wengine zaidi ya 14 toka nchi za Afrika walikuwepo wageni 1800, na 1000 zaidi walitoka nje ya nchi.

"Wiki iliyopita kulikuwepo na viongozi wa Africa Food Systems Summit zaidi ya wageni 5400, na wageni 3000, walitoka nje ya nchi.

"Sasa tukasema tufanye wastani wa 1000 ukiwa na wageni 1000 wakaja hapa Tanzania kwa muda wa siku nne, utatengeneza dola milioni 1.6 za Kimarekani kwa mkutano mmoja.

"Sisi tukajipima kwa mwaka, mwaka jana juhudi zilizofanyika tulikuwa na mikutano 18, sisi tumejiwekea lengo la mikutano 30 mwaka huu na ukiona sasa hivi toka mwaka umeanza tuna mikutano zaidi ya minne au mitano yote ya Kimataifa.

"Bado tuna miezi tisa mingine katika mwaka huu wa fedha, tunaamini tutafika mikutano 30 na kuzidi, tukifanya vizuri tukawa na mikutano 30, tukawa na watu 1000 tu, na wakakaa siku nne na kila mmoja akatumia dola 400 tu, hizi ni sawa na dola milioni 48.

"Kwa hiyo Kituo cha AICC na JINCC kwa mikutano 30 ninaamini tutafika na tutaingizia uchumi wa nchi hii dola milioni 48, hizi ni sawa sawa na shilingi bilioni 120 za kitanzania.

"Kama mikutano iliyopita tulikuwa na watu zaidi ya 1000, kwa mfano tukiwa na watu 2000 katika mkutano fedha zitaongezeka hadi shilingi bilioni 240 ambazo ni zaidi ya dola milioni 90 za kimarekani,

"Hili jambo linawezekana, kwa miaka iliyopita performance haikuwa nzuri na tulikuwa tukijiendesha kwa hasara, kulikuwa na uchakavu wa miundombinu yetu na wageni walitukimbia, kwa hiyo uchumi wa mikutano uli-shake Dunia nzima.

"Lakini baada ya mapato yetu kushuka yameanza kuongezeka,kama ambavyo mnaona tulikuwa na bilioni 11, tukaenda bilioni 14 lakini tumekwenda bilioni 18 kwa hesabu zilizoishia Juni, mwaka huu, hapa leo tulipo hatujafanya mambo mazuri sana.

"Lakini tumekuwa kwa asilimia 27 mwaka hadi mwaka kuanzia mwaka 2022 hadi mwaka 2023, kwa hiyo kwa hesabu zilizowasilishwa kwenye ripoti rekodi zetu zilikuwa kama bilioni 18, vituo vyetu vya mikutano ndio vinaleta fedha nyingi ikifuatiwa na hospitali.

Tathimini

"Tunaamini Serikali ina mpango mkakati wa kufanya evaluation ya performance ya taasisi zake, evaluation ya bodi na sisi kama kituo tumejipanga waweze kupima kwa kile tunachofanya.

"Kitu cha kwanza tunakwenda kusaini performance objectives kwa team hawa mnaowaona, ni sehemu tu ya wafanyakazi wa AICC.

"Kila mmoja atakuwa na objectives performance. Mimi nitasaini na wanaoripoti kwangu, na wanaoripoti kwao kwa hiyo hatutakuwa na salia Mtume kwa yeyote yule ili kuleta ufanisi. Tutasaini kila baada ya miezi mitatu, tutakaa kuona nini kimefanyika sitaweza kukubali nasema mbele ya wahariri.

"Pia tutakwenda kutengeneza activities za AICC na JINCC. Tuna fursa zilizopo katika sekta husika,tulifanya survey miezi michache iliyopota ziko hoteli Dar es laam, idadi ya vyumba na bei ya hivyo vyumba na Mkoa wa Arusha kuna hoteli na hivyo vyumba data hii ni endelevu kuna zingine zinatoka zingine zinaingia.

"Ili tunapokwenda ku-market tunaongelea kila kitu kinachohusika kwenye mnyororo wa thamani wa uchumi wa kidigitali,"amefafanua kwa kina Mafuru.

Duniani

Wakati huo huo, Mafuru amebainisha kuwa, AICC na JINCC ni mwanachama wa Taasisi ya AIPC (The International Association of Convention Centres) ambayo inaviunganisha vituo vyote ambavyo vinatoa huduma za mikutano duniani.

"AICC na JNICC ni members wa taasisi inayoitwa AIPC, hii ni taasisi inayounganisha sekta zote ambazo zinaandaa mikutano duniani.

"Kwa hiyo association hii inatusaidia sisi kama kituo cha mikutano kuweza kupata taarifa za utafiti wa sekta, lakini kuendeleza uwezo wa wataalamu wetu na kuweza kushare-experience na kujua mambo yanayotokea katika sekta hii ya diplomasia ya mikutano.

"Kujua mchango wa sekta hii ni upi, ajira za sekta hii na kuangalia mchango wa GDP katika dunia nzima ukiangalia hapa inatoa nafasi kubwa ya nafasi za kazi.

"Na mchango wake katika Global GDP ni dola za kimarekani Trilioni 1.62 ambazo ni kubwa zaidi ya makampuni yote ya simu duniani, hebu chukua hapa Tanzania leo makampuni yote ya simu yaliyopo mchango wake kwa taifa sekta hii mchango wake ni mkubwa sana.

"Na mnaweza kuona mchango wake ni mkubwa sana, katika Africa AICC na JINCC tunaposhiriki katika mikutano na wenzetu mwaka 2019 kabla ya UVIKO-19 Afrika iliandaa mikutano 450. Lakini trend hii ikashuka wakati wa UVIKO-19 kila mmoja alishuka.

"Lakini baada ya UVIKO-19 mwaka 2022 imefanyika mikutano kama 200 na kitu au 180, lakini ukija Tanzania tuliandaa mikutano 15 kabla ya UVIKO-19 tukashuka mpaka mkutano mmoja, lakini baada ya UVIKO-19 Tanzania imepanda mpaka kuandaa mikutano 18 mwaka 2022.

Wageni nchini

"Sasa Tanzania inaonesha kukua kwa kasi kuliko Afrika, maana yake wageni wameipenda Tanzania na wanakuja zaidi Tanzania, pia kuna kitu fulani ambacho kimefanyika kimeleta mageuzi haya, kwa nini sasa Tanzania imeweza kupendwa zaidi?.

"Kwa hapa naomba nisimumunye maneno, namshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Hassan kwa kazi kubwa ya kuifungua nchi, najua kuna Royal Tour, lakini amekuwa akifanya mikutano mbalimbali ya kuitangaza Tanzania na kuwakaribisha wageni.

"Wageni hawa wanapokuja, wanakuja kwa mambo mbalimbali, mojawapo ni kushiriki katika diplomasia ya mikutano, kwa hiyo tumepata mialiko mingi kutoka nchi mbalimbali za Afrika na duniani ambao wanakuja Afrika na Tanzania kwa mara ya kwanza.

"Tanzania imeonekana unique kuliko nchi nyingine za Afrika, hii ni kutoka na uongozi thabiti wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwavuta wageni hao.

"Miaka minne iliyopita tulikuwa wa 13 kwa kuandaa mikutano na tulikuwa na asilimia 5, lakini baada ya kampeni kubwa ya kuifungua nchi Tanzania imepanda hadi nafasi ya tano kwa kuandaa mikutano 18 ambayo ni asilimia 10 ya market share ya Afrika.

"Kwa hiyo mikutano yote ya Africa iliyofanyika 180, tumeandaa mikutano 18 kwa hiyo tuna ten percent ya market share ya Afrika kwa kuandaa mikutano hii.

"Sisi kama AICC tunaendelea na juhudi mbalimbali, kuna nchi kama Afrika Kusini, Morocco, Rwanda na Misri ziko mbele yetu tunafanya analysis kuangalia wanatushinda wapi?. Tunaandaa sasa mkakati kuweza kupanda kwa haraka,"amefafanua Mafuru.

Pia, Mafuru amesema kuwa, utajiri wa miaka wa 45 ya historia ya AICC pamoja na wito wake wa We Bring the World to Tanzania (Tunaileta Dunia Tanzania), unakwenda kudhihirishwa na mkakati wake kwa kuhakikisha wanaandaa mikutamo ya kimataifa ambayo imekuwa ikiitangaza Tanzania katika ramani ya Dunia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news