ARUSHA-Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt.Doto Biteko amesema, kama Serikali haitafanya Tathmini ya Shughuli zake haitakuwa na uwezo wa kujipima na vihatarishi vya utekelezaji wa mipango yake.
Dkt.Biteko ameyasema hayo Septemba 12, 2023 jijini Arusha alipofungua Kongamano la Pili la Kitaifa la Ufuatiliji, Tathmini na Mafunzo.
Amesema, Serikali imegawanyika katika maeneo mengi kama vile Serikali Kuu na Serikali za Mitaa hivyo ufuatiliaji na tathmini ni eneo muhimu na linalopaswa kutiliwa mkazo.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt.Doto Biteko akimkabidhi tuzo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Mhe.Jenista Mhagama wakati wa Kongamano la Pili la Wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini lililofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa AICC jijini Arusha.
Kutokana na umuhimu huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan anasisistiza Serikali kuwa na uratibu wa shughuli zake.
“Unaweza kukuta Serikali za Mitaa na Serikali Kuu kila mtu anafanya jambo lake, hakuna vinavyosomana, tujifanyie tathmini ili tusije kuwa watu wa kuduwaa kunini hili limetokeaje,”alisisitiza.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt.Doto Biteko alipotembelea Banda la Idara ya Menejimenti ya Maaafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu wakati Kongamano la Pili la Wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini lililofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa AICC jijini Arusha.
Dkt.Biteko aliongeza kuwa, asiyejifanyia tathmini atakuwa ni mtu wa hasara, hivyo kujifanyia tathmini kunaifanya Serikali kubaini matatizo mapema na kuweza kuyatafutia ufumbuzi kabla hayajaleta hasara.
Pia, ametoa wito kwa washiiriki wa kongamano hilo hasa watendaji wa serikali kufanya ufuatiliaji na tathmini bila kuweka mbele rasilimali fedha.
Sambamba na hilo, Naibu Waziri Mkuu Dkt.Biteko amewataka maafisa masuhuli wote nchini kuviwezesha vitengo vya ufuatiliaji na tathmini katika wizara na taasisi zao kwa kuhakikisha kunakuwa na wataalamu wa kutosha, vitendea kazi na rasilimali fedha ili viweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu, Mhe.Jenista Mhagama akitoa salamu wakati wa Kongamano la Pili la Wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini lililofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa AICC jijini Arusha.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshugulika na masuala ya (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe.Jenista Mhagama amesema, wakati kongamano hili likifanyika kwa mara ya pili hapa nchini, Serikali imefanyia kazi kwa asilimia 100 utekelezwaji wa agizo la uanzishwaji wa Idara za Ufuatilijaia na Tathmini katika Wizara na Serikali.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt.Doto Biteko akiwa na Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu baada ya kuhutubia Kongamano la Pili la Wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini lililofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa AICC jijini Arusha.
Awali akiongea wakati wa Ufunguzi wa Kongamano hilo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt.Jim Yonazi alisema, kwa kufuatilia mwendeno wa utekelezaji wa kujipima matokeo,taasisi za umma zinaweza kujihakikishia kuwa zipo katika njia sahihi za utekelezaji katika kufikia malengo yake, hivyo ufuatiliaji na tathmini ni njia nzuri ya kujifunza na kuwajibika.