BASATA VIBES kutikisa bara na visiwani

DAR ES SALAAM-Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo ametoa agizo kwa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lihakikishe kuwa Mradi wa Baraza wa ''BASATA VIBES ''unawafikia Wasanii mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar ili azma ya Serikali ya kukuza sanaa nchini itimie.
Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro (kushoto) na Balozi Msaidizi wa Ubalozi wa Ufaransa hapa nchini Alex David Guillon wakisaini Hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya Wizara na Ubalozi huo Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Ndumbaro ametoa agizo hilo Septamba 14, 2023 Jijini Dar es Salaam mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa Makubaliano ya Mradi wa BASATA Vibes na Kituo cha Utamaduni Cha Ufaransa hapa nchini wenye lengo la kuimarisha maonesho ya Sanaa, kutoa mafunzo kwa Wadau wa Sanaa na kuwajengea uwezo wa kuandaa matukio ya burudani.

"Kupitia Ubalozi wa Ufaransa natumia nafasi hii kwenu Ubalozi kuhakikisha mashindano ya michezo ya Olimpiki ya Paris mwaka 2024 uhusishe burudani kutoka kwa wasanii wetu, hili naomba mlizingatie sana, pia katika mashindano hayo naomba mhakikishe Watanzania wanapata nafasi za kutosha kwenye michezo hiyo kwakua vigezo vya kushiriki wanavyo,"amesisitiza Mhe. Ndumbaro.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA ) Dkt.Kedmon Mapana pamoja na Mkuu wa kituo cha Utamaduni cha Ufaransa Frola valleur kilicho chini ya Ubalozi wa Ufaransa hapa nchini wakisaini Makubaliano ya Mradi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA VIBES) Jijini Dar es Salaam. 

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) DKT. Kedmon Mapana amesema Makubaliana hayo kati ya kituo cha Utamaduni cha Ufaransa na Basata una lenga kukuza na kutafuta masoko ya kutangaza kazi za wasanii wa Kitanzania duniani.

"Makubaliano haya kati ya Basata na kituo cha Utamaduni Cha Ufaransa yataenda kukuza uchumi kwani tumeandaa matukio zaidi ya 12 kwa baadhi ya Mikoa hivyo wasanii watashiriki na watalipwa pesa zao kupitia matukio hayo."

Aidha ameongeza kuwa Malengo pia kuwajengea uwezo wa kufanya kazi maafisa Utamaduni wa baraza hilo katika kutumikia majukumu ya kisanaa nchini kwa weledi kutokana na mafunzo watakayopata kutoka Ufaransa.

Hata hivyo ameongeza kuwa Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma ataongozana na viongozi wa wizara hiyo pamoja na wasanii wanne kuelekea Ufaransa kujifunza vitu mbalimbali ili kuweza kuboresha sanaa hapa nchini.

Aidha, Mkurugenzi wa Kituo hicho Bi. Flora Valleur amesema mradi huo pia utahusisha kujifunza Lugha la Kifaransa, na kupata nafasi kwa wasanii wa Tanzania kuhudhuria na kutoa burudani kwenye majukwaa ya burudani ya nchi hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news