Bei ya shilingi milioni 1.5 au 500,000/- kwa kilo ya Vanila haipo duniani-Waziri Bashe

DAR ES SALAAM-Waziri wa Kilimo,Mheshimiwa Hussein Bashe amesema sio kweli kwamba zao la Vanilla linauzwa kwa kilo shilingi milioni 1.5.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus akizungumza na viongozi pamoja na wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari kuhusiana na Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF-Afrika Food Systems Summit 2023), Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 03 Septemba, 2023.Mkutano huo wa Mifumo ya Chakula Afrika unatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 05 -8 Septemba 2023.

Mheshimiwa Waziri amesema taarifa hizo ni za uongo huku akiwataka waandishi wa habari kuisaidia Serikali kufikisha taarifa sahihi kwa wakulima kuhusu bei za mazao na taarifa nyingine za kilimo.

Ameyasema hayo Septemba 3, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akiongea na viongozi pamoja na wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini kuhusiana na Tanzania kuwa Mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF-Afrika Food Systems Summit 2023).

Ni mkutano wa aina yake ambao unaotarajiwa kufanyika Septemba 5 hadi 8,2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam.

“Nitaanza na swali la mwandishi aliyeuliza je? Vanilla inauzwa shilingi milioni 1.5 ni uongo, nimesikia iliandikwa gazeti la Mwananchi ni vizuri kutochukua taarifa ambazo hazina uthibitisho.

"Kwa kuwa ninyi ni waandishi ni vizuri vyombo vya habari mkalipia ada kidogo kujiunga kwenye International Commodity Platform Prices ambazo zinawasaidia kuona bei za bidhaa duniani kote.

"Lakini zipo platform kama Business Insiders ukiingia unaweza kuona bei halisi ya bidhaa fulani duniani kwa wakati fulani.

“Tanzania tunazalisha Vanilla kwa kiwango kidogo, mikoa kama ya Kagera na Kilimanjaro na vanilla ni zao ambalo soko lake ni kama pareto.

"Pareto sisi Tanzania ni wazalishaji wa pili duniani, lakini tunazalisha tani 2,000 hadi 3,000 anayeongoza duniani anazalisha tani 8,000.

“Kwa hiyo, Vanilla zipo nchi zimeshapiga hatua sana duniani zinazofanya vizuri kwenye zao hili, Vanilla ilipanda bei hapa miaka miwili mitatu baada ya nchi kama Madagascar zilipokumbwa na vimbunga kwa sababu wao ni wazalishaji wakubwa.

"Na sisi ikasaidia wakulima wetu kupata bei nzuri, kwa hiyo bei ya shilingi milioni 1.5 haipo duniani, bei ya 500,000 haipo duniani.”

Kuhusu bei ya zao la pamba ambayo yenyewe inatokana na bei ya soko la dunia, Waziri Bashe amesema, "Niwaambie wanasiasa chakula sio siasa , ni maisha ya watu, ni uchumi wa watu, ngoja nitaje bei ya pamba kuanzia mwaka 2012 kilo ya pamba ilikuwa sh.660 mwaka uliofuata ikawa sh.700, sh.750, sh.1000, sh.1200, sh.1100 na mwaka 2020 bei ikawa sh. 850 kwa kilo moja.

"Mwaka jana 2022 bei ya kilo moja ya pamba ilikuwa sh.2000 na sasa ni sh.1060.Sasa ni ipi ya bei nchi zinazotuzunguka, tukianza na nchi ya Zambia bei ya kilo ya pamba ni sh.780 mpaka sh. 800.

"Kenya sh.900 na Burundi sh.700 wakati wastani wa bei ya pamba duniani, wastani wa bei ya dunia kwa leo ni senti 78 mpaka senti 88 au senti 89. Hii ndio bei ya pamba katika soko la dunia,"amefafanua Mheshimiwa Bashe.

Ameendelea kufafanua kuwa, "Mtu anasema makao ya Bodi ya Pamba yako Dar es Salaam kwa sababu kuna jengo la Pamba House.Nchi ambazo zinatuzunguka kama Zambia wanauza pamba sh.780 lakini wananunua mbolea na mbegu wenyewe.

"Mkulima wa Tanzania anapewa ruzuku ya mbegu na mbolea, hivyo akichukua fedha yake anaweka mfukoni yote.Hivyo pamoja na hayo Serikali inachukua hatua ya kubadilisha uzalishaji wa pamba ili uwe wenye tija, " amesema.

Pia amezungumzia kuchelewa kulipwa kwa wakulima wa zao la tumbaku ambapo amesema, kiasi ambacho kimelipwa ni dola za Marekani milioni 200 na ambazo hazijalipwa ni dola milioni 40.

Amesema, kutokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali katika zao hilo uzalishaji umeongezeka kutoka tani 60 mpaka tani 120, 000 lakini na bei nayo imepanda.

Wakati huo huo,Mheshimiwa Bashe amesema yapo mazao ikiwemo mchele, maharage na mahindi ambayo Tanzania ikiamua kutoyauza nje nchi nyingi zitapiga kelele na hii ni kutokana na kuwa Tanzania ina mchango mkubwa kwenye uzalishaji wa mazao hayo kwa wingi.

“Kuna swali limeulizwa sisi Tanzania ni bidhaa gani tunajivunia na kwamba tukiamua kwamba tusiuze, nchi nyingine zitakwama?.

"Ninyi ni wanahabari, sisi tukisema leo haturuhusu kupeleka mahindi yetu nje nchi zote zilizopo Jumuiya ya Afrika Mashariki na baadhi ya nchi zinazotuzunguka zitapiga kelele.

“Tukizuia kuuza nje mchele nchi nyingi za Afrika ambazo zinanunua mchele Tanzania zitapiga kelele, tukisema tunazuia kuuza nje maharage kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na Nchi nyingi zilizopo ukanda wa SADC ukiitoa Afrika Kusini Watu wa Wizara ya Mambo ya Nje watapata shida sana”

“Kwa hiyo yapo mazao ambayo tukisema hatuuzi itakuwa ni ishu, yapo mazao kama nchi tunafanya vizuri na ndio malengo ya Serikali.

"Sisi sasa hivi kama Serikali na ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais tunaondoa ile dhana inayoitwa mazao ya chakula na biashara, mazao yote ya kilimo ni ya biashara,mkulima anapoenda kulima mpunga sio tu kwa ajili ya kula na familia yake ni biashara yake pia.”

Washiriki

Katika hatua nyingine,watu 3,000 kutoka nchi 70 duniani wanarajiwa kushiriki katika mkutano huo wa siku nne wa Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF).

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus amesema, mkutano huo unafanyika kutokana na jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuomba ufanyike nchini Tanzania.

Amesema, mkutano huo utakutanisha watu wa kada mbalimbali kama viongozi wa nchi, watu maarufu, vijana, watalaam wa kilimo, watunga sera, wafanyabiashara, wawekezaji, wakulima, wafugaji na wavuvi kutoka kila kona ya dunia.

Pia, amesema hadi sasa zaidi ya watu 3,000 kutoka nchi 70 wamethibitisha kushiriki, hivyo ni matumaini ya Serikali kuwa mkutano huo utakuwa na matokeo chanya.

“Desemba 12, 2022 Rais Samia alihudhuria mkutano wa AGRF ambao ulifanyika nchini Senegali, ambapo alitumia nafasi hiyo kuomba Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa mwaka huu na tulikubaliwa kutokana na jitihada za Serikali kutenga bajeti kubwa katika sekta ya kilimo,”amesema.

Amesema, mkutano huo utawezesha wahusika kujadili kwa kina namna ya kusimamia mifumo ya chakula Afrika na duniani kwa ujumla, hiyo ikitokana na ukweli kuwa chakula ni muhimu kwa kila kiumbe.

Mkurugenzi huyo amesema kupitia mkutano huo Tanzania itaweza kutangaza fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya kilimo, uvuvi, mifugo na utalii ambazo zina mchango mkubwa katika pato la taifa.

Amesema, taarifa za sasa zinaonesha Tanzania ina ng’ombe zaidi ya milioni 36.6, mbuzi milioni 26, kondoo 6.1, kuku milioni 97.4 na samaki katika Ziwa Victoria inadaiwa kuna akiba zaidi ya tani milioni 2.23.

“Pia jukwaa hili la kimataifa litatoa fursa za kujadiliana kwenye eneo la uchumi wa buluu, kilimo cha mwani na mengine ambayo yana mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi,”amesema.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samwel Shelukindo amesema, mkutano huo unatarajiwa kushirikisha marais saba, mawaziri wakuu na wawakilishi wa nchi zote 70.

Balozi huyo amesema mkutano huo utachangia ukuaji wa uchumi, kutokana na shughuli ambazo zitafanyika kwa siku hizo.

Amesema, idadi ya washiriki wataweza kutumia bidhaa za Tanzania kama vyakula, maji, vinywaji na malazi, hali ambayo itawezesha nchi kuingiza fedha za kigeni.

Balozi Shelukindo amesema Rais Dkt.Samia aliagiza wizara hiyo na nyingine kuhakikisha Tanzania inakuza utalii wa mikutano na AGRF ni mwendelezo wa mkutano wa Rasilimali Watu ambao ulifanyika mwezi Julai, mwaka huu JNICC.

Mbali na hayo, Katibu huyo amesema, mwezi ujao mawaziri wa miundombinu kutoka nchi za Afrika wanatarajiwa kukutana jijini Zanzibar, hivyo ni ushahidi tosha kuwa nchi imefunguka kiuchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news