GEITA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeanza zoezi la ununuzi wa dhahabu kwa lengo la kuchangia maendeleo ya sekta ya madini nchini pamoja na kuongeza akiba ya fedha za kigeni.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, akipewa maelezo na mtaalamu wa mitambo ya kusafisha dhahabu wa kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Geita (Geita Gold Refinery), alipofanya ziara kiwandani hapo kujionea uendeshwaji wa shughuli mbalimbali.
Akizungumza baada ya ziara katika kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Geita (Geita Gold Refinery) na kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza (Mwanza Precious Metals Refinery Co. Ltd), Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, amesema kuwa tayari BoT imenunua na kusafisha dhahabu yenye uzito wa kilo 418.
“Kama alivyoeleza Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba kwenye bajeti, serikali imetenga fedha kwa ajili ya kununua dhahabu na mwaka huu tumepanga kununua tani sita ya dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo, wakati na wakubwa," alisema.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, akijadiliana jambo na wataalamu wa kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Geita, alipofanya ziara kiwandani hapo kujionea uendeshwaji wa shughuli mbalimbali.
Gavana Tutuba aliongeza kuwa kupitia Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Ajili ya Mauzo ya Bidhaa za Nje ya Nchi (Export Credit Guarantee Scheme), BoT imetenga pesa kwa ajili ya kuongeza mauzo nje pamoja na kuboresha bidhaa zinazoagizwa nje ya nchi ziweze kuzalishwa na kuuzwa ndani ya nchi.
“Tumefanya majadiliano ili tuangalie namna tunavyoweza kuwasaidia wachimbaji wadogo ili wapate fedha, wachimbe na kuuza kwenye viwanda vya kusafisha dhahabu ili itakapo chujwa iweze kuuzwa kwa Benki Kuu,” alisema.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, akipewa maelezo na mmiliki wa kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Geita, Bi. Sarah Masasi, alipofanya ziara kiwandani hapo kujionea uendeshwaji wa shughuli mbalimbali.
Vilevile, Gavana Tutuba amewaasa wauzaji wakubwa wa dhahabu kuzingatia sheria ya fedha za kigeni ambayo i inawataka kuleta nchini fedha za kigeni zinazopatikana katika mauzo ya dhahabu ndani ya siku 90 ili ziweze kusaidia ukuaji wa uchumi wetu.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, akifafanua jambo wakati wa ziara katika kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza (Mwanza Precious Metals Refinery Co. Ltd) ambapo alijionea uendeshwaji wa shughuli mbalimbali.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwasse, ameishukuru Serikali kwa kuwezesha ujenzi wa viwanda vya kusafisha dhahabu nchini ambapo kupitia viwanda hivyo, Benki Kuu ya Tanzania itaweza kununua na kuhifadhi dhahabu na kuongeza akiba ya fedha za kigeni ili kuimairisha uchumi wa taifa kwa ujumla.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, akifurahia jambo na viongozi mbalimbali alioongozana nao kwenye ziara katika kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza (Mwanza Precious Metals Refinery Co. Ltd).
“STAMICO tutashirikiana na Benki Kuu kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogo wanapata udhamini wa mikopo kwa ajili ya kuwawezesha kuchimba dhahabu zaidi na kuileta katika kiwanda chetu cha kusafisha dhahabu cha Mwanza ili Benki Kuu ipate dhahabu zaidi kwa ajili ya kutunza kwenye hifadhi yetu, alisema.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, akitazama dhahabu iliyosafishwa katika kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza (Mwanza Precious Metals Refinery Co. Ltd) alipofanya ziara kiwandani hapo kujionea uendeshwaji wa shughuli mbalimbali.
Benki Kuu ya Tanzania inashiriki katika Maonesho ya Sita ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Bombambili vilivyopo Mkoani Geita kuanzia tarehe 20 hadi 30 Septemba, 2023. Maonesho haya ni fursa adhimu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Benki Kuu na sekta ya madini nchini.