NA MATHIAS CANAL
MASHINDANO ya mpira wa miguu yaliyopewa jina la "CHEREHANI CUP 2023" yameanza kurindima katika Wilaya ya Ushetu mkoani Shinyanga.
Mashindano hayo yatakayohusisha timu 20 kutoka kata 20 za halmashauri hiyo yanatarajiwa kufanyika kwa wiki tatu kuanzia leo tarehe 24 Septemba 2023.
Akitoa maelezo ya awali wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Dkt.Emmanuel Cherehani amesema kuwa, mashindano hayo yatakuwa na lengo mahususi ambalo ni kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 inayobainisha umuhimu wa michezo.
Pia malengo mengine ni kuimarisha afya kwa vijana,kusaka vipaji na kuviendeleza kwa kuunda timu ya halmashauri itakayoshiriki katika ligi mbalimbali ndani na nje ya Wilaya ya Kahama.
Ili kufanikisha mashindano hayo, Mbunge Cherehani amegawa jezi jozi moja na mpira mmoja kwa kila timu.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika uzinduzi wa Mashindano hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe.Mboni Mhita amempongeza Mbunge Cherehani kwa kuanzisha mashindano hayo kwani yatawaweka pamoja vijana wengi, kuimarisha urafiki, na kuinua vipaji kwa vijana.
Amesema kuwa, jambo hilo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa vitendo, kwani mashindano hayo yatatoa fursa ya Serikali kueleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Amesema kuwa, Serikali inafanya kazi kubwa ikiwemo uimarishaji wa miradi ya maji, miundombinu, elimu, afya na uwekezaji.