NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imewataka wateja wote wa huduma za bima nchini kupitia kampuni mbalimbali pale ambapo hawaridhishwi na mchakato wa malipo ya bima zao baada ya kufikisha malalamiko kwa kampuni husika, wayawasilishe kwa mamlaka kwa hatua zaidi.
Kuhusu bima
Huu ni mpango unaotoa fidia endapo janga litatokea kwa mkatabima,fidia hiyo hutolewa kutoka kwenye michango ya wakatabima wanaounda umoja wa kukabiliana na majanga.
Aidha, mpango huu ni mkataba wa kisheria unaohusisha pande mbili kwa maana ya mkusanyaji michango ambaye ni kampuni ya bima na mkatabima ambaye huchangia ada iliyokubalika.
Rai hiyo imetolewa Septemba 18, 2023 jijini Dar es Salaam na Kamishna wa TIRA, Dkt.Baghayo Saqware katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Amesema,mamlaka hiyo ina wajibu wa kuendelea kuzisimamia kampuni za bima kuhakikisha zinalipa madai na fidia stahiki kwa wakati na kwa haki.
"Sera yetu ipo hivi,kampuni yoyote ya bima inayolalamikiwa, hilo ni kosa namba moja, na hapo ndio tunaanza kumfuatilia, tunaweza hata kumnyang’anya leseni ya kutoa huduma. Tuko imara kusimamia hilo,"amesema Dkt. Saqware.
Amesema, hadi sasa ulipaji wa madai na fidia stahiki kwa wateja wa bima yamefikia asilimia 95, hivyo kupungua kwa
malalamiko.
"Hata hivyo asilimia tano ya madai na fidia yana changamoto ambazo TIRA inafuatilia na kutoa suluhisho.Kwa mfano, ulipaji wa madai ya bima za kawaida uliongezeka kwa asilimia 10.1 kutoka shilingi bilioni 301.9 mwaka 2021 hadi shilingi bilioni 332.09 mwaka 2022."
Pia, amesema malipo ya madai na mafao ya bima za maisha yaliongezeka kwa asilimia 29.3 kutoka bilioni 95.7 mwaka 2021 hadi bilioni 123.71 mwaka 2022.
"Jumla ya kiasi cha madai kilicholipwa mwaka 2022 ni shilingi bilioni 455.80 hivyo, kupunguza umaskini kwa wanufaika na kufanya biashara kuwa endelevu,"amesema Kamishna Dkt.Saqware.
Dkt.Saqware anatumia nafasi hiyo kutoa rai kwa Watanzania kuendelea kutumia bima ikizingatiwa kwa sasa ni asilimia 18 tu nchini wanaotumia huduma hiyo.
"Nawasihi taasisi na watu binafsi kutumia huduma ya bima ili kujiondolea umaskini, unaoweza kutokana na mtu akikosa bima,"amesisitiza Dkt.Saqware.
Aidha, amesema mamlaka hiyo inaendelea na uendeshaji wa mikutano ya kupokea na kusikiliza malalamiko ya bima kwa wananchi ambapo hivi karibuni mamlaka imefanikiwa kuandaa mikutano mitano katika kanda zote za mamlaka.
Dkt.Saqware amesema, mamlaka kwa kushirikiana na Bodi ya Taifa ya Bima itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwenye Sekta ya Bima kwa ajili ya kuendeleza na kusimamia soko la bima kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Pia, amesema mamlaka inapenda kuona soko la bima lisilokuwa na udanganyifu, lenye ushindani, soko linalofuata weledi na soko lenye kuleta faida.
Ukuaji
Kwa kipindi cha miaka mitano, Dkt.Saqware amesema, sekta ya bima imekuwa kwa wastani wa asilimia 12.8 kwa mwaka huku mauzo ghafi ya yakiongezeka kutoka shilingi bilioni 691.9 mwaka 2018 hadi kufikia trilioni 1.2 mwaka 2022.
Amesema, mchango wa Sekta ya Bima kwenye pato la Taifa unazidi kuongezeka kutoka asilimia 0.56 kwa mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 1.68 kwa mwaka 2021.
Aidha,amesema TIRA imeendelea kuongeza gawio serikalini ambapo kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Juni 2023 imeweza kulipa gawio kwa serikali la shilingi bilioni 2.9.
Dkt.Saqware amesema sekta ya bima imechangia kwenye ajira kwa vijana ambapo hadi Septemba 2022 imetoa ajira za kudumu kwa Watanzania 4, 173.
Vile vile amesema, Sekta ya Bima nchini imepitia hatua mbalimbali ambapo kabla na baada ya Uhuru, mwaka 1961 licha ya sekta hiyo kupiga hatua, kuna hatua kadhaa zilichukuliwa ili kudhibiti utoroshaji wa fedha kwenda nje ya nchi miaka ya nyuma.
Dkt.Saqware anasema,katika kuwezesha maendeleo ya sekta ndogo ya bima, mwaka 2009, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilifuta Sheria ya Bima namba 18 ya mwaka 1996 na kutunga Sheria ya Bima Sura ya 394 ikiwa na majukumu kadhaa ikiwemo kusajili na kutoa leseni kwa watoa huduma za bima.
“Kuandaa na kutoa kanuni na miongozo mbalimbali ya kusimamia soko la Bima na kurekebisha sheria, kutoa elimu ya bima kwa umma, kulinda haki za mteja wa bima, kushauri Serikali kuhusu mambo ya bima."
Muundo
Dkt.Saqware amesema, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima ni taasisi ya Muungano chini ya Wizara ya Fedha na inaongozwa na Kamishna wa Bima akisaidiwa na Naibu Kamishna na inasimamiwa na Bodi ya Taifa ya Bima inayoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi.
Amesema,Muundo wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) uliidhinishwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 11 Septemba 2021.
Kamishna huyo amesema, muundo ulioidhinishwa unajumuisha Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima (TIO), Kurugenzi tatu, Ofisi ya Zanzibar, Ofisi za Kanda na vitengo saba.
“Sisi katika katika kutekeleza majukumu yetu na kusogeza huduma kwa wananchi tuna ofisi makao makuu Dodoma, Zanzibar, Dar es Salaam.”
Pia, amesema wana ofisi za kanda mkoani Tabora ambayo inahudumia Mkoa wa Tabora, Katavi na Kigoma.
Kwa upande wa ofisi ya Kanda ya Mashariki iliyopo Dar es Salaam amesema, inahudumia mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.
Dkt.Saqware amesema, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, ofisi ipo mkoani Mbeya ambayo inahudumia mikoa ya Mbeya, Njombe, Rukwa, Iringa na Songwe.
Aidha, Kanda ya Ziwa ofisi ya TIRA ipo jijini Mwanza ikiwa inahdumia mikoa ya Mwanza,Mara, Shinyanga, Kagera, Simiyu na Geita.
Kanda ya Kaskazini, Dkt.Saqware amesema, ofisi ipo mkoani Arusha ikiwa inahudumia mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga.
Vile vile, Kanda ya Kati ofisi ipo mkoani Dodoma ikihudumia mikoa ya Dodoma, Manyara na Singida. Kwa upande wa Kanda ya Kusini ofisi ipo mkoani Lindi ikihudumia mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.
Amesema,mamlaka imefanikiwa kusajili watoa huduma 1361 hadi Septemba 2023 ikiwa ni ongezeko la asilimia 12 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Miongozo
Dkt.Saqware amesema, kati ya mwaka 2022 na 2023 mamlaka kwa kushirikiana na wadau wa bima wamefanikiwa kuandaa miongozo mbalimbali kwa ajili ya kusimamia na kuendeleza soko la bima.
Miongozo hiyo ni pamoja na Mwongozo wa Usimamizi wa Ubakizaji wa Bima na Bima Mtawanyo,Mwongozo wa Bima ya Afya na usajili wa Watoa Huduma za Afya na Mwongozo wa Utoaji wa Ithibati kwa Warekebishaji na Watengenezaji wa Vyombo vya Moto katika Sekta ya Bima.
Pia, amesema miongozo mingine ni Mwongozo wa Uendeshaji huduma za Takaful,Mwongozo wa Utoaji Huduma za Bima Kidijitali,Mwongozo wa Maafisa Wauza Bima, Mwongozo wa Utekelezaji wa viwango vya kimataifa vya taarifa ya kifedha kuhusu mikataba ya Bima (IFRS 17).
Vile vile kuna Mwongozo wa Uwekezaji na Usimamizi wa Ukwasi,Mwongozo wa Kushughulikia Madai ya Bima,
Mwongozo wa Uendeshaji wa Biasharaya Benkiwakala na Mwongozo wa Viwango Elekezi vya Fidia ya Bima kwa Madai ya Majeraha ya Mwili na Vifo kwa mtu wa tatu kutokana na ajali.
Elimu
Dkt.Saqware amefafanua kuwa, mamlaka hiyo inaendelea na mkakati wake wa utoaji wa elimu kwa umma kwa kushirikisha wadau wote kwenye sekta. Lengo ni kufikia asilimia 80 ya Watanzania wote wenye umri wa miaka zaidi ya 18 ifikapo mwaka 2030.
Mbali na hayo, amesema mamlaka inaendelea na utekelezaji wa mkakati wa utoaji elimu na uhamasishaji kwa wizara na taasisi za umma kutekeleza Sheria ya Bima Sura Na. 394 ya mwaka 2009 na Sheria ya Manunuzi Na. 7 ya mwaka 2011.
Amesema, lengo mkakati ni utoaji elimu ya bima na uhamasishaji wa Serikali, Idara, Taasisi za Umma ili ziweze kuzingatia Sheria ya Bima Sura 394, kif.133 (1) hadi (3), kif.140 na Sheria ya Umma Na. 7 ya mwaka 2011, kif. 4 (2) (b).
Dkt.Saqware amesena,hadi Julai 2023,mamlaka hiyo imezitembelea Wizara ya Kilimo, Wizara ya Nishati na Wizara ya Uchukuzi na Ujenzi na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI).
Amesema, mamlaka imeendelea kuishauri Serikali katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na eneo la ukatiaji wa bima za lazima, ukatiaji wa bima kwa mali za serikali,bima ya afya kwa wote na nyinginezo.
Mafanikio
Dkt.Saqware amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2022/2023 mamlaka imepata mafanikio kadhaa ikiwa ni pamoja na uanzishaji wa Konsotia ya Bima ya Kilimo.
Amesema, uanzishwaji huo ni njia ya kutekeleza skimu ya bima ya Kilimo Tanzania kwa ufanisi ambapo Julai Mosi, 2023 ilizinduliwa Konsotia ya Bima ya Kilimo (Agriculture Insurance Consortium).
Kamishna huyo amesema, uzinduzi huo ulifanyika mkoani Tabora ambapo ulifanywa na Waziri wa Kilimo,Mheshimiwa Hussein Bashe katika kilele cha Siku ya Ushirika Duniani.
Amesema, Konsotia ya Bima ya Kilimo imeanzishwa ili kuweka ufanisi katika utekelezaji wa Skimu ya Taifa ya Bima ya Kilimo (TAIS) na kuongeza uwezo wa kimtaji wa soko la bima nchini kwa ajili ya kukinga majanga kwenye sekta ya kilimo.
Pia, Dkt.Saqware amesema kuwa,Konsotia ya Bima ya Mafuta na Gesi Tanzania imeanzishwa ambapo ilizinduliwa Novemba 16, 2022 jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, Hamad Chande.
“Vihatarishi vyote vya nishati vinavyotoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama vile vihatarishi kutoka kwa mradi wa LNG vitakatiwa bima kupitia Konsotia ya bima ya nishati ya mafuta na gesi Tanzania
“Mantiki ya kuanzisha konsotia ni kuhakikisha miradi yote ya gesi na mafuta inabakiza sio chini ya asilimia 45 ya ada zitokanazo na gesi na mafuta.
"Kutokana na kutokuwa na uwezo wa soko la ndani,vihatarishi vya nishati vilielekezwa nje ya nchi kwa asilimia 100, jambo ambalo sio na lisilo na tija kwenye uchumi wa nchi."
Amesema, kuanzishwa kwa miradi mikubwa ya nishati kama vile Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ni fursa kwenye sekta ya bima kujipanga kwa ajili ya kuongeza tija, uchumi na ajira nchini.
“Malengo ya kuanzisha konsotia ni kutoa fursa kampuni za bima za ndani kushiriki na kuandika vihatarishi vya nishati ya gesi na mafuta ndani ya nchi, kushiriki katika bima ya mradi wa LNG unaokadiriwa kuwa na gharama ya uwekezaji wa dola za Kimarekani bilioni 40,"amefafanua Dkt.Saqware.
Kamishna huyo amesema,kampuni 22 za bima zimesaini mkataba wa muungano wa Bima ya Nishati ya Mafuta na Gesi Tanzania zenye jumla ya laini (hisa) 238.
Amesema, kila hisa ina thamani ya dola za Kimarekani 25,000 ambayo ni jumla ya uwezo wa muungano wa kiasi cha mtaji cha wa dola za Marekani milioni sita.
Dkt.Saqware amesema, konsotia itasimamiwa na kampuni ya bima mtawanyo ya Tanzania Reinsurance Company Limited (Tan Re).
Pia, Kampuni ya Bima ya Phoenix ya Tanzania ndiyo kiongozi wa konsotia huku Kamati ya Kiufundi ya Konsotia imeundwa na wanachama kutoka kampuni 10 za bima.
Miongoni mwa kampuni hizo ni Shirika la Bima la Taifa (NIC),Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC),Phoenix, Jubilee, Britam, Heritage, Reliance, UAP, Tanzania na Alliance Insurance Corporation.
"Wajumbe wa kamati wana idadi ya laini kuanzia tano mpaka 95 katika muungano wao,faida za moja kwa moja za konsotia kwa nchi yetu ni pamoja na kuhakikisha miradi yote ya gesi na mafuta inabakiza sio chini ya asilimia 45 ya ada zitokanazo na gesi na mafuta,”amesema Kamishna huyo.
Dkt.Saqware akizungumzia mipango ijayo ya mamlaka hiyo amesema, mamlaka hiyo kwa kushirikiana na wadau wa bima inaendelea na utekelezaji wa mipango na mikakati ya Taifa ambayo ni pamoja na Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa (FYDPII-2020-2025).
Nyingine ni Mpango Mkuu wa Taifa wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Nchini (FSDMP 2020-2030), Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (2020-2025), Sera ya Uchumi wa Buluu Zanzibar.
Sambamba na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan wakati akilihutubia Bunge mwezi April 2021 ikiwemo kupokea na kufanyia kazi maelekezo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi.
Miradi
Dkt.Saqware amesema, mamlaka hiyo, ina mradi wa TIRAMIS na TIRA-ORS TIRAMIS (TIRA Management Information System) na TIRA-ORS (TIRA Online Registration System).
“Mamlaka, kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2019/2020 hadi 2021/2022, imetekeleza miradi miwili ya Mifumo ya TEHAMA (TIRAMIS na TIRA-ORS).
"Mifumo hii yote imejengwa na watumishi wa umma. Mifumo yote miwili inafanya kazi na imesaidia kuleta manufaa kadhaa kwenye soko ikiwa ni pamoja na kurahisisha huduma za utumaji na upokeaji wa taarifa za kibima miongoni mwa wadau.
“Kurahisisha usimamizi wa biashara ya bima nchini, kuharakisha uchambuzi wa takwimu na utaoji wa taarifa,” amesema Dkt.Saqware.
Mbali na hayo wameendelea kuunganisha mifumo ya kidigitali na taasisi mbalimbali za umma ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA),
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA),Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC),Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA).
Dkt.Saqware amesema, lengo ni kuongeza usimamizi na maendeleo ya soko la bima na kuendelea na utoaji wa elimu ya bima kwa umma na wadau mbalimbali nchini.
“Kwa mfano mamlaka imeandaa Semina ya Pili ya Makatibu Wakuu wote nchini kwa lengo la kutoa elimu ya umuhimu wa ukataji bima. Semina imepangwa kufanyika Oktoba 27, 2023,”amesema Kamishna huyo.
Pamoja na hayo, amesema mamlaka hiyo itafungua ofisi za bima mtawanyo za kikanda ambazo Serikali ya Tanzania inamiliki hisa za moja kwa moja au kupitia taasisi zake ili kampuni hizo ziweze kufungua ofisi nchini kwa utaratibu wa mikataba ya uenyeji ili kuwa na soko la bima lisilokuwa na udanganyifu.
Hata hivyo, Kamishna Dkt.Saqware amesema, Sekta ya Bima itakuwa kinara katika ukuaji na uendelezaji wa sekta ya fedha nchini.
Naibu Kamishna
Wakati huo huo, Naibu Kamishna wa Bima, Khadija Said amesema,katika mkakati wa kutoa elimu nchini, mamlaka hiyo imewatafuta mabalozi ambao watakuwa wanasaidia kutoa elimu nchini.
"Mabalozi hao wapo watatu, wawili ni kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mmoja kwa upande wa Serikali.
"Kwa hawa wabunge watatusaidia kwa upande wa Bunge na jamii, kwa sababu wabunge wapo upande wa jamii sana, kwa hiyo wanapokuwa majimboni huko wanaweza vile vile kutoa elimu kwa wananchi kuhusu bima, kwa hiyo ninaamini watatusaidia."
Mabalozi wa Bima ni Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Mhandisi Zena Said, Mheshimiwa Japhet Hasunga na Wanu Ameir ambao ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, mabalozi hao walioteuliwa Februari 2023 huku majukumu yao yakiwa ni kutoa ushauri kwa mamlaka na sekta ya bima kwa ujumla kuhusu maendeleo ya sekta ya bima.
Sambamba na kutoa elimu kwa umma juu ya masuala ya bima katika ngazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi na makatibu wakuu kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar.
TEF
Katika kikao kazi hicho, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF),Deodatius Balile aliipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kuratibu vikao kazi hivyo ambavyo vimesaidia kuongeza uelewa kuhusu mashirika na taasisi hizo za umma.
Wakati huo huo, licha ya kuipongeza TIRA kwa kazi nzuri hususani usimamizi wa watoa huduma za bima ambao wamewezesha huduma kuwafikia wananchi wengi nchini, pia alishauri.
Balile alisema, pengine ni wakati wa mamlaka hiyo kuangalia namna ambavyo itaingiza mikopo maarufu ya 'Kausha Damu' mitaani iweze kuingia katika mfumo wa bima ili kukabiliana na changamoto ambazo zinaikabili mikopo hiyo ingawa si rasmi.
"Kuna mikopo maarufu sana kama Kausha Damu mitaani, tunafanyaje ili kuausha damu kukatiwa bima ili vyombo viache kuchukuliwa kutoka nyumbani, kwa wale wanaodaiwa."
Pia, alisema TIRA imesaidia kwa kiwango kikubwa, kwani usimamizi wao umewezesha kupunguza changamoto mbalimbali za waendesha vyombo vya moto ambao awali walikuwa wanakutana nazo barabara kupitia maafisa wa usalama barabarani.