GERSON PARTINUS MSIGWA: HONGERA SANA MSIGWA

NA LWAGA MWAMBANDE

“Chochote tunachokifanya tutangulize maslahi ya Taifa, upendo, amani, haki, mshikamano na tuchape kazi kwa juhudi na maarifa. Tutakula kwa jasho letu;

Hii ni kati ya nukuu ambayo huwa anapenda kuisisitiza aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali,Gerson Partinus Msigwa.

Aprili 4,2021 ndugu Msigwa aliteuliwa kushika wadhifa huo na Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kabla ya uteuzi huo,Msigwa alikuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu ambako amehudumu kwa miaka mitano na nusu baada ya kuteuliwa na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu akitokea katika wadhifa wa Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi (Ikulu) alioteuliwa Novemba, 2014 na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Kabla ya kuteuliwa katika nyadhifa hizo, alikuwa Mwandishi wa Habari Mwandamizi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kituo cha Songea mkoani Ruvuma ambako aliripoti kwa umahiri matukio mbalimbali na kuandaa makala za kuutangaza Mkoa wa Ruvuma.

Juhudi na maarifa katika kazi zake zilimwezesha kuiwakilisha TBC katika majukumu makubwa yakiwemo ya kuripoti ziara za viongozi wakuu wa nchi akiwemo Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, kuripoti matukio makubwa ya Kitaifa na Kimataifa yakiwemo Uchaguzi Mkuu, Mikutano ya Umoja wa Mataifa, ziara za Rais nje ya nchi, ziara za Marais wa nchi mbalimbali waliotembelea Tanzania na Mikutano ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Bunge la Katiba.

Mwaka 2014 baada ya kuhamishiwa Ikulu, Dar es Salaam akiwa Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi, Ndugu Msigwa alitoa mchango mkubwa katika kutangaza kazi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne kupitia Makala Maalum ya Ikulu iliyoitwa “Makala ya Rais”.

Makala hii pamoja na mambo mengine ilisaidia uelewa wa wananchi kuhusu kazi zinazofanywa na Mheshimiwa Rais hasa anapokuwa nje ya nchi.

Akiwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Ndugu Msigwa aliongoza mageuzi makubwa ya Kitengo cha Mawasiliano ya Rais kwa kuanzisha kurasa rasmi za mitandao ya kijamii yaani facebook, twitter na instagram na kuboresha uwekaji wa maudhui katika chaneli ya youtube ya Ikulu Mawasiliano.

Pia aliongoza uanzishaji wa kitengo kidogo cha urushaji wa matangazo Mbashara ambapo Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu iliweza kuzalisha na kurusha matangazo hayo na kuvifikia vyombo vya habari vyote bila gharama.

Hatua hii pia ilisaidia kuondoa upotoshaji, ilipunguza gharama kwa vyombo vya habari, iliongeza muonekano wa Rais kwa wananchi (visibility) na kuwawezesha wananchi kupata muktadha halisi wa hotuba na matamko ya Rais.

Aidha, alianzisha uchapishaji na usambazaji wa Taarifa kwa Vyombo vya Habari (Press Release) kupitia nakala picha (screenshots) ambavyo vilisambaa kwa urahisi kupitia mitandao ya kijamii vikiwa vimewekwa saini yake. Jambo hili lilisaidia kukabiliana na upotoshaji na kuwawezesha wananchi kupata taarifa moja kwa moja.

Ndugu Msigwa pia aliongoza uanzishaji gari maalum la matangazo (OB Car) lililofungwa mitambo ya matangazo ya satelite ili kuwezesha shughuli za Rais kurushwa mbashara hata pale ambapo kuna changamoto za mtandao wa intaneti.

Halikadhalika, akiwa Ikulu aliongoza mageuzi katika uendeshaji wa shughuli za Rais hasa matukio yaliyohusisha wageni mfano Dhifa za Kitaifa, Mikutano, Ziara za Viongozi na Sherehe za Kibalozi ambapo zilihusisha burudani za Wasanii wa ndani, kutengeneza muonekano mzuri (branding) na kuhamasisha Wasanii kufanya kazi kwa karibu na Ikulu.

Akiwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndugu Msigwa aliongoza mageuzi muhimu ya idara hiyo yakiwemo kuanzisha Utoaji wa Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Serikali ya kila wiki.

Kupitia utaratibu huo, taarifa hiyo hutolewa katika mikoa mbalimbali ili kutoa nafasi kwa Waandishi wa Habari tofauti tofauti kuuliza maswali na kuruhusu wananchi kupiga simu na kuuliza maswali moja kwa moja kwa Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia simu.

Pia,Msigwa ameongoza uanzishaji wa kitengo cha urushaji wa matangazo mbashara ambapo Idara ya Habari (MAELEZO) imeweza kuzalisha na kusambaza maudhui ya shughuli za Serikali kwa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii yote nchini.

Aidha, amewezesha Idara ya Habari (MAELEZO) kupata gari la matangazo ya nje (OB Van) ambalo lina mitambo ya kurushia matangazo hayo ili kurahisisha kazi.

Vile vile, Msigwa amewezesha Idara ya Habari (MAELEZO) kujenga studio ya muda kwa ajili ya kuwezesha uzalishaji wa vipindi vya kimkakati vya Serikali ambavyo vitavifikia vyombo vyote vya habari na mitandao ya kijamii.

Aidha, Idara ya Habari (MAELEZO) imefanya uboreshaji wa muonekano wake (branding) na kujipambanua kama Idara ya Kitaifa yenye majukumu na uwezo wa kutangaza shughuli za Serikali kimkakati na kuongeza muonekano wa Serikali kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Idara ya Habari (MAELEZO) imeboresha kazi zake zikiwemo kuchapisha Jarida la Nchi Yetu la mtandaoni la kila siku, kuzalisha makala ya Juvyo na kuandaa majarida ya nakala ngumu ya Nchi Yetu.

Juhudi hizo ndiyo zimemfanya kuendelea kuaminiwa zaidi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, ambapo leo Septemba 23, 2023 ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande licha ya kumuombea kwa Mungu ndugu Msigwa aendelee kutimiza majukumu yake kwa ufanisi nchini, pia amempa hongera. Endelea;

1.Asubuhi hii njema, mazuri tumesikia,
Kiongozi wetu mwema, ngazi amejipandia,
Azidi kutenda mema, nasi tukifurahia,
Kwa Ukatibu Mkuu, hongera sana Msigwa.

2.Umefanya kazi njema, kote ulikopitia,
Umewakilisha vema, hata yetu tasnia,
Sasa mzimamzima, utendaji wakalia,
Kwa Ukatibu Mkuu, hongera sana Msigwa.

3.Rais Samia mama, jicho umetutupia,
Vile umeona vema, Msigwa kumwangalia,
Kwa saluti twasimama, hili tumefurahia,
Kwa Ukatibu Mkuu, hongera sana Msigwa.

4.Msigwa nenda salama, taifa kutumikia,
Mambo yetu yawe mema, isikike Tanzania,
Michezo ing’are vema, na utamaduni pia,
Kwa Ukatibu Mkuu, hongera sana Msigwa.

5.Umeshaacha alama, Maelezo nakwambia,
Jinsi ilivyosimama, kwa kweli inavutia,
Ya kisasa tunasema, habari yatupatia,
Kwa Ukatibu Mkuu, hongera sana Msigwa.

6.Maelezo ninasema, kazi tunafurahia,
Mwatuhabarisha vema, mara kwa mara sikia,
Mko vema kwa TEHAMA, Msigwa umechangia,
Kwa Ukatibu Mkuu, hongera sana Msigwa.

7.Wengi tutaona vema, makombe jichukulia,
Kwa uwakilishi mwema, katika yetu dunia,
Lizidi kutajwa vema, jina letu Tanzania,
Kwa Ukatibu Mkuu, hongera sana Msigwa.

8.Na Sanaa himahima, tuzidi kufurahia,
Ajira zikisimama, kipato kujipatia,
Ule wizi kazi noma, uweze kufwatilia,
Kwa Ukatibu Mkuu, hongera sana Msigwa.

9.CAF sisi twazizima, kwa soka la Tanzania,
Wanawake wanavuma, hakuna wa kuzuia,
Pia twapenda kuvuma, michezo mingine pia,
Kwa Ukatibu Mkuu, hongera sana Msigwa.

10.Kazi kaifanye vyema, tuzidi kufurahia,
Nchi izidi kuvuma, katika yetu dunia,
Sasa sote twasimama, makofi twakupigia,
Kwa Ukatibu Mkuu, hongera sana Msigwa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news