NA FRESHA KINASA
WANANCHI pamoja na wavuvi katika Kisiwa cha Rukuba kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuanza kutoa vifaa tiba vyenye thamani zaidi ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya kituo chao cha afya ambacho ujenzi wake umekamilika.
Vifaa hivyo ni pamoja na Oxygen Machine, mashine za kusaidia mtoto upumuaji na kufyonza maji hata mama akiwa amemeza maji wakati wa uzalishaji ambavyo vinalenga kuokoa maisha ya mama na watoto wanaozaliwa kituoni hapo.
Elizabeth Paul amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Hassan imeendelea kuwagusa wananchi kwa kiwango kikubwa kwa kuimarisha sekta ya afya katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizo kwa ufanisi na karibu na makazi yao jambo ambalo ni neema kwa wananchi.
"Tunamshukuru Prof.Muhongo kwa juhudi kubwa ambazo amekuwa akizifanya kuhakikisha wananchi tunapata huduma,kituo cha afya kimekamilika na tayari vifaa tiba tunaona vinakuja ili sasa tupate huduma hapa, haya ni mageuzi makubwa ya kupongeza ambayo Serikali imefanya,"amesema Jesca Amony.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Vijijini, Denis Ekwabi amesema, anamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha na kuyatazama maeneo ya visiwani yapate vituo vya afya na zahanati ili Watanzania wote wahudumiwe kwani hatua hiyo ni njema na ya kupongezwa.
Aidha, amemshukuru Mbunge Prof.Muhongo kwa uhamasishaji wake ambao amekuwa akiufanya na ushiriki wake wa moja kwa moja katika ujenzi wa miundombinu ya afya, elimu na sekta mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya wana Musoma Vijijini.
Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijni Prof. Sospeter Muhongo akizungumza na wananchi wa kisiwa hicho amesema,"kwa sababu tuna Kituo cha Afya hapa wataletwa madaktari wa upasuaji.
"Tuna vituo vya afya sita cha zamani cha Mrangi, Mugango na vituo ambavyo ni vipya ni cha Kisiwa cha Rukuba, Kiriba, Makojo, na Masinono,"amesema Prof.Muhongo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Septemba 28, 2023 imeeleza kuwa, "Kisiwa cha Rukuba kimekamilisha ujenzi wa Kituo chake cha Afya na tayari kimeanza kupokea vifaa tiba vya kituo hicho.
"Utoaji wa huduma za afya ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini unaendelea kuboreshwa na kuimarika,"imeeleza taarifa hiyo na kusema.
"Kwa sasa tuna hospitali ya halmashauri hii ina hadhi ya Hospitali ya Wilaya, vituo vya Afya sita Murangi, Mugango, Bugwema, Makojo, Kiriba na Kisiwa cha Rukuba. Zahanati 42, kati ya hizo 24 za Serikali, 4 za Binafsi na 14 zinajengwa."
Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa, "Maombi yaliyopelekwa serikalini wafanyakazi wa kutoa huduma mbalimbali za Afya wapo wachache sana. Idadi iongezeke sana.
"Tunaomba idadi iongezeke hasa kwenye hospitali yetu mpya na kwenye vituo vyote vya afya. Vifaa tiba vinahitajika, ni pungufu sana.Wingi wa dawa za aina mbalimbali uongezeke sana,"imeeleza taarifa hiyo.