Kopa kwa maendeleo, wala si kwa kutafuna

NA LWAGA MWAMBANDE.

MIONGONI mwa watumishi wa Mungu waliojijengea heshima kubwa hapa nchini, Wakili na Mtume Justine Kaleb amewahi kuandika katika Jukwaa la Sheria kupitia ukurasa wa Facebook kuwa, mkopo sio anasa.

Anasema, mkopo unaweza kukuinua, kukutajirisha na kuwa mkombozi wako, kama utazingatia mambo ya msingi kisheria na kibiashara kabla ya kukopa.

Wakili huyo, anasema mkopo ni makubaliano ya kupeana fedha au vitu kwa lengo la kurudisha fedha/vitu hivyo baada ya muda fulani, kama zilivyo au zikiwa na ziada au riba.

Makubaliano hayo ya mkopo yaweza kufanyika kwa kuhusisha dhamana ya mkopo huo au pasipo dhamana kutegemeana na namna wahusika wenyewe walivyokubaliana.

Aidha, Wakili Kaleb anasema kuwa, makubaliano hayo pia yaweza kuwa ya mdomo au ya maandishi kutegemeana na namna wahusika walivyoona katika kuingia makubaliano hayo.

Mkopo ni moja kati ya nyenzo kubwa sana zinazoweza kutumiwa na mfanyabiashara au mtu mwingine yeyote yule, katika kupata pesa zinazoweza kuendesha biashara yake.

Anasisitiza kuwa, mkopo ukitumiwa vizuri husaidia kuongeza mtaji wa biashara, kukuza wigo wa biashara, kujenga mahusiano mazuri ya kifedha kati ya taasisi ya fedha na kampuni au mfanyabiashara/mjasiriamali.

Huwajengea wafanyabiashara nidhamu ya matumizi bora ya fedha na kujenga mustakabali mzuri wa biashara. Mambo ya msingi yasipozingatiwa kabla ya kukopa, mkopo huwa ni kero, balaa, mzigo, utumwa na karaha.

Pia,anasema, usipokuwa mwangalifu mkopo unaweza kuharibu jina la biashara yako, unaweza kupoteza wateja, kufilisiwa, kupoteza mwelekeo wako kibiashara, kuharibu uhusiano na taasisi za fedha.

Mkopo unaweza kuvunja ndoa, undugu, urafiki na kusambaratisha kabisa mahusiano yaliyodumu kwa muda mrefu kati ya pande mbili.

Wakili Kaleb anasema, kuna umuhimu mkubwa sana wa kuwa makini sana na kuzingatia mambo yote ya msingi kisheria na kibiashara kabla hujakopa.

Kwa mujibu wa sheria ya Mikataba Sura ya 345 kama ilivyorejewa mwaka 2002, anasema ni muhimu sana makubaliano yenu ya mkopo yakawa kwa maandishi, mali iliyokopeshwa ijulikane wazi na kama kuna riba na yenyewe ikawekwa bayana kwenye mkataba na muda maalumu ambayo italipwa.

Vile vile anasema, ni muhimu sana kila kitu kikajadiliwa na kuwekwa wazi kabla ya kusaini mkataba wenyewe wa mkopo.

Haki zijulikane, wajibu utambulike na nini kitatokea endapo upande mmoja utashindwa kutekleza au utavunja masharti ya mkataba.

Unapotaka kukopa usielekeze macho yako kwenye pesa au kitu utakachokopeshwa bali elekeza macho yako, ufahamu wako, akili yako na moyo wako wote kwenye wajibu wako au masharti unayopaswa kuyatimiza na nini kitatokea endapo utashindwa kuyatimiza.

Ukiweza kuchanganua kwa kina na kiunaga ubaga kuhusiana na wajibu wako ndipo uingie kuelekeza macho yako kwenye kiasi cha pesa unachokopa au bidhaa.

Kuingia mkataba wa mkopo kwa maneno ni kuhatarisha usalama wa fedha na mali zako. Ni muhimu ijulikane unadaiwa nini, riba kiasi gani, dhamana ni nini, utalipa kwa muda gani, kivipi.

Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha sura ya 342 pamoja na kanuni zake inazitaka taasisi za fedha ambazo zinakopesha kuwa na leseni na vibali vyote vya kufanya hivyo.

Ni muhimu ujiridhishe juu ya uhalali wa taasisi hiyo unayotaka kwenda kukopa ili usije ukapoteza kiholela mali zako ulizoweka dhamana.

Kwa mikopo ambayo dhamana yake huwa ni mali ya wanandoa, ni muhimu sana kumshirikisha mwenzi wako kabla ya kufanya chochote.

Usimfiche mkeo au mumeo, utakuja kuumbuka mali inapouzwa. Kama mali ni ya urithi washirikishe warithi wote, usiweke rehani mali ya urithi kimya kimya, utajuta.

Usitoe mali yako kienyeji kumdhamini mtu ili akope. Jiepushe na matapeli ambao wako tayari kukufundisha kufanya udanganyifu kwenye nyaraka ambapo unaweza ukatengenezwa nyaraka zitakazoonyesha kuwa mke au mume wako ameridhia.

Ni ili wewe kuweka dhamana mali yenu na ukaambiwa leta tu picha yake kisha picha hiyo ikawekwa kwenye nyaraka hizo na mtu mwingine badala ya mume au mke wako akasaini kuonyesha kweli ameridhia.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande licha ya kusisitiza kuwa, ukikopa na kuwa makini kwa ajili ya shughuli za maendeleo kamwe hauwezi kujutia. Endelea;


1:Mkopo wala si deni, hiyo hasa biashara,
Mtu fikira kichwani, afanye kilicho bora,
Fedha zake mfukoni, ni chache zinamkera,
Kopa kwa maendeleo, wala si kwa kutafuna.

2:Kopa lisiwe ni deni, zingatia marejesho,
Ukishindwa lawa deni, na kwako hiyo michosho,
Tafwatwa hadi nyumbani, leo wala siyo kesho,
Kopa kwa maendeleo, wala si kwa kutafuna.

3:Endapo uko makini, unalipa kwa wakati,
Huku kazi kiwandani, unazidi panda chati,
Ikishafika jioni, kwa amani unaketi,
Kopa kwa maendeleo, wala si kwa kutafuna.

4:Usiende utumwani, kukopa bila kulipa,
Utatiwa kitanzini, hadi utakapolipa,
Au na mali nyumbani, ziuzwe uweze lipa,
Kopa kwa maendeleo, wala si kwa kutafuna.

5:Utumwa wa duniani, mikopo husababisha,
Watu hawana amani, madeni yanawawasha,
Wanakimbia nyumbani, kufichama wanakesha,
Kopa kwa maendeleo, wala si kwa kutafuna.
(Mithali 22:7)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news