Kuelekea mvua za vuli, Serikali yawapa mbinu wakulima nchini

NA GODFREY NNKO

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema, utabiri wa hali ya hewa unaonesha kuwa, nchi inatarajiwa kupata mvua nyingi hususani za vuli katika msimu wa kilimo 2023/2024.

Amesema, ili kuhakikisha mvua hizo zinatumika vizuri na zinaleta tija katika uzalishaji, wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo kwa wakati ili kuongeza uzalishaji.

Pia kufuatilia kwa ukaribu taarifa za mara kwa mara kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) na kuwasiliana kwa ukaribu na kufuata ushauri wa Maafisa Ugani walioko katika maeneo yao.

Ameyasema hayo Septemba 8, 2023 wakati wa kuahirishwa Mkutano wa 12 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.

"Sote tutakumbuka kuwa tarehe 24 Agosti, 2023 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ilitoa utabiri kuhusu mwelekeo wa mvua za vuli kwa mwaka 2023.

"Utabiri huo unaonesha uwezekano wa kunyesha mvua kubwa kuanzia Oktoba, 2023 ambapo mvua hizo zitanyesha kwa kiwango cha wastani na juu ya wastani katika baadhi ya maeneo."

Waziri Mkuu amesema kuwa, maeneo yanayotarajia kuwa na mvua hizo ni pamoja na mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Mara, Simiyu na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Kigoma.

Mikoa mingine ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Dar es salaam, Pwani na Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro.

"Mheshimiwa Spika, kiwango hicho cha mvua kitawezesha uzalishaji wa kuridhisha wa mazao ya chakula. Hata hivyo, kuna uwezekano wa mvua hizo kuleta athari katika baadhi ya maeneo kama vile mafuriko yanayoweza kusababisha kutokea kwa mmomonyoko wa udongo pamoja na uharibifu wa miundombinu ya uzalishaji wa mazao."

Upatikanaji wa pembejeo

Waziri Mkuu amesema, Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa pembejeo nchini ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo.

"Sote tunafahamu kuwa tija katika uzalishaji wa mazao ya kilimo hutegemea teknolojia za kilimo, utaalam na upatikanaji wa pembejeo bora ikiwemo mbolea."

Amesema, katika msimu wa kilimo 2022/2023, matumizi ya mbolea yaliongezeka kutoka tani 363,599 hadi tani 538,000 sawa na ongezeko la asilimia 48.

Waziri Mkuu amefafanua kuwa, ongezeko hili limetokana na upatikanaji wa mbolea ya ruzuku ambayo Serikali imekuwa ikitoa kuanzia msimu wa kilimo wa 2022/2023.

"Kipekee, nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha upatikanaji wa mbolea nchini unaimarika."

Pia, amebainisha kuwa, ongezeko la matumizi ya mbolea limeenda sambamba na ongezeko la uzalishaji hususan mazao ya chakula ambapo upatikanaji wa chakula umeongezeka nchini.

"Makadirio ya mahitaji ya mbolea kwa msimu wa kilimo 2023/2024 ni tani 849,219. Hadi kufikia tarehe 31 Agosti, 2023, upatikanaji wa mbolea umefikia tani 480,662 sawa na asilimia 56.6 ya wastani wa mahitaji kwa mwaka."

Katika msimu huu wa kilimo, Waziri Mkuu amesema, Serikali itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima ili kuwapunguzia makali ya bei ya pembejeo hii muhimu katika uzalishaji.

"Hivyo, ninaielekeza Wizara ya Kilimo kusimamia kikamilifu ugawaji wa mbolea kwa wakulima kwa kuboresha mfumo wa ugawaji ikiwemo kuongeza vituo vya mauzo ya mbolea pamoja na kuvisogeza vituo hivyo karibu na wananchi."

Masoko

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema, katika kuhakikisha kuwa mazao yaliyovunwa katika msimu wa mwaka 2022/2023 yanapata soko la uhakika, bei nzuri na nchi kuwa na uhakika wa usalama wa chakula, Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imepanga kununua tani 305,000 za nafaka.

Hadi kufikia Septemba 5, 2023, Waziri Mkuu amesema, jumla ya tani 175,000 za nafaka sawa na asilimia 57 za lengo zimeshanunuliwa kupitia katika vituo 75 vilivyopo katika kanda nane za NFRA.

"Nitumie fursa hii kuielekeza Wizara ya Kilimo kupitia NFRA kuimarisha miundombinu ya uhifadhi ili kuepuka kupoteza mazao ya chakula wanayoendelea kununua."

Amesema, katika msimu 2022/2023 bei za mazao mengine ya biashara zimeendelea kuimarika hususan mazao yanayotumia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani.

Mathalan, zao la kakao linalolimwa kwa wingi Wilaya za Kyela na Mvomero bei imefikia shilingi 8,700 kwa kilo.
Kwa upande wa mbaazi, Waziri Mkuu amesema, bei imeongezeka kutoka shilingi 1,000 hadi 1,500 kwa kilo hadi shilingi 2,000 kwa mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi na shilingi 2,200 kwa Mkoa wa Manyara.

Bei ya ufuta imeongezeka na kufikia shilingi 4,000 kwa kilo ikilinganishwa na shilingi 1,000 hadi 1,200 kwa kilo msimu uliopita.

"Nitoe wito kwa wakulima nchini waendelee kutumia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwa mazao haya kwa sababu tumeanza kuona tija ya bei nzuri. Hivi karibuni tuliona video ya wananchi kutoka Nanyumbu wakicheza ngoma kushangilia kupatikana kwa bei nzuri ya zao hilo."

AGRF 2023

Waziri Mkuu amesema,Septemba 7, 2023 hapa nchini, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amehitimisha Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula barani Afrika (AGRF) lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema, kwenye kongamano hilo walijadili na kuangalia mifumo ya kilimo na namna nchi itakavyoweza kunufaika na kumudu kujiongezea uwezo wa kuwa na chakula cha kutosha na ziada.

"Jukwaa hilo lilibainisha fursa zitokanazo na kilimo na mijadala hiyo ilihusisha fursa zilizopo kwenye sekta za mifungo na uvuvi katika kutoa fursa za kiuchumi kwa ujumla."

Waziri Mkuu amesema, jukwaa hili kwetu limeleta manufaa makubwa, limekutanisha wataalamu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi na kuweza kupeana uzoefu wa namna upatikanaji wa chakula cha kutosha katika kila nchi.

"Nasi Tanzania tumejikita kwenye eneo hili katika kuhakikisha kwamba jamii yetu inapata chakula cha kutosha,"amebainisha Waziri Mkuu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news