Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Jomaary Mrisho Satura ameyasema hayo mbele ya mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo wakati wakiongeza na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo.
"Leo peke yake Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya na jana nimekutumia umeona, ni leseni feki, na risiti za malipo feki, jambo ambalo nimemuona Mheshimiwa Rais akilizungumza alipokuwa kwenye mkutano na viongozi wengine pale Kibaha.
"Sisi pia, ndugu zanguni naomba mtambue, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, wannachi hawa wafanyabiashara wa Kariakoo na Dar es Salaam kwa ujumla hawana muda wa kufuatilia mambo.
"Akili zao zinafikiria kufanya biashara tu, na wakati mwingine wanalazimika sasa kuwatuma vijana, wanampa fedha, pale halmashauri yale mambo ya kushinda kutwa kwenye foleni, shika ukafanye wewe, niache mimi niende bandarini nikashughulikie mambo mengine makubwa.
"Sasa, wale vijana kwa sababu ile fedha wanaitaka, wanaingia kwenye mifuko ya nyuma wanazunguka huku wanazunguka huku, anamletea mzee leseni anamwambia mkuu nimeshaangaika leseni hii hapa.
"Lakini tukiingia kwenye mfumo, leseni haipo, leseni imetengenezwa stationary, ninyi mnajua malipo yenu mmelipa na mnahitaji huduma, lakini zaidi ya asilimia 50 ya leseni zinazoendelea hapa mjini, Mheshimiwa Mkuu wa wilaya ni leseni feki.
"Lakini, risiti mnazopewa kwa ajili ya malipo mbalimbali nazo ni feki,kwa hiyo mnajua mnatoa fedha kwa ajili ya maendeleo ya Taifa hili, lakini fedha hizi hazifiki serikalini.
"Sasa, utashangaa mfanyabiashara wa hapa mjini anakula mchana, Mheshimiwa Mkuu wa wilaya, muhogo na kachumbari ili achangie mapato ya Serikali, lakini yule aliyepewa zile hela yuko pale DDC, yuko anakunywa bia na anakula nyama.
"Na ana-enjoy maisha kuliko mfanyabiashara mwenyewe, kwa hiyo shughuli nyingi hapa mjini Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya zinafanywa na vishoka, yaani vishoka wananeemeka kuliko wafanyabiashara, na sisi Serikali, fedha hizo hatuzipati.
"Kwenye hili eneo Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya tumesema nalo tulidhibiti, kwa nini tunaibiwa, ni vema wafanyabiashara wakafahamu, tunaibiwa kwa sababu halmashauri hatuna kanzi data.
"Mheshimiwa Mwenyekiti ana orodha ya wanachama wake,anawajua, anajua Juma Hamis amelipa, huyu amelipa, nani ambaye hajalipa, hata shule wana orodha ya watoto na wazazi, wanajua huyu amelipa huyu hajalipa.
"Huyu mtoto tumuulize, huyu tumpigie simu baba yake tumtaarifu, sisi orodha hiyo ya wafanyabisahara hatuna, hatuna naomba niseme hapa sisi jiji hatuna, sasa kama hauna kwa nini usiibiwe?.
"Lakini, jaribu kuangalia biashara zilizopo ndani ya Jiji la Dar es Salaam, ndugu zanguni mkumbuke jiji lenu linaenda mpaka Bonyokwa, linaenda mpaka Segerea, linaenda mpaka Kinyerezi, Kifuru tunaenda kukutana na Kibaha huko, tunaenda mpaka Mkuranga huko.
"Hatuna watumishi ambao wanaweza kuanzia Kivukoni jengo kwa jengo mpaka wafike Kinyerezi na maeneo mengine, wakifika kule mwisho wa mwaka utakuwa umeisha, na kwa jinsi hiyo sasa tumekuwa tukiibiwa, imeruhusu makanjanja kuja kuwasumbueni ninyi wafanyabiashara.
"Na kuwatisha na wakati mwingine kuwaeleza viwango vya kodi visivivyostahiki ili kusudi muanze kubageini naye, yaani anakutajia viwango ambavyo haustahili kulipa na siyo saizi yako, ili kusudi uanze kuomba nafuu.
"Ndani ya Jiji la Dar es Salaam Mheshimiwa Mkuu wa wilaya ndiyo eneo ambalo hata wastaafu na watu waliofukuzwa kazi bado wanaendelea kukusanya mapato.
"Hakuna anayejua huko busy, hauwezi kufahamu huyu alifukuzwa kazi, huyu kasimamishwa kazi as long as alikuwa anakuja dukani kwako miaka na miaka akifika dukani kwako unajua utaratibu ni kumpa shilingi laki moja aondoke.
"Na hili Mheshimiwa Mkuu wa wilaya ukitaka kujua watu wa Dar es Salaam hawana muda, wewe angalia asubuhi kwenye foleni watu walivyokuwa na haraka.
"Akitokea chizi akaanza kuelekeza magari yaende upande mmoja, hata wenye akili zao wote wanafuata huko, halafu wakishafika huko ndiyo wanaanza kugundua yule alikuwa akiwaelekeza ni chizi,"amefafanua Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Jomaary Mrisho Satura.
DC
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, akizungumzia hali ya udhibiti na ukusanyaji wa mapato katika Jiji la Dar es Salaam, amewataka wafanyabiashara kutoa ushirikiano kwa kuhakikisha wanafuata taratibu za upatikanaji wa leseni halali.
Aidha,katika kipindi hiki cha kuhuisha taarifa za wafanyabiashara aliwatoa hofu kuwa hakuna mfanyabiashara atakaye nyanyaswa au kubughudhiwa na maafisa wa kuchukua takwimu.
"Hakuna mtu atakayekwenda kunyanyaswa katika kipindi hiki sisi tunakwenda kuhuisha taarifa zetu, tuanze sasa...kwamba ndugu yangu ulikuwa una duka na mtu aliyekupa leseni alikupa leseni feki sasa tunakupa wiki mbili nenda kajiandae ukate leseni halali na sasa tumeanzisha kanda kurahisisha huduma, hivyo nenda Kanda iliyokaribu yako kakate leseni yako uweke dukani kwako,"alisema Mheshimiwa Mpogolo.
Aidha, Mheshimiwa Mpogolo amesema kuwa, zoezi la ukusanywaji na uhuishaji wa taarifa za wafanyabiashara katika Halmashauri ya Jiji hilo ambao ulianza mapema jana na kutarajiwa kukamilika Septemba 14, mwaka huu, taarifa hizi zitasaidia kujua idadi ya wafanyabiashara waliopo ikiwa pamoja na kujua wenye leseni feki.
"Na huyu mtu, huyu mfanyabiashara ajue hii leseni anaenda kukata ina faida gani kwake, jamii yake na Taifa lake. Tunaomba wafanyabiashara wote na wananchi tuungane mkono, tusaidiane tunakwenda kukusanya hizo taarifa na katika hicho kipindi cha kukusanya data, tunategemea kuanza tarehe 1 Septemba mpaka tarehe 14 mwaka huu,"slisema Mheshimiwa Mpogolo.
Ameongeza kuwa, katika kipindi hicho cha ukusanyaji wa taarifa, halmashauri itatumia watumishi kutoka Serikalini ikiwemo walimu ambao watakuwa kwenye kipindi cha mapumziko, ili kuhakikisha wanapata data zote za wafanyabiashara kwa kila mtaa katika mitaa yote 159.
"Kwa maana yake hizo data zitatumiwa na sisi Serikalini, lakini zitatumika kwa taasisi mbalimbali, aidha, zitatumika pia na taasisi za Elimu ya Juu kwa ajili ya tafiti mbalimbali kwa manufaa ya taifa letu, hivyo tunawaomba na kuwasihi, ninyi ndiyo wadau wenyewe muhimu tunahitaji ushirikiano wenu,"aliongeza Mhe. Mpogolo.