NA GODFREY NNKO
SOKO la Bidhaa Tanzania (Tanzania Mercantile Exchange-TMX) limendelea kuwa mkombozi kwa wauzaji na wanunuzi wa bidhaa mbalimbali nchini.
Uanzishwaji wa soko hilo linalosimamia mnada wa kidigitali licha ya kuwaunganisha wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi, limetoa jukwaa pana la uhakika wa masoko,kuongeza ushindani,uhuru wa kuamua bei na uhakika wa malipo.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX),Godfrey Malekano ameyabainisha hayo Septemba 7, 2023 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
TMX ni taasisi ya 11 tangu vikao kazi hivyo vianze ambapo, mashirika, taasisi za umma zinapata nafasi ya kuelezea zilipotoka, zilipo na zinakoelekea kwa ustawi bora wa umma na Taifa.
Kuhusu TMX
Malekano amesema, Soko la Bidhaa Tanzania ni mfumo rasmi unaokutanisha wauzaji na wanunuzi kwa pamoja na kufanya biashara ya mkataba inayotoa uhakika wa ubora, ujazo na malipo hivyo ili kupata mafanikio makubwa inahitaji uwekezaji wa kisasa wa maghala.
"Soko hili huleta wanunuzi wengi wa ndani na nje ya nchi ambao sio lazima wafike kwenye soko la bidhaa au nchini kwa kuwa mauzo katika Soko la Bidhaa hufanyika kwa kutumia mfumo wa kidijitali ambao huwawezesha wanunuzi wa bidhaa kufanya manunuzi popote walipo ndani na nje ya nchi.
“Mchakato wa kuanzisha Soko la Bidhaa ulianza muda mrefu, mwaka 2009 wakati wa uzinduzi wa ule Mpango wa Kilimo Kwanza ambapo mazungumzo makubwa yalikuwa ni kuongeza uzalishaji wa mazao.
“Ikaonekana kwamba zaidi ya kuongeza uzalishaji kuna suala la masoko, Soko la Bidhaa likatajwa kama moja ya jambo muhimu, kazi ikaanza mwaka 2012 kwa kupata baraka za Baraza la Mawaziri mwaka 2014,” amesema.
Amesema kuwa, mradi wa kuanzishwa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) ulizinduliwa Novemba 30,2015 na Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete.
“Sheria ya Masoko ya Bidhaa ilipitishwa na Bunge mwaka 2015 na kanuni za Soko la Bidhaa zilitolewa na Waziri wa Fedha mwaka 2016, mchakato wa kukamilisha sakafu ya bishara ulianza mwaka 2017 na Soko la Bidhaa Tanzania lilianza rasmi mwaka 2018,"amesema.
Ushirikishwaji
"Pia suala la ushirikishwaji wa wadau ndugu zangu waandishi wa habari tunahitaji sana, na pia kuwa na engagement sana, lakini tumefanya sana maeneo mengine.
"Tumeweza kukaa na wizara mbalimbali ambazo hasa zinahusika kwa mfano Wizara ya Kilimo, Wizara ya Fedha,Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Uvuvi, Wizara ya Nishati, Wizara ya Madini na nyinginezo."
Kupitia kikao kazi hicho chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, Afisa Mtendaji Mkuu wa TMX amesema, utafiti ni sehemu ya jukumu muhimu kwa TMX katika kutekeleza majukumu yake.
“Kazi ya kujenga mfumo imara wa Soko la Bidhaa inategemea mchango wa serikali, taasisi na sekta binafsi hivyo, ushirikiano ni muhimu sana kufikia adhima hiyo.
"Pia taasisi za Serikali ikiwemo bodi za mazao, wadau wa Benki ya Dunia tumeweza kushirikiana nao ili kuweza kujenga mfumo ambao utasaidia sote katika kuleta maendeleo katika nchi yetu.
"Dira yetu ni kuwa soko linaloongoza anuai zaidi na linalokwenda na wakati katika nchi za Afrika Mashariki na nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
"Na dhima ni kutoa huduma za kisasa na ufanisi kwa uwazi na uadilifu,pia kuwa jukwaa la kuaminika kwa mauzo ya bidhaa kwa njia ya teknolojia ya juu na kutimiza malengo ya maendeleo ya Taifa.
"Tuna Sheria ya Masoko ya Bidhaa ya mwaka 2015,lakini pia tuna taratibu za masoko ya bidhaa ya mwaka 2016 na kuna hizi kanuni za masoko ya bidhaa.
"Lakini,kuna sheria zingine kama sheria na miongozo ya mauzo ya bidhaa, mfano unataka kuuza bidhaa kama kahawa lazima muongozo unatengenezwa mara nyingi Soko la Bidhaa,Tume ya Ushirika,Wizara ya Kilimo wanahusika kutengeneza huu mwongozo na mara nyingi huwa unatolewa na Wizara ya Kilimo kwenda ku-cover hilo zao.
"Kuna Sheria ya Fedha, katika kufanya malipo lazima sheria uangalie inasemaje kwa malipo yanayofanyika kwa malipo ya bidhaa, lakini pia kuna sheria za chakula na ghala za mwaka 2005 na mabadiliko ya mwaka 2015 kifungu cha 70 (a).
"Sheria ambayo ilifanyiwa mabadiliko ili kuruhusu mazao yanayoingia kwa mfumo huo yauzwe kupitia Soko la Bidhaa, lakini pia tunaangalia Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na mabadiliko ya mwaka 2017.
"Kama mnavyokumbuka suala la makinikia, Serikali ilisema ianzishe vyombo vingine kwa ajili ya kuhusika na mauzo ya madini mojawapo ni hizi Mineral Trading Centers mikoani.
"Kwa hiyo, sheria hiyo pia pawepo na Mineral Exchanges, kwa hiyo sasa hivi tunafanya kazi kwa karibu na Mineral Exchanges ili kuangalia mifumo ya mauzo jinsi ilivyo kwa kupitia mfumo huo kwenda katika mfumo wa Soko la Bidhaa."
Nje
Afisa Mtendaji Mkuu huyo amesema, TMX watajitahidi kuendelea kushirikiana na kufanya kazi na masoko mengine makubwa ya bidhaa duniani kwa ajili ya kupata uzoefu na ujuzi zaidi katika kuendesha soko hilo.
Miongoni mwa masoko hayo amesema ni Nasdaq Futures na London International Financial Futures Exchange (LIFFE),Soko la Bidhaa la Ethiopia, Soko la Bidhaa la Ghana, MCs na NCDEX India.
"Duniani kuna masoko ya namna hii mengi,hivyo tutaendelea kushirikiana na kufanya kazi nayo ili kutoa huduma bora, hata ndani ya China kuna jumba la makumbusho unaona kuna siti pale kwa ajili ya traders kukaa na kufanya biashara.
"Lakini kutokana na advancement ya teknolojia wote wanafanya kazi kutoka kwenye ofisi yao,ukienda MCs pale Libya unaweza ukaona chumba kimejaa watu unadhani ni traders, lakini ni wafanyakazi kwa ajili ya kusapoti trade.
"Lakini, wale wanaofanya biashara wapo kwenye maofisi yao, majumbani lakini hata kwa simu unaweza ukafanya biashara hata njiani kwa kutumia simu yako."
Benki
Kwa sasa soko hilo nchini limewekeza katika teknolojia mbalimbali ikiwemo mabango ya kidigitali ya kusambaza taarifa za mauzo,uwekezaji katika Soko la Bidhaa-Trading Floor.
Pia,uwekezaji katika Soko la Bidhaa-Data Centre ambapo linashirikiana na benki nane ambazo zimekuwa zikifanya malipo kwa kiasi kikubwa nchini.
“Mabango ya Kidijitali (Electronic Display Units) yanaendelea kuwekwa katika baadhi ya maeneo ya kimkakati kwa ajili ya usambazaji wa taarifa za bei na soko kwa wadau na umma.
"Hivyo, Mfumo wa Kielektroniki umetengenezwa katika njia ambayo wadau wanashiriki popote walipo.Mpaka sasa tuna benki karibu nane ambazo tumeshaingia nazo mikataba, ambazo zina akaunti kwa ajili ya minada hii, hizi fedha hazichanganywi, hii ni muhimu sana.
"Pia tuna mfumo wa kielekitroniki tunautumia japo kuna marekebisho kwa mfano kama kwenye pamba kuna mfumo tulikuwa tunautumia."
Hamasa
"Tumehamasisha watu wengi tumeshawafikia kama watu 190,000 mikoa 25 kutoka mwaka 2018, pia tunafanya tathimini ya mnyororo wa thamani kwa mazao kama choroko, pamba, ufuta na kahawa, na mazao kama iliki,mkonge, nyama,mbuzi,nyanya,vitunguu na ndizi.
"Lakini pia tunafanya ushirikiano na masoko mengine ili kupata ujuzi na uzoefu, lakini pia huko mbele ku-process mikataba.
"Lakini pia mfumo wetu unaruhusu price filter, hii ni muhimu kwa ajili ya kukinga bei, sisi tunapata bei za Marekani, na nchi nyingine kupitia huu mfumo.
"Mpaka sasa tumeuza bidhaa za tani 135, 000, toka mwaka 2019 ambapo mauzo yalianza rasmi mpaka mwaka 2023, mwaka 2020 tuliuza tani 41,134 na zaidi ilikuwa suala la ufuta na choroko katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
"Lakini pia kahawa,mfumo wetu umefanya kazi vizuri, wakulima wanakuja na wanapata bei nzuri sana hasa Arabika na Robusta wao kwa sasa ndio wanakuja kwetu na mfano tumeuza tani 47,000 za kahawa na mwaka huu bado unaendelea na mauzo bado yanaendelea.
"Kwa hiyo, thamani ya zile bidhaa tulizoziuza ni karibia shilingi bilioni 287.98 na hizi fedha kwa kiasi kikubwa kimelipwa kwa wakulima hapa nchini.
"Na ukiangalia katika mapato ya ziada kabla ya kuleta Soko la Bidhaa kwa wastani kwa kilo wakulima wameweza kuongeza 1,850.Wakulima pia wanakuwa huru kuuza bidhaa zao kwa uhakika mzuri, pia ufahamu umeongezeka sana.
"Pia imekuwa njia rahisi ya halmashauri kukusanya mapato tofauti na zamani wanakuwa hawana haja ya kutumia nguvu nyingi bali wanapata mapato makubwa.
"Hii itasaidia biashara ya Kimataifa kwa gharama nafuu sana, mfumo wa kielektroniki una faida kubwa sana. Soko la Bidhaa litaendelea kutoa elimu na kuwafikia wadau wengi zaidi ili wafahamu mchango wake katika uchumi wa nchi.
"Pia soko la bidhaa litaendelea kujiendesha kwa ufanisi, uadilifu na uwazi ili kulinda maslahi ya washiriki wake wote kwenye soko la bidhaa hakuna njia za mkato, bali uadilifu.
"Ili kujenga uchumi imara tutaendelea kufanya utafiti kwa kushirikisha na wadau mbalimbali kuongeza ufanisi unaotakiwa sambamba na kuuza taarifa muhimu.
"Aidha, Soko la Bidhaa litaendelea kushirikiana na wanahabari kuhakikisha taarifa zinawafikia watu wengi zaidi na kujenga ushirikiano unaoleta tija kwa maendeleo ya taifa letu.
"Kama uliahidi kununua mahindi shilingi labda kilo moja shilingi 1500, sokoni ni shilingi hata kama ni shilingi 1000, lazima umlipe shilingi 1500.
"Sasa kibinadamu sio rahisi sana ndio maana katika masoko haya kuna vyombo vingine ambavyo vinaanzishwa kama Central Counterparty (CCP).
"Hizi CCP ni kama benki tu, mfano wewe ukienda leo ukasema nitalipa, mimi nitanunua haya mahindi shilingi 1500, kwa hiyo ile bei kama iko shilingi 1200, inabidi ulipe kule kwenye CCP ile jinsi bei inavyofanyika kwenye soko.
"Kama bei imefika 1300, ina maana kwamba shilingi 200 iweze kuwekwa kwenye CCP ikifika mwezi wa Desemba kule kwenye CCP tayari kuna tofauti ya bei kati ya soko na hela ambayo ulikuwa part, hata kama bei ni 1300, wewe mkulima kuna shilingi 200 umeshawekewa.
"Hii inaweza kuwafanya wakulima wakajikinga na madhara hasi, mkulima angependa apate bei nzuri, lakini kuna processor ambaye anazalisha unga angependa naye mwezi wa 12 anunue mahindi kwa bei fulani watu wote hawa wanaingia sokoni.
"Kuwa part mbili tu bado haijakamilika ile side inahitaji kuwa na regulators hawa ni watu ambao kama wabashiri, kazi yao ni kama investors wanaangalia bei ya mahindi inaweza kuwa hata 1800, ndio wanaingia kuongeza impurity kwenye hilo soko.
"Lakini pia kuna watu ambao wanatake-advantage kutoka soko moja kwenda soko jingine kwa mfano kuna soko ambalo lina high price na jingine low price wao wanakuja kutake hilo gape hapo kati.
"Ili tuwe na futures contract lazima tuwe wote watatu CCP,Arbitrator katika development ya haya masoko ukiangalia kwa Afrika bado hatujafikia level ya kuwa na futures contract kwa sababu kuna futures option, kwamba nitakuuzia mahindi 1500, mwezi wa 12 hata kama kuna premier unatoa premier zaidi ikifika mwezi wa 12 unaangalia bei nzuri.Na kwa hili, Afrika Kusini wana hilo.
"Lakini, ukiangalia Ghana, Nigeria, Burundi, Rwanda, Malawi wote wako kwenye Spot Market, bidhaa zinakuwa kwenye maghala kwa hiyo inakuja kufanyika kama mnada ambao una exist.
"Lakini ningependa kusema kwamba masoko yote duniani hata ukienda Marekani utakutana na Futures Contract kwa sababu ya advantage kubwa unakuwa na mfumo ambao unakinga risk na unatoa faida.
"Wanaouza wanaona na wanaonunua wanaona na katika ushindani wanashindana na kama una bei kubwa ndiye utakayeshinda.
"Ushindani wa haki pia unasababisha ufumbuzi sahihi wa bei mnaposhindana pale bei inakuwa haijulikani kila mtu anaweka pale bei kulingana na need aliyonayo.
"La msingi, masoko haya ya bidhaa ni kuwa na washiriki wengi kwa maana ya wanunuzi upande mmoja na wanunuzi wengi upande wa pili ili washindane kupata bei.
"Sasa hivi kazi ninayoifanya ni kuwaandalia miaka ya usoni ili kuwa na hizo Futures Option Sontract, tunaendelea kujadiliana na watu kuangalia sheria ya mifumo na mikataba inasemaje na sheria za malipo ili kulinda sheria za washiriki.
Kwa nini soko hili?
Afisa Mtendaji Mkuu huyo anasema, Soko la Bidhaa Tanzania limekuwa na mchango mkubwa kwa wauzaji, wanunuaji na serikali kwa ujumla ikiwemo kuimarisha bei ya soko.
Pia, upatikanaji wa taarifa za soko, kuvumbua bei za bidhaa, kupunguza gharama za kuuza na kununua, wakulima wako huru kuamua bei walioridhia kuuza bidhaa zao.
Aidha, amesema imekuwa ni njia rahisi ya kukusanya mapato kwa halmashauri, lakini pia urahisi wa usimamizi wa utoaji wa vibali husika kwa usafirishaji wa bidhaa zilizouzwa, imesaidia upatikanaji wa fedha za kigeni.
Kwa sasa soko hilo limejipanga kutoa elimu na kuwafikia wadau wengi zaidi ili wafahamu mchango wake katika uchumi wa nchi, kujiendesha kwa ufanisi, kidijitali na kutoa huduma zake kwa uadilifu ili kulinda maslahi ya washiriki wake wote, kufanya utafiti kwa kushirikiana na wadau husika ili kuongeza bidhaa zaidi.
"Kwa nini Soko la Bidhaa? Kama nilivyosema Mpango wa Kilimo Kwanza walikaa watu wakaangalia sana na mifumo ya nchi nyingine waliofanikiwa wakaona kuna hitaji la kuwa na Soko la Bidhaa.
"Lakini pia waandaaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2016 ulioishia 2021 na ule wa mwaka 2021 na 2025 yote imetaja kwamba Soko la Bidhaa liwepo na lifanye kazi zake ili kuchangia maendeleo ya taifa.
"Lakini pia pia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili imataka Soko la Bidhaa lifanye kazi liweze kutatua matatizo ya soko, pia Ilani ya chama tawala 2015/ 2020 na ile ya 2020 na 2025 imetaja pia.
"Kuna haja sasa ya kuimarisha mifumo iliyopo, kwa mfano mfumo wa ushiriki wa ghala na mfumo wa ushirika. Sasa hivi mazao wanayashusha hadi kwenye maghala yale yaliyopewa leseni.
"Lakini utaratibu wa mauzo hayo na kutambua kwamba sasa hivi tunatumia masanduku yale ya watu kufanya hiyo minada.
"Changamoto kubwa ni ubora wa bidhaa, uhifadhi wa mazao yetu unaofanyika majumbani, tunaishuru Serikali ya Awamu ya Tano, Awamu ya Nne na Awamu ya Sita wamefanya kazi kubwa kujenga maghala.
"Hizi nafaka kwenye haya maghala ya kawaida kwenye magunia tunayotumia sio namna nzuri sana ya kuhifadhi, kwa sababu hilo gunia linaweza kuwa na mawe, mchanga na kila kitu.
"Lakini hizi bidhaa za nafaka zikiwekwa kwenye sailoti ukifika pale wanasoti mawe kushoto, mahindi kulia kwa hiyo unakuwa na uhakika kwenye ghala kiasi kadhaa.
"Kama mnavyojua vijijini mazao mengi hayana utunzwaji mzuri, panya nao wanaishi kwenye mazao hayo unaweza kuwa na gunia saba za mahindi mwisho wa siku unakuta zimepukuchuliwa na panya.
"Lakini ukiwa na miundombinu ya kisasa inakuwa vizuri, lakini tunapokuwa tunasema tuna tani milioni 7 za mahindi kwenye maghala ni rahisi tu kusema tuna ziada ya tani milioni 2, lakini kama mahindi yako majumbani tunakuwa na hisia tu, tunasema tuna ziada, lakini kumbe ile ziada haitoshelezi,"amefafanua kwa kina Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX),Godfrey Malekano.
Pia anasema, litakuwa jambo la faraja iwapo wafanyabiashara kutoka nchi jirani watanunua mahindi na mchele hapa nchini kwa kutumia dola.
"Vivyo hivyo ili shilingi yetu iwe imara, lakini kama Mheshimiwa Waziri wetu alivyosema kuna miradi mingi ya kimkakati ambayo inaendelea kutekelezwa hapa nchini ikiwemo Bwawa la Mwalimu Nyerere na Reli ya Kisasa, hivyo tunahitaji dola, kwa hiyo tunapopata dola nyingi zaidi tunaweza ku-cover masuala kama hayo."
Malekano amesema, hatua hiyo si tu itasaidia Taifa kukabiliana na upungufu wa fedha za kigeni ambao unazikumba nchi mbalimbali duniani kwa sasa, bali utazidi kuimarisha akiba ya fedha za kigeni nchini na kusaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati.
"Lakini pia haya mahindi au mpunga tungependa na sisi tupate dola kama wanavyofanya kwenye mifugo, watu wanatoka Kenya kuja kununua mifugo hapa Tanzania kwa kutumia shilingi wanavuka mipaka wanaingia, lakini wenyewe wanapeleka Uarabuni, wanakwenda kuuza kwa dola.
"Kwa sababu sisi tunaponunua mbolea au viuatikifu tunalipa kwa dola nje, ni vizuri hata wanaokuja kununua wakalipa kwa dola na ili lifanyike ni lazima mazao yakae kwenye maghala."
Amesema, ili haya yaweze kufanikiwa kwa ufanisi ni wakati wa Serikali na wadau mbalimbali kuwekeza katika maghala ya kisasa ambayo yatawezesha mifumo kama yao ifanye kazi, pia kuwe na ubora wa bidhaa unaotakiwa na kuthibitika.
Ni salama
Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX),Godfrey Malekano anasema, wanunuzi na wauzaji wakitumia masoko ya namna hii ni salama zaidi kwa upande wa fedha, mali na maisha yao.
"Lakini malipo kukosa uhakika,wafanyabiashara wengi Zambia, Malawi wakileta kuuza hapa Dar es Salaam kwenye magodauni wanazungushwa, wengine wanatapeliwa, tunamshukuru Waziri wa Kilimo anasimama imara kutetea wafanyabiashara.
"Lakini kama yale mavuno wakiyafanya wakitumia masoko kama ya kwetu ya bidhaa hilo suala la risk linaondoka.
"Jambo jingine gharama kubwa za miamala ukitaka mahindi hadi uende huko kijijini na wafanyabiashara wengi kuna ushahidi kwamba wanawapa watu fedha mtu anakwenda kujikata kata mikono anasema nilivamiwa na majambazi.
"Lakini ukiwa na masoko ambayo ni imara na malipo yanafanyika vyema ukinunua unalipa benki yako suala la kujikata kata linakuwa halipo.
"Pia upatikanaji wa taarifa sahihi ni muhimu, pia kuleta ufanisi, kwa mfano ukiangalia kwenye mazao kama ya mahindi ukienda Ruvuma, Katavi, Shinyanga utakuta kuna watu wengi sana wananunua moja kwa moja kwa wakulima kule chini,"amesisitiza Afisa Mtendaji Mkuu huyo.
Mbali na hayo amesema kuwa, wataimarisha zaidi mfumo wa stakabadhi ghalani, na ushiriki wa vikundi vya wakulima ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ili kuwafikia wadau wengi nchini.
Pia amesema, kazi ya kujenga mfumo imara wa Soko la Bidhaa inategemea mchango wa Serikali taasisi na sekta binafsi hivyo ushirikiano ni muhimu kufikia adhima hiyo.
Amesema kuwa, kwa sasa soko hilo linafanya mauzo ya papo kwa papo huku lengo likiwa ni kuanzisha mauzo ya mkataba pale miundombinu itakapoboreshwa.
Amesema, soko hilo linasaidia taarifa za ukusanyaji wa mapato, usimamizi wa utoaji wa vibali kwa usafirishaji wa bidhaa pamoja na upatikanaji wa fedha za kigeni.
Malekano amesema. kutokana na kuipa kipaumbele sera ya soko la pamoja la Afrika hivyo ni muhimu kuzingatia viwango vinavyofanana ili kuboresha biashara kati ya nchi na nchi ndani ya Afrika.
Alisema juhudi zilizofanyika hadi sasa ni kuendelea kuboresha mfumo wa kielektroniki ili kuongeza bidhaa zaidi kwa ajili ya mauzo.
Vile vile amesema, kwa sasa mfumo wa kielektroniki wa TMX unaweza kuhusisha ‘reverse actions’ ambapo wanunuzi wanaweza kutangaza kununua kiasi fulani cha bidhaa ya daraja maalum katika eneo maalumu la kuwasilisha na wauzaji kushindana kwa bei kwenye mfumo wakati wa mauzo.