GEITA-Mkurugenzi wa Royal Family Schools, Mhandisi Lazaro Philipo amesema kuwa, wanafunzi wanaosoma katika shule hizo wanaandaliwa kimaadili kwa tumia masomo ya dini ili kuwaandaa kuwa raia wema katika jamii.
Ameeleza hayo Septemba 16 ,2023 katika mahafali ya kidato cha nne wa Sekondari ya Royal Family Sekondari na Darasa la Saba wa Royal Family Primary yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari ya Royal Family mkoani Geita.
Amesema kuwa, shule hizo zinatumia vipindi vya elimu ya dini kuwakaribisha viongozi wa dini wa Kikristo na Kiislam kuadubu na kupata mafunzo ya maadili mema jambo ambalo linawafanya wanafunzi hao kuwa na tabia njema.
Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Mkuu wa Wilaya ya Nyang'hwale, Grace Kingalame ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Geita, amesema wazazi watakiwa kuwalea watoto wao katika maadili mema ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili ambao unasumbua Dunia kwa sasa.
Amesema, mmomonyoko wa maadili ni tatizo linaloitesa dunia kwa sasa,hivyo kila mzazi achukue hatua na kuhakikisha mtoto wake analelewa katika maadili mazuri, hivyo kuepuka pia ukatili kwa watoto.
Ameeleza kuwa, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanafunzi wanasoma kwa vitendo zaidi ili wakihitimu waweze kujiajiri na kuajiri wengine.