MBINGA DC YAVUKA LENGO UKUSANYAJI WA MAPATO, YAKUSANYA BILIONI 6.478/- KWA MWAKA WA FEDHA 2022/2023

RUVUMA-Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imevuka lengo katika ukusanyaji wa mapato kwa kukusanya mapato ya ndani kiasi cha shilingi Bil. 6.478 katika mwaka wa fedha 2022/ 2023 ulioanza Julai 1, 2022 hadi Juni 30, 2023.
Makisio ya awali ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2022/2023 yalikuwa Shilingi 4,598,598,800 yakijumuisha mapato lindwa na mapato halisi.
Mapato hayo yametokana na kodi na tozo, miamala ya kibiashara,tozo na ushuru mbalimbali,misaada kutoka nje pamoja na mapato mengineyo.

Taarifa hii imetolewa 31 Agosti 2023 na Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga CPA Samwel James Marwa katika Kikao cha Baraza la Madiwani kujadili na kuidhinisha hesabu kwa kipindi kilichoanzia tarehe 01 Julai 2022 hadi 30 Juni 2023.

Marwa ameongeza kuwa jumla ya mapato ya Ruzuku yaliyopokelewa ni Shilingi Bil. 30.7 fedha ambazo zimetumika kwa matumizi ya kawaida na maendeleo kama vile stahiki za watumishi, manunuzi ya huduma mbalimbali,matengenezo pamoja na haki za kijamii.

Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya usimamizi wa Menejimenti,Ufatiliaji na Ukaguzi (MMI) Mkoa wa Ruvuma Phiniel Mbula ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato ameitaka Halmashauri hiyo kuendelea kuimarisha usimamizi katika ukusanyaji na matumizi ya mapato. 

Amesema"Nitoe pongezi zangu kwa Halmashauri hii Mkoa unafahamu jitihada mnazofanya katika kuhakikisha mnasimamia ukusanyaji wa mapato, endelezeni ari hii."

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Ndg. Andrew Mbunda amebainisha kuwa Halmashauri itaendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani ili fedha hizo zitumike katika kutekeleza miradi ya maendeleo yenye kuleta tija kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news