Mheshimiwa Mpina aibua hoja nzito Itifaki ya Biashara ya Huduma ya SADC 2012

MCHANGO WA MBUNGE WA JIMBO LA KISESA, MHESHIMIWA LUHAGA JOELSON MPINA (MB) KUHUSU AZIMIO LA BUNGE LA KURIDHIA ITIFAKI YA BIASHARA YA HUDUMA YA JUMUIYA YA MAENDELEO KUSINI MWA AFRIKA YA MWAKA, 2012 (SADC PROTOCOL ON TRADE IN SERVICES,2012) BUNGENI DODOMA TAREHE 31 AGOSTI 2023

UTANGULIZI

Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Southern African Development Community-SADC) ili kuendelea kuimarisha mtangamano na fursa za biashara hususani Biashara ya Huduma kwenye Kanda ya SADC na Kitaifa nchi wanachama zilisaini na kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya mwaka, 2012.

Itifaki ya Biashara ya Huduma (Protocol on Trade in Services) ikiwa inaletwa kwa hatua ya kuridhiwa na Bunge wakati ambao soko la SADC ni soko la kutegemewa katika kuuza na kuagiza bidhaa na huduma.

Soko la SADC ni soko la pili kwa ukubwa ikitanguliwa na Bara la Asia, Masoko mengine ni pamoja na EAC, EU, AGOA. 

Mfano mauzo ya katika Soko la SADC ilifikia Dola za Marekani milioni 1802.2 sawa na shilingi trilioni 4.51 na uagizaji wa bidhaa ulifikia Dola za Marekani 551.3 sawa na shilingi trilioni 1.38 mwaka 2022.

Tunapoliendea suala la lolote kuhusu soko la bidhaa na huduma la SADC inatupasa kuwa na umakini wa hali ya juu.

MAMBO YA KIUJUMLA

Baada ya kupitia Ibara za Itifaki hii,Hotuba ya Waziri wa Viwanda na Biashara na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo nimebaini mambo yafuatayo:-

(i) Tanzania imechelewa kuridhia Itifaki hii kwa muda wa miaka 11 tangu Itifaki hii isainiwe na Marais wa nchi wanachama Agosti 18, 2012 mjini Maputo nchini Msumbiji. Sababu za kuchelewa kuridhiwa itifaki hii hazijaelezwa mahali popote. 

Mazingira yaliyokuwepo ni kama ifuatavyo:-
(a) Katibu Mtendaji wa SADC alikuwa Dkt.Stergomena Lawrence Tax kutoka Tanzania tangu mwaka 2013 hadi 2021, lakini Itifaki hii haikuridhiwa katika
kipindi chote hicho.

(b) Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete hakuipeleka Itifaki hii kuridhiwa Bungeni hadi anaondoka madarakani Novemba 
2015 miaka minne (4) baadaye tangu aliposaini Itifaki hiyo mwaka 2012.

Serikali inapaswa kutoa maelezo ya kina na kuwaeleza watanzania sababu zilizokwamisha Itifaki hii kutoridhiwa na nchi yetu kwa miaka 11, na leo nini kimeisukuma Serikali kuileta Itifaki hii kuridhiwa? Na je changam I oto za awali zimetatuliwaje ili tusije kuliingiza taifa letu kwenye matatizo.

(ii) Haijaelezwa kwa ufasaha Itifaki hii inaenda kutatua tatizo gani katika Mtangamano huu wa biashara wa nchi za SADC, kwani zipo Itifaki zilizoridhiwa na zinatumika kwa sasa ikiwemo Itifaki ya Biashara ya SADC (SADC Protocol on Trade), Itifaki ya Biashara na Uwekezaji ya SADC ( SADC Protocol on Finance and I'm vestment). 

Nilitegemea Bunge lingeelezwa tathmini ya utekelezaji wa Itifaki zilizopo za SADC ba dala ya kuletewa Itifaki nyingine kuridhiwa.

(iii) Itifaki ya Biashara ya Huduma, inahusisha sekta sita za kipaumbele ambazo ni Mawasiliano, Fedha, Utalii, Uchukuzi, Nishati na Ujenzi kama ilivyoelezwa katika
Ibara ya 16 (2) ya Itifaki hii.

Lakini, haijaelezwa kwa kina ni kwa namna gani na kwa muktadha gani nchi hizi 
wanachama zitashirikiana katika sekta husika ili kuliwezesha Bunge na wananchi kuelewa kinachoridhiwa na faida zitakazopatikana kwa nchi yetu.

(iv) Haijalezwa kwa nini nchi tano za Tanzania, Angola,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Madagascar na na Comoro hazijaridhia Itifaki hii kwa zaidi ya miaka 11 tangu iliporidhiwa 2012. Lakini pia haijaelezwa faida zinazopatikana katika nchi 11 zilizoridhia Itifaki hiyo.

UCHAMBUZI WA ITIFAKI

(i) Ibara ya 6 (2) na 6 (3) ya Itifaki hii inataka kuanzishwa kwa Mahakama na Mabaraza ya Usuluhishi kwa kila nchi ili kuwezesha utatuzi wa athari zinazoweza kuwapa watoa huduma (an affected Service supplier).

Je?, Mfumo wa Mahakama zetu utabeba vipi matakwa ya Ibara hizi ili kukidhi masharti ya Itifaki.

(ii) Ibara ya 6 (4) ya Itifaki hii inataka CMT-Committee of Ministers Responsible for Trade kuanzisha utaratibu wa kinidhamu kwa nchi wanachama (CMT shall develop any necessary discipline ).

Ibara hii inakwenda kinyume  na matakwa ya WTO ambapo nchi zote katika utengamano wa kibiashara zinasimamiwa na utaratibu wa kinidhamu uliowekwa chini ya General Agreement on Trade in Services (GATS).

Kuruhusu CMT kuandaa utaratibu mpya wa kinidhamu ni kuleta mkanganyiko ambao unaweza kusababisha nchi za SADC kutumia muda mwingi kusuluhisha migogoro badala ya kujenga uchumi wa nchi zetu.Tuepuke kufungua hili Pandora’s box.
 
(iii) Ibara ya 8 (2) inaweka sharti la mabadiliko yoyote ya sheria,kanuni na miongozo inayoathiri biashara ya huduma katika nchi wanachama kuitaarifu TNF-Service (Trade Negotiating Forum for Services).

Takwa hili la Itifaki hii linaweza kutuletea matatizo makubwa kwa nchi wanachama na kuvuruga mahusiano yetu ya kibiashara tuliyoyajenga kwa muda mrefu katika Jumuiya na Soko la SADC ambalo tunalitegemea kwa kiwango kikubwa katika kuuza bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini.

Sisi hatuko vizuri sana na bahati mbaya tumekataa kubadilika, mfano katika Sheria za Fedha (Domestic Fiscal Legislations) kila mwaka tumekuwa tukibadilisha viwango vya kodi, tozo, ada na ushuru bila utafiti wala tathmini ya kina hali inayopelekea malalamiko kila kona. 

Unakuta kodi mpya zinaanzishwa bila maelezo,zinafutwa bila maelezo, viwango vinaongezwa au kupunguzwa bila maelezo na misamaha ya kodi inatolewa bila maelezo. 

Hivyo, itatupasa kila mwaka kupeleka mabadiliko ya kodi TNF-Services ambayo hayana justification.

(iv) Ibara ya 16 (2) ya Itifaki hii ambayo huduma zilizofunguliwa katika sekta 6 ni Mawasiliano, Fedha,Uchukuzi, Utalii, Nishati na Ujenzi.

Changamoto ya nchi nyingi za SADC zinategemea utalaamu na bidhaa kutoka nje ya ukanda ya SADC, hivyo ushirika huu unaweza kukosa maana. Mfano hapa nchini.

(a) Sekta ya Mawasiliano, Mradi wa TEHAMA ambapo mkataba uliingiwa baina ya TANESCO na TechMahindra (India) wa zaidi ya shiliongi Bilioni 70, Mradi wa ETS ambapo mkataba umeingiwa baina ya TRA na Kampuni ya SICPA, 

Makubaliano baina ya Shirika la Posta na Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa uendeshaji wa Posta. Pia kumekuwepo na uazishwaji holela wa mifumo  ya TEHAMA bila hata kibali cha eGA, mfano Mfumo wa Mbolea ya Ruzuku na Mfumo wa TEHAMA wa TANESCO (huduma hizi zilikuwa zinapatikana katika ukanda wa SADC lakini tulizinunua nje).

(b) Sekta za Ujenzi na Uchukuzi, kazi nyingi katika sekta hii wanapewa wageni wa nje ya ukanda wa SADC na Afrika kwa ujumla miradi ya Barabara,Reli, Meli na Bandari.

(c) Sekta ya Fedha, nchi nyingi za SADC zinatumia Dola za Kimarekani na hivi sasa kuna upungufu mkubwa sana wa Dola hasa hapa nchini kwetu na kusababisha biashara kukwama. 

Ukosefu wa Dola hapa nchini hauna maelezo ya kutosha huku ikielezwa kuwa uwekezaji na watalii nchini wameongezeka mara dufu. 

Pengine chanzo kikubwa inaweza kuwa ni ufisadi uliotamalaki ambapo taarifa ya Financial Intelligence Unit (FIU) inaonyesha kuwepo kwa miamala shuku yenye thamani ya zaidi ya shilingi Trilioni 280 kuishia Februari 2023. 

Hii ni ushahidi kwamba fedha nyingi za kigeni zimeibiwa na kutoroshwa nje ya nchi kupitia mipakani na mabenki (Illicit Financial Flows).

(d) Uzalishaji mdogo, usio endelevu na masuala ya ubora katika mazao ya madini, pamba, chai,parachichi, kahawa, vigae, vyandarua, saruji,sabuni na mafuta ya kupaka ambayo yanauzwa kwa wingi katika ukanda wa SADC hali inayopelekea kushindwa kukidhi mahitaji ya soko.

(e) Nchi nyingi za SADC zinategemea bidhaa na huduma kutoka nje ya Kanda hali inayoharibu urari wa biashara, uhamishaji wa ajira, mfumko wa bei na kuadimika kwa fedha za kigeni.

(f) Mfumko mkubwa wa bei usioratibiwa mfano Waziri wa Nishati, Mhe. Januari Makamba baada ya  ongezeko la bei ya nishati ya mafuta la karibia shilingi 500 kwa lita moja katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Agosti 2023, alipokutana na wafanyabiashara wa mafuta ilielezwa kuwa, kuadimika na kupanda kwa bei ya mafuta kunasababishwa na upungufu wa dola huku akijua fika kuwa malipo ya mizigo ya mafuta yanalipwa moja kwa moja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hapa tuelezwe kwa ufasaha sababu ya kupanda kwa bei ya mafuta ni nini?

Na sababu za kuadimika kwa dola za Marekani ni nini? Leo tunataka kuridhia Itifaki hii ambayo imeweka utaratibu wa nidhamu katika Ibara ya 6 na utaratibu wa namna ya kutatua migogoro kama ulivyoanishwa katika Ibara ya 25 na Kiambatisho Na. 1 (Annex 1) tukiwa hatuna maandalizi na bado Mikataba inaendelea kuingiwa nje na ukanda wa SADC tena katika maeneo yanayojumuishwa katika Itifaki hii.
 
Kwa kuwa, kuna uzalishaji mdogo wa mazao na huduma zinazouzwa katika soko la SADC na hivyo kuhitajika jitihada za makusudi kuongeza uzalishaji huu kwa kutumia mkakati ya Eliminate, Reduce, Raise and Create (ERRC) Grid.
 
Na kwa kuwa, hakujatolewa maelezo ya kina yaliyosababisha Itifaki hii kutokuridhiwa kwa zaidi ya miaka 11, lakini pia haijaelezwa kwa ufasaha namna ya nchi na nchi zitakavyonufaika na Itifaki hii ikizingatiwa kuwa kuna Itifaki ya Biashara ya SADC (SADC Protocol on Trade) na Itifaki ya Biashara na Uwekezaji ya SADC (SADC Protocol on Finance and Investment).

Hivyo basi, kwa maelezo yaliyotolewa inathibitisha mapungufu makubwa ya Itifaki hii (Prima facie) Bunge lisiridhie azimio hili mpaka pale litakapoletewa maelezo ya kina juu ya changamoto  zilizopo katika Itifaki hii na sababu zilizopelekea kutoridhiwa kwa zaidi ya miaka 11 tangu kusainiwa kwake mwaka 2012.

Nawasilisha,
……………………………
Luhaga Joelson Mpina (Mb) 
Mbunge wa Jimbo la Kisesa

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news