Mheshimiwa Pinda asifu mifumo ya Elimu Huria na Masafa kwa maendeleo endelevu

PWANI-Mifumo ya Elimu kwa njia za Huria, Masafa na Mtandao ni daraja muhimu ambalo linaweza kuzivusha nchi za Afrika na Tanzania.
Vile vile kuhakikisha wananchi wake wote wanapata elimu, maarifa na ujuzi utakaowawezesha kujiajiri, kuajiriwa na kuifanya jamii kuwa na maendeleo endelevu.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda katika uzinduzi wa Kongamano la Kwanza la Kimataifa kuhusu tafakuri ya mifumo ya elimu kwa maendeleo endelevu.
Kongamano hilo linafanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kibaha Mkoa wa Pwani kuanzia Septemba 27 hadi 29, 2023.
Mhe. Pinda ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania amesema:"Katika kipindi hiki ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaojiunga na elimu kwenye ngazi za chini kumefanya kuwa na mahitaji makubwa ya wanafunzi wanaotaka kujiunga na masomo ya elimu ya juu baada ya kuhitimu ngazi za chini za elimu.
"Hii inatoa ishara kwamba ni lazima vyuo na taasisi za elimu ya juu zijiandae kwa kujenga miundombinu toshelevu kwa mahitaji hayo.
"Hata hivyo, mifumo ya elimu Huria, Mtandao na Masafa inaonekana kuwa ni muafaka zaidi kwa sababu ufundishaji na ujifunzaji unafanywa huku wanafunzi wakiwa wanaendelea na shughuli zao, kazi zao, majukumu yao na tena wakiwa huko huko walipo.
"Hivyo, mifumo inayotumiwa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na vyuo vikuu Huria vingine katika bara la Afrika na kwingineko duniani ni suluhisho la changamoto ya mahitaji ya miundombinu ya elimu ya juu katika Ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia.
"Kupitia mifumo hii hakuna uthibiti wa idadi maalumu ya wanafunzi wa kusoma. Wanafunzi wengi zaidi wanaweza kujiunga wakiwa katika maeneo ya mjini na vijijini,"amesema Mhe.Pinda.
Kwa upande wake mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Kenneth Hosea ambaye pia ni Mkurugenzi wa Elimu ya Juu amesema kwamba, wizara imepokea mwaliko wa kushiriki kwenye kongamano hili kwa furaha kubwa.
Amesema, kongamano hio limekuja katika kipindi ambacho nchi yetu inafanya kazi ya mapitio ya sera ya elimu na mitaala katika ngazi zote za elimu nchini.

"Wizara yetu inatekeleza kwa vitendo maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuhusu kufanya mapitio ya sera na mitaala ya elimu na kwa sasa tumeshafika katika hatua nzuri na kinachosubiriwa ni maamuzi kutoka katika vyombo husika vya serikali yetu.
"Mitaala ambayo tunapendekeza ni zao la maoni ya wananchi na lengo lake ni kutoa elimu ambayo itawajenga wanafunzi kuwa wabunifu, wenye ujuzi na kujitegemea, kujiajiri na wenye kupenda ujasiriamali.

"Hivyo nitumie fursa hii kuwaeleza mjiandae katika kufanya utekelezaji wa sera na mtaala mpya wa elimu pale utekelezaji utakapoanza,"amesema Prof. Hosea.
Naye, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda ameihakikishia wizara kwamba Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimejipanga vizuri katika utekelezaji wa mtaala mpya na daima chuo hiki kimekuwa msitari wa mbele sana katika kufanya bunifu na kuanzisha programu mbalimbali zenye kukidhi mahitaji ya jamii.
"Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kipo tayari katika kutekeleza sera na mtaala mpya wa elimu nchini ambapo mpaka sasa tayari chuo kimeanzisha stashahada ya ualimu wa shule za msingi, stashahada ya ualimu wa elimu ya awali, stashahada ya uzamili ya ualimu wa ufundi na mafunzo ya amani.
"Wahitimu kadhaa wameshahitimu wanaendelea kulitumikia taifa letu. Kwa sasa chuo kupitia Kitivo cha Elimu kimeshaandaa mtaala wa shahada ya kwanza wa ualimu wa shule za msingi na utaanza kutumika mara baada ya kupata ithibati,"ameeleza Prof.Bisanda.
Kimsingi, programu hizi ni sehemu tu ya nyingi zilizopo Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambazo kwanza zinasaidia kuzalisha walimu wa shahada ya kwanza wenye weledi katika kufundisha masomo mbalimbali ikiwemo ya sayansi.
Kwa mfano, shahada ya sayansi na ualimu ambayo ipo kwa miaka mingi sasa itaendelea kufundisha walimu ambao bado mahitaji yao katika jamii ni mengi na hususani katika kipindi hiki ambacho sera na mtaala mpya vinaelekeza na kusisitiza katika kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kujiajiri na kuajiri wenzao.
Akitoa neno la shukurani, Mkuu wa Kitivo cha Elimu Dkt.Theresia Shavega, amewashukuru washiriki wote wa Kongamano hili ambapo wapo waliotoka katika mataifa 14 ndani na nje ya Bara la Afrika.
Dkt.Shavega ameeleza kwamba, takribani mada 102 zitawasilishwa kwenye kongamana hilo. Hakika huu ni mchango mkubwa na kupitia kongamano hili tutapata maarifa ya kutosha na tena kutoka uzoefu wa wataalamu kutoka nchi mbalimbali na kuutumia katika kuendeleza na kukuza elimu katika nchi yetu kwa maendeleo endelevu.
Kongamano la Kimataifa la tafakuri ya mifumo ya elimu kwa maendeleo endelevu linafanyika kwa siku tatu (27-29 Septemba, 2023) chini ya uratibu wa Kitivo cha Elimu cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania mwenyekiti akiwa ni Dkt. Caroli Mrema na katibu Dkt. Janeth Kigobe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news