Mfumo wa ufuatiliaji na tathmini utasadia kuimarisha utendaji-Dkt.Yonazi

DODOMA-Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshugulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Dkt.Jim Yonazi amesema, mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Shughuli za Serikali ni mfumo mahususi wa uboreshaji wa utendaji Serikalini kwa lengo la kuona ni namna gani Rasilimali za Serikali zinaboreshwa na Kutumika vizuri. 
Hayo ameyasem Septemba 4,2023 ofisini kwake jijini Dodoma alipokuwa katika mahojiano maalum na chombo kimoja cha habari, katika kuelekea Kongamano la Wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini litakalofanyika jijini Arusha wiki Ijayo.
Dkt.Yonazi ameeleza kuwa, Uratibu wa Shughuli za Utendaji wa Serikali katika eneo la Ufuatiliaji na Tathmini una nia ya kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya Serikali unafanikiwa na malengo yanafikiwa. 

Aliendelea kusema kuwa, dhana hii, ni dhana ambayo inalenga katika kuangalia utekelezaji wa Miradi ya Serikali nchi nzima na kuona kama malengo yaliyowekwa katika miradi hiyo yanafanikiwa. 
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshugulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Dkt Jim Yonazi akizungumza na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Augustino Tendwa mara baada ya Mahojiano maalumu yaliyofanyika Ofisi kwake Ngome jijini Dodoma. 

“Ili malengo hayo yaweze kufanikiwa ni lazima tufanye Ufuatiliaji tujue nini kinaendelea, tufanye Tathmini dhidi ya ile mipango ambayo ilikuwa imewekwa, lakini vilevile tuangalie kwamba tunajifunza nini kutokana na kile ambacho tumekiona kutoka katika Ufuatiliaji na Tathmini,”alifafanua.

Aidha, Dkt. Yonazi alimshukuru Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuja na wazo la kuanzisha mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini Nchi nzima.

Sambamba na kuweka vitengo na Idara mahususi kwa ajili ya kazi hiyo katika Wizara na Taasisi za Serikali kwa lengo la kuzipa uzito mkubwa ripoti zinazotokana na Ufuatiliaji na Tathmini katika maamuzi, mijadala na mipango ya Serilikali ili kufikia malengo tarajiwa. 
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshugulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Dkt Jim Yonazi akisalimiana na Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini wa Ofisi hiyo,Bi. Sakina Mwinyimkuu wakati wa mahojiano maalumu aliyoyafanya Ofisini kwake Ngome Jijini Dodoma.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bi. Sakina Mwinyimkuu amesema, pamoja na kongamano hilo kuhusisha wataalam na wadau mbalimbali nchini na nje ya nchi, wananchi kwa ujumla wanaalikwa kupata fursa ya kufahamu namna ambayo serikalini inatekeleza miradi, kwani kwa kiasi kikubwa miradi mingi inakwenda kwa wananchi.

“Mwananchi ndiyo mdau wa kwanza kwani yeye ndio anaweza kujua mradi fulani unatekelezwa vizuri katika eneo husika, kwa hivyo tunaona pia ni fursa kwa mwananchi kuweza kufahamu na kutoa hali halisi ya utekelezaji wa miradi katika maeneo yao,”alisisitiza. 

Kongamano hilo la Pili la Kitaifa la wiki ya Ufuatiliaji na Tathmini litakalofanyika jijini Arusha linaongozwa na kauli mbiu inayosema “Kuimarisha Ufuatiliaji na Tathmini kwa ajili ya kujifunza na kuboresha Utendaji wa Serikali.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news