SONGWE-Wanachi wa Wilaya ya Momba wameeleza kufurahishwa kwao na ujenzi wa Barabara ya Ikana - Iyendwa – Namchika yenye urefu wa kilomita 33 ambapo hapo awali ilikuwa haipitiki na kusababisha adha kubwa ya usafiri na usafirishaji wa mazao kutoka mashambani hadi sokoni.
Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Mtendaji Mku wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor H.Seff aliyeambatana na Mbunge wa Jimbo la Momba Mhe. Condester Sichalwe katika ziara maalum ya ukaguzi wa Barabara na miundombinu yake ndani ya Jimbo la Momba.
Akielezea kuhusu hali ya Barabara hiyo Bw. Samwel Malya ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kasunde amesema kuwa mwanzoni Barabara hiyo ilikuwa haipitiki na shida kubwa ilikuwa ni kipindi cha masika ambapo watu walishindwa kuvuka tofauti na wakati huu baada ya kujengwa na TARURA.
’’Barabara hii ilikuwa haipitiki na kama mnavyoona sasa imejengwa na inatumika, sisi wananchi tunaipongeza TARURA na leo tumetembelewa na Mtendaji Mkuu wa TARURA pamoja na Mhe. Mbunge hivyo tunaimani kuwa na maeneo mengine yasiyopitika sasa yatapitika,"amesema Bw. Malya.
Naye, Mbunge wa jimbo la Momba Mhe. Condester Sichalwe ameeleza kuwa ilikuwa ni ndoto yake kuhakikisha Barabara hiyo inapitika na kutoa huduma kwa wananchi hasa katika kusafirisha mazao na kuzifikia huduma za kijamii kwa urahisi.
"Barabara hii ni ya umuhimu kwa wananchi wa Momba, tunaipongeza kazi inayofanywa na TARURA chini ya Mhandisi Victor Seff, wananchi sasa wanaitumia barabara hii ambayo hapo awali haikuwahi kuwepo na kutumika,"amesema Mhe. Sichalwe.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Itumba,Swedi Laurent Sikonde amempongeza Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff kwa kufika Kijijini hapo na kujionea hali ya Barabara hiyo na kwamba matarajio ya wananchi ni kuona serikali inaendelea kuboresha suala la usafiri na usafirishaji katika Kijiji hicho.
Akizungumza na wananchi wa maeneo hayo, Mhandisi Seff amesema kuwa maelekezo aliyotoa wakati wa ziara yake hapo awali yamefanyiwa kazi na Ofisi ya TARURA Mkoa wa Songwe na kwamba hali ya Barabara hiyo kwa sasa ni nzuri na inapitika.
Kuhusu changamoto zilizopo katika baadhi ya maeneo ya barabara hiyo, Mtendaji Mkuu huyo amwagiza Meneja wa TARURA Mkoa wa Songwe kuendelea na matengenezo yaliyobaki ikiwa ni pamoja na kujenga makalavati kwa maeneo yenye uhitaji ili Barabara iendelee kutoa huduma kwa wananchi kwa kipindi chote.
’’Mwanzoni nilifanya ziara katika eneo hili nikatoa maelekezo na kweli kazi imefanyika na Barabara inatoa huduma kwa wananchi, tayari nimeelekeza kufanyika matengenezo kwa maeneo machache yaliyobaki ikiwa ni pamoja na kujenga makalavati ili Barabara iendelee kutoa huduma kwa wananchi kama yalivyo malengo ya Serikali,’’amesema Mhandisi Seff.