NA GODFREY NNKO
BOHARI ya Dawa nchini (MSD) imesema kuwa,imeendelea kufanya mageuzi makubwa katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo kununua teknolojia ambayo itamtibu mgonjwa au kumfanyia uchunguzi hapa nchini.
"Leo MSD ananunua bidhaa moja ya shilingi bilioni 5.7, ananunua teknolojia, tulikuwa tunanunua boksi za dawa, kwenye kopo la vidonge 1000,syrup, dripu,bandeji, sasa tunapotoka kwenye kununua dawa mpaka leo tumefika kununua teknolojia ni hatua kubwa.
"MSD inanunua teknolojia ambayo inakwenda sasa kumtibu Mtanzania au kumfanyia uchunguzi. Kwa hiyo, ninadhani kuna ile-revolution tunayokwenda nayo.
"Yale mageuzi ukikosea tu kwenye timing, yanakuacha, yakikuacha taasisi ina-struggle, tunachofanya sasa hivi ni reform ya MSD iendane na matakwa ya leo, matakwa ya leo ni tofauti na wakati ambao tunaanzisha taasisi hii;
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai ameyabainisha hayo Septemba 27, 2023 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Bohari ya Dawa nchini (MSD), ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya, iliyoanzishwa mwaka 1993 kwa mujibu wa Sheria ya Bohari ya Dawa iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2021.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu huyo, MSD inatekeleza majukumu manne ikiwemo uzalishaji, ununuzi, utunzaji na usambazaji.
"Tulianza 1993, na sheria yetu ilibadilika mwaka 2021 ambapo tuliongezewa jukumu la uzalishaji, sasa ukiangalia kwenye upande wa uzalishaji, hili ni jukumu muhimu sana kwa mwelekeo wa Tanzania hasa kwa kuzingatia uchumi ambao unategemea zaidi viwanda au ina mkakati wake wa ndani wa viwanda.
"Mkakati huu umepitishwa, imefanya upembuzi yakinifu ya namna ya kufanya kazi kuboresha sekta ya viwanda, katika maeneo ambayo tumefanya vizuri sana mwaka huu katika reform zetu ni eneo hili.
"Tulichofanya cha kwanza baada ya viwanda vya masks (barakoa) kuwepo pale na kiwanda cha gloves (mipira ya mikono) ambacho kinajengwa tukatengeneza kitu kinaitwa MSD Subsidiary Company (MSD Med Farm).
"Lengo ni kwamba tusiipe mzigo taasisi kama ilivyo, tuitengenezee specializing vehicle ambayo itafanya kazi kwa utaratibu na usimamizi wa utararibu mzima wa uendeshaji wa masuala ya viwanda, na inatakiwa ishirikiane na sekta binafsi.
"Kushirikiana na sekta binafsi ni moja ya mafanikio au mkakati mzuri zaidi wa kufanikisha, kwa hiyo tutakuwa tuna miradi mmeona (wahariri) kwenye magazeti yenu tukiwatangazia ya Idofi, ya pamba za dawa Simiyu na kiwanda kingine cha dawa huko Kibaha, ile ni zao la hii kampuni.
"Tulikaa tukasema hapa tuweke sekta binafsi, tushirikiane nao, kwa hiyo tumekaribisha na matokeo ni mazuri kwa sababu hadi sasa ninapokea maombi mengi sana ya kuwekeza, kufanya kazi kwa ubia.
"Na kingine ambacho tumemuita msimamizi mkuu wa kiwanda cha Keko aje hapa ni kwa sababu kiwanda cha Keko kinamilikiwa na Serikali kwa asilimia 70, asilimia 30 inamilikiwa na sekta binafsi.
"Msajili wa Hazina ametukasimisha sisi MSD kuhakikisha kwamba kile kiwanda kinasimama,kwa hiyo moja wapo ya vitu ambavyo tumefanya ni kupeleka watu wetu pale,na tunatarajia ndani ya muda mfupi ujao tutaona mabadiliko makubwa katika kiwanda cha Keko.
"Upande wa manunuzi, tunanunua bidhaa nyingi kutoka nje,lakini kwa sasa tunaboresha zaidi manunuzi kutoka ndani,suala la ununuzi, kitu ukiwa unataka kununua kama dawa ni rahisi kukipata kwa sababu inazalishwa, inatuzwa kwenye ghala unachukua.
"Lakini vifaa kwa mfano unanunua leo Mortuary Cabinet, mashine kama CT-Scan unaponunua ndipo inapoanza kutengenezwa,zile malighafi za kutengeneza utakuta zinatoka nchi hadi tano.
"Kwa hiyo mpaka aunganishe akuletee itachukua miezi tisa hadi mwaka kupata bidhaa, ndiyo maana tangu mwaka jana kulikuwa na pressure sana ya vifaa tiba, lakini sasa hivi tunapokea vifaa tiba vingi kwa sababu viliagizwa miezi tisa mpaka 12 iliyopita.
"Na hii ndiyo inaonesha ule ugavi wetu, kuwa impact ya leo inatokana na kazi kubwa ambayo ilifanyika mwaka jana mwezi wa tisa mpaka wa nane.
"Na makosa tutakayoyafanya leo, tutayaona mwakani mwezi wa 10, kwa hiyo inabidi tu-sustain hii effort kwa sababu wanakuja kuona matokeo baadae.
"Jukumu la tatu katika MSD,ni suala la utunzaji na ni eneo ambalo pia tumewekeza vizuri na mmeona juhudi zetu, tunatunza katika kanda zetu 10 na makao makuu ya Dar es Salaam."
Amesema, pia wana jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa uhakika katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini na wamekuwa wakitekeleza hilo kwa ufanisi mkubwa.
Mkurugenzi Mkuu huyo amefafanua kuwa,MSD imekuwa ikifanya usambazaji wa bidhaa za afya moja kwa moja kwenye vituo (direct delivery).
“Usambazaji unafanyika kila baada ya miezi miwili tukiwa na magari zaidi ya 185 na makabidhiano yanafanyika kwa mfumo wa PoD (kupitia TEHAMA),” amebainisha.
Amesema, kupitia kanda zake 10 ambazo zinajumuisha mikoa ya Dar es Salaam,Tanga, Kilimanjaro, Iringa, Mbeya, Mwanza, Tabora,Kagera,Mtwara na Dodoma wanahudumia zaidi ya vituo 7,600 vya afya.
"Sasa katika utunzaji huo, kutokana na wingi wa mizigo, ninaweza kusema kwa ujasiri kabisa MSD inakuwa, inakuwa kwa namna gani, inakuwa kwa size (volume of busines) na tunaanza kuwa na mali nyingi ghalani.
"Lile tatizo la uhaba wa hifadhi limekuwa kubwa zaidi, kwa sasa hivi tunatumia kama square mita 56,000 za maghala yetu, lakini katika hizi pia kuna ambazo tumekodi na kuna ambazo tunatakiwa tujenge ili kuboresha miundombinu ya utunzaji.
"Lakini,eneo la nne ambalo ninaweza kusema tumefanya vizuri sana katika mwaka huu ni usambazaji,tunapeleka moja kwa moja katika vituo 7,600 nchi nzima.
"MSD ina wafanyakazi 630, lakini wanafika vituo elfu saba mia sita na kitu, na tulikuwa tunaenda kabla ya mwaka jana mara nne tu kwa mwaka ile tunaita quater.
"Sasa hivi tunaenda mara sita kwa mwaka na tumefanikiwa kufikisha huduma kwa mwaka kwa asilimia zaidi ya 95, hii maana yake tumeongeza kasi ya usambazaji kwa asilimia 50.
"Sasa kama magari yalikuwa yale yale,tumeweza kufanya hii maana yake wafanyakazi wetu wanafanya kazi zaidi, na ndiyo maana wanajitolea sana kwa sababu sisi tunasambaza huduma za kiuponyaji, si ule wa kiimani, lakini huu wa kawaida wa kibinadamu, kwa hiyo tutakaposinzia tu sisi tunakwenda kuleta maafa,"amefafanua Mkurugenzi Mkuu wa MSD Tukai.
Upatikanaji bidhaa
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa nchini (MSD), Mavere Tukai amesema kuwa, upatikanaji wa dawa nchini umefikia asilimia 81 mwezi Juni 2023 kutoka asilimia 57 mwezi Juni 2022 jambo ambalo limechangia kurahisisha utoaji huduma nchini.
Amesema kuwa, upatikanaji wa bidhaa za afya nchini umeendelea kuimarika siku baada ya siku kutokana na uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.
“Kutokana na uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Rais Samia umechangia upatikanaji wa bidhaa za afya kutoka asilimia 51 mwezi Juni 2022 hadi kufikia asilimia 64 Juni 2023,”amesema Tukai.
Fedha
Tukai amesema kuwa, fedha iliyopokelewa mwaka wa fedha 2022/23 ni shilingi bilioni 190.3 ikilinganishwa na shilingi bilioni 134.9 mwaka wa fedha 2021/22 sawa na asilimia 95.
“Mapato kwa mwezi Agosti 2023 lengo ni shilingi bilioni 35.68, utendaji halisi shilingi bilioni 34.08,”amesema huku akiongeza kuwa,kwa sasa MSD inajitegemea katika uendeshaji wake licha ya Serikali kuendelea kuwapa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa.
Sambamba na vifaa tiba na vitendanishi, hivyo ameendelea kuishukuru Serikali ya Rais Dkt.Samia, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu pamoja na Wizara ya Fedha ambayo hivi karibuni ilitangaza kuwaongezea fungu.
Pia amesema, ununuzi wa bidhaa za afya kutoka kwa wazalishaji wa ndani umeongezeka kutoka shilingi bilioni 14.1 mwaka wa fedha 2021/22 hadi kufikia shilingi bilioni 39.77.
Aidha, amesema wamejipanga kutoagiza bidhaa kutoka nje ya nchi hususani zile ambazo zinakidhi mahitaji na viwango vya ubora, hivyo kutegemea wazalishaji wa ndani.
“Na tumefanikiwa kuongeza idadi ya mikataba ya muda mrefu kutoka mikataba 100 yenye bidhaa za afya 711 kwa mwaka wa fedha 2021/22 hadi kufikia mikataba 233 yenye bidhaa 2,209 kwa mwaka wa fedha 2022/23,”amefafanua Tukai.
Aidha, kwa upande wa uzalishaji wa bidhaa za afya, Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, MSD imeendelea na uzalishaji barakoa, huku mradi wa wa viwanda vya Idofi ulioko Makambako uko hatua za mwisho
Tukai amesema,mradi huo ukikamilika utazalisha mipira ya mikono (eurgical and examination gloves), vidonge (tablets), rangi mbili (capsules), vimiminika (syrup), na dawa za ngozi (ointment and cream).
“Miradi hii chini ya MSD itasaidia kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini," amesema huku akiongeza kuwa, MSD imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kushiriki katika ujenzi wa viwanda nchini kwa njia ya ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi ambapo hadi sasa mchakato huo unaenda vizuri.
Pia amesema kuwa, utekelezaji wa majukumu ya MSD unaenda sambamba na utekelezaji wa maelekezo ya maboresho ya utendaji yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, wakati alipoteua uongozi mpya wa bohari hiyo.
Amesema kuwa, MSD inapitia mifumo yote ya uendeshaji ikiwemo mnyororo wa ugavi, usimamizi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuendana na kasi ya ongezeko la ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya vinavyojengwa na Serikali na kuhakikisha malengo ya Serikali katika upatikanaji wa bidhaa za afya yanafikiwa.
Mbali na hayo, Tukai amesema, MSD imeendelea kuwa kinara kwa usambambazaji wa dawa kwa nchi za Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Amesema, bohari hiyo inaendelea kushirikisha balozi mbalimbali hususani China, Algeria, Urusi na Korea ya Kusini ili kutafuta wadau wa uzalishaji na ununuzi na kutumia wadau wa ndani na nje ya nchi, lengo likiwa ni kuongeza uzalishaji wa bidhaa za afya nchini.
Pia amesema, wameboresha muundo wa taasisi kwa lengo la kuimarisha utendaji wa taasisi, ugatuzi wa shughuli zilizokuwa zikifanyika makao makuu kwenda Ofisi za Kanda na Kutumia vyanzo mbadala vya fedha ili kuongezea uwezo wa kifedha taasisi.
Tukai akizungumzia utekelezaji wa Mradi wa Ununuzi na Usambazaji wa vifaa vya huduma kwa wajawazito wanaopata uzazi pingamizi wakati wa kujifungua (CEmONC) amesema, awamu za utekelezaji ni tano.
“Na idadi ya vituo vya kutolea huduma vinavyopelekewa vifaa ni 284, jumla ya vifaa vilivyopangwa kusambazwa ni 345 na idadi ya vifaa vilivyosambazwa hadi kufikia Juni 2023 ni 299, sawa na asilimia 87,”amefafanua Mkurugenzi Mkuu huyo.
Ameongeza kuwa,thamani ya vifaa vinavyotarajia kusambazwa ni shilingi bilioni 99.7 ambapo thamani ya vifaa vilivyosambazwa ni shilingi bilioni 79.4 ikiwa ni sawa na asilimia 80 za utekelezaji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile akizungumza kwa niaba ya wahariri ameishauri serikali kulipa deni wanalodaiwa na MSD ili kuwezesha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa haraka, pamoja na kupongeza ushirikiano uliopo kati ya MSD na sekta binafsi nchini.
Balile pia ameipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kuweka utaratibu wa ofisi za umma kukutana na wahariri ili kueleza changamoto na mafanikio na kujibu maswali ya wanahabari. “Hii ndio tofauti na wale wanaoitwa waandishi wa kisasa,”amebainisha.
Tags
Afya
Habari
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
Makala
MSD
MSD Tanzania
Ofisi ya Msajili wa Hazina