Mtanzania aibuka kidedea Miss Africa International 2023

NA DIRAMAKINI

MTANZANIA Nazimizye Adam Mdolo ameibuka kidedea katika michuano ya Miss Africa International 2023 iliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Palm Royal Beach jijini Accra nchini Ghana.

Mrembo huyo alichuana vikali Jumamosi ya Agosti 26, 2023 na Adian Mehari kutoka nchini Eritrea, Sephanie Chukwuemeka kutoka nchini Nigeria, Atangana Damienne kutoka nchini Cameroon.

Wengine ni Jessica Geoge kutoka Liberia, Christine Warun kutoka Sudan Kusini, Helen Tamotumo kutoka nchini Botswana, Stella Amu kutoka nchini Ghana na Sanaa Youssef kutoka nchini Misri.

Miss Africa International ambao ni waandaaji wa tukio hilo la aina yake kupitia toleo lake la 2023 walisema shindano hilo ni mahususi kuonesha utajiri wa utamaduni wa Kiafrika na kutangaza utalii, likisimamia nchi 54 zinazowakilisha warembo wengi wa Bara la Afrika.

Aidha, kama shirika, wanaamini ni muhimu kwa raia wote wa bara hilo kufahamiana kuanzia tamaduni na mila mbalimbali na ni lengo lao kuonesha kila kipengele cha utofauti wao ili kufahamiana zaidi.

Pia, wamejipa kazi muhimu kupitia Lengo la 5 la Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ambalo linaangazia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.

Lengo lao la shindano hilo ni kuwawezesha washiriki ujuzi wa uongozi na ujasiriamali ambao utawasaidia kubaki shupavu na wenye uwezo wa kusimama, kujitegemea na kujieleza bila woga.

Pia, wanaamini kuwa wanawake ni mojawapo ya nguvu kazi kubwa zaidi ya uchumi wa Afrika na ni muhimu kwamba wawe na kila kitu wanachohitaji ili kuwa na mchango mzuri katika majukumu yao.

Baada ya ushindi huo, Nazimizye Adam Mdolo licha ya kuonesha tabasamu la hali ya juu pia, alitoa shukurani za kipekee, "kitu chochote changu ambacho ninakipigania, ninahakikisha kuwa ninafikia asilimia 50 ya kitu hicho, bila kuangalia kukata tamaa.

"Sasa kama mshindi wa Miss Africa International 2023, najiona ninakaribia asilimia 100 ya malengo yangu katika tasnia ya urembo, asante tena Miss Africa International kwa kuona uwezo wangu na kuniamini mimi.

"Ninaahidi kuwa balozi mzuri wa shirika.Kwa washiriki wenzangu wote, kwa kuwakilisha nchi zetu sisi sote ni washindi, tutaendelea na urafiki wetu kwa sababu sisi ni dada sasa, kwa warembo wote wa Kiafrika,tumia fursa zote kuzifikia kwa njia yako.

"Kuna neema katika kila moja yapo, usiwaangalie wanaokatisha tamaa, jiangalie mwenyewe. Nashukuru familia yangu, marafiki, mashabiki, vyombo vya habari Tanzania, kurasa za warembo na wote walioniunga mkono kwa namna moja au nyingine, Mungu awabariki kwa kufanikisha safari yangu."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news