Naibu Waziri Mkuu aielekeza REA kutumia muda mwingi vijijini

NA VERONICA SIMBA-REA

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Dkt. Doto Biteko ameiagiza Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kutumia muda mwingi zaidi wa kazi vijijini na muda mchache ofisini ili waendelee kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini. 
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (katikati) akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Septemba 19, 2023 Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy. 

Ameyasema hayo Septemba 19, 2023 wakati alipokutana na kuzungumza na Menejimenti ya REA katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Nishati, zilizoko jijini Dar es Salaam. 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba (aliyesimama), akizungumza wakati wa kikao cha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Septemba 19, 2023, Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam. 

“Najua mnafanya kazi kubwa ya kuandaa na kuratibu miradi mnayoitekeleza lakini nawashauri nendeni vijijini na tumieni muda mwingi zaidi wa kazi vijijini ambako ndiko miradi yenu inakotekelezwa ili muweze kuisimamia vizuri na kuhakikisha inatekelezwa kwa ufanisi,” amesisitiza. 
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (katikati) akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini - REA (hawapo pichani), Septemba 19, 2023 Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam. 

Aidha, Dkt. Biteko ameipongeza REA kwa kazi nzuri inayofanya katika kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata huduma za nishati bora sawa na walioko mijini. Amewataka kuendelea kuchapa kazi ili azma ya Serikali kuhakikisha kila mwananchi aliyeko kijijini anatumia nishati bora iweze kufikiwa. 

Awali, akiwasilisha taarifa za miradi inayotekelezwa, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amesema mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuongeza hali ya upatikanaji umeme vijijini kutoka asilimia mbili wakati Wakala unaanzishwa mwaka 2007 hadi asilimia 69 mwaka 2020. 
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (kushoto), akimwelekeza jambo Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy (aliyesimama), wakati wa kikao chake na Menejimenti ya REA katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, Septemba 19, 2023. 

Mhandisi Saidy amesema kuwa mafanikio mengine ni kuwezesha upatikanaji wa huduma ya umeme katika Makao Makuu ya Wilaya 26 ambayo yalikuwa hayajafikiwa pamoja na kuanzisha mpango wa kupeleka umeme katika vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara. 

“Hadi Agosti 31 mwaka huu jumla ya vijiji 10,987 sawa na asilimia 89 ya vijiji vyote vimefikiwa na umeme na vilivyobaki vitakamilika kabla ya Juni 2024,” ameeleza. 

Vilevile, ametaja mafanikio mengine kuwa ni kuunga vijiji na vitongoji 4, 234 kwa kipindi cha miaka miwili kupitia miradi mbalimbali, kusaini mikataba ya miradi sita kwa ajili ya kupeleka umeme vijijini ndani ya kipindi cha miezi 12 iliyopita pamoja na kuwezesha ujenzi wa miradi midogo 121 hivyo kuunganisha wateja 178,401 katika maeneo mbalimbali yaliyo mbali na gridi ya Taifa. 
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy (aliyesimama), akiwasilisha taarifa kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (katikati) kuhusu miradi inayotekelezwa na REA katika kikao kilichofanyika Septemba 19, 2023 Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam. Wa pili kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu. 
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy baada ya kikao kazi baina yake na Menejimenti ya REA, Septemba 19, 2023 Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam. 

Mengine ni kuanzisha mpango wa kuwezesha ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta vijijini, kuongezeka kwa uwekezaji katika viwanda vya kuzalisha vifaa vya ujenzi wa miradi kutoka viwanda sita mwaka 2007 hadi viwanda 56 mwaka 2021 ambavyo huzalisha nguzo, nyaya, mita, mashineumba na viunganishi. 
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Septemba 19, 2023 Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, baada ya kikao kazi baina yao. Kushoto kwa Naibu Waziri Mkuu ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy. 

Mkurugenzi Mkuu amemhakikishia Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kuwa, REA itaendelea kujituma pamoja na kuleta ubunifu katika kuharakisha upatikanaji wa nishati bora maeneo ya vijijini. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news