NIC,sisi ndiyo bima-Dkt.Elirehema

NA GODFREY NNKO 

SHIRIKA la Bima la NIC Insurance (NIC) limesema ndani ya miaka mitatu ya mageuzi licha ya kutengeneza faida kubwa, kuboresha huduma zake pia limekuza mtaji.
Hayo yamesemwa leo Septemba 11, 2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Dkt.Elirehema Doriye katika kikao kazi na wahariri nchini ambapo ameeleza mafanikio ya NIC kwa miaka mitatu kuanzia 2019/2020 hadi 2021/2022. 

Ikiwa ni mwendelezo wa vikao vinavyoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ili mashirika na taasisi zilizopo chini yake ziweze kueleza zilipotoka,zilipo na zinapokwenda. 

NIC ni kati ya mashirika ambayo yamefanya mageuzi makubwa sana kwa muda mfupi,licha ya awali kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Kutokana na kuichukua hatua mbalimbali, NIC wameweza kuondoa hasara kwa kuongeza mapato kutoka shilingi bilioni 76.45 mwaka 2019/20 hadi shilingi bilioni 103.94 kwa mwaka 2021/22 ikiwa ni ongezeko la asilimia 17.98 kwa mwaka. 

Mkurugenzi Mtendaji wa NIC,Dkt.Elirehema amesema kuwa,NIC imekuwa ikitekeleza shughuli zake kwa kuzingatia mwongozo wa uanzishaji wake (MEMART) na Sheria ya Bima Na.10 ya mwaka 2009. 

Aidha, amesema shirika hilo la umma ambalo lipo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina lilianza kuchukua hatua za mabadiliko ya kiutendaji ili kujiimarisha kibiashara tangu Julai, 2019. 

“Kutokana na ukuaji wa NIC katika nyanja mbalimbali ikiwemo mwendelezo mzuri wa kupata faida na ukuaji wa mtaji, NIC limeendelea kuvutia wateja wa bima kwa vigezo mbalimbali. 

“Kwanza, tuna uzoefu wa muda mrefu katika sekta ya bima nchini, pia tuna hekima na urithi, kwa hiyo sisi ndiyo bima.” 

Pia, amesema kutokana na thamani, ubora na imani waliyonayo kwa wateja wao ndiyo iliwawezesha kupata chapa ya East Africa Superbrand. 

“Na tumekuwa certified na ISO kutokana na kukidhi vigezo vya ubora vya kutoa huduma nzuri Kimataifa.” 

Dkt.Elirehema amesema, shirika hilo ambalo ni la kwanza katika sekta hiyo kuanzishwa na Rais wa Kwanza, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage, Oktoba 16,1963 ndilo lililenga kuongeza ufanisi katika kuwafikia wananchi. 

“Wakati ule ndiyo tulikuwa tumepata Uhuru na kwa sehemu kubwa, Tanganyika ilikuwa inaendeshwa na wakoloni, hivyo Watanganyika walikuwa wanatambulika kama watu wa daraja la chini sana. 

“Kwa hiyo, maisha ya mtu mweusi yalikuwa yanatambulika ni ya chini sana, na mali zao pia, na kibima hauwezi kuweka kinga ya bima kwa watu ambao maisha yao ni duni. 

“Pili, biashara ya bima ilikuwa inafanyika kutokea Nairobi, kwa hiyo ilikuwa ni nchi ya mavuno, lakini matumizi yalikuwa yanafanyikia nje ya nchi.” 

Dkt.Elirehema amesema, kutokana na makampuni mengi yalikuwa ya nje na yalikuwa yakifanya kazi kwa manufaa ya wamiliki kutoka nje. 

“Mwaka 1963 hadi 1967 NIC ilikuwa inaendeshwa kwa ubia kati ya Serikali na kampuni kutoka nje, lakini baada ya Azimio la Arusha ambalo lilikuja na utaifishaji NIC tangu mwaka 1967 ilikuwa inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100."

Amesema, NIC iliendelea kuwa kampuni ya pekee, mpaka mwaka 1996 ambapo, 1999 Serikali ikaingiza NIC kwenye mchakato wa kubinafsishwa, ingawa baadaye iliamua badala ya kubinafsishwa iendelee na uendeshaji. 

Aidha, Januari Mosi, 2010 yalitolewa maelekezo ya kuwekeza katika TEHAMA, kulipa madai na kufanya biashara katika mazingira ya ushindani, ingawa mabadiliko hayo hayakuzaa matunda. 

“Mwaka 2018, Desemba, miaka 10 baada ya maamuzi ya Baraza la Mawaziri, Serikali ikaamua kuondoa kabisa maamuzi yake ya kulibinafsisha shirika, kuanzia mwaka huo, shirika lilikuwa huru kufanya biashara.” 

Dkt.Elirehema amesema, NIC kwa sasa ni kampuni inayomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. 

Aidha, amesema shirika au kampuni hiyo inafanya biashara katika maeneo mawili, biashara ya bima za kawaida, kwa maana ya vitu vile ambavyo tunaweza kuviona au kuvigusa. 

“Mara nyingi hizi ni bima za mwaka mmoja, lakini zinagawanyika katika kipindi hicho katika eneo la mradi. 

“Eneo la pili ni bima za maisha, bima ya maisha mara nyingi ni ya muda mrefu, inawezekana unataka kupata bima ambayo unataka kuongeza kiwango chako cha maisha. 

“Bima za maisha mara nyingi zinaangalia katika eneo la uhai, na ni sehemu ya uwekezaji ili kupata kiwango fulani cha fedha. Kupitia bima hii, mtu anapata faida.” 

Dkt.Elirehema amesisitiza kuwa, NIC ni moja kati ya makampuni ya bima nchini, lakini, “sisi ndiyo bima, tunasema sisi ni bima ya mambo mbalimbali.Hii ni kampuni ya kibiashara ya bima ya Serikali. 

“Lakini kwa maana ya Sheria ya Bima Na. 10 ya mwaka 2009, hii ndiyo kampuni ya kwanza kusajiliwa Tanzania, kwa hiyo inatupa ujasiri wa kusema sisi ndiyo bima.” 

Dkt.Elirehema amesema kuwa, kurudi nyuma ya mwaka 2019, kulikuwa na madai mengi ambayo watu walikuwa wanadai, lakini baada ya uchambuzi ilibainika kuna madai hewa. 

Ufanisi 

Pia, amesema waliangalia ni namna gani ya kuondoa maeneo ambayo yanavujisha mapato, ili shirika lisiendelee kupata hasara kwa ajili ya kutengeneza faida. 
Pia,eneo la weledi na ubora wa wafanyakazi, miundombinu na mazingira ya ufanyaji kazi ni miongoni mwa maeneo ya maboresho yao. 

“Tulihakikisha kwamba, kila mfanyakazi anafanya kazi kwa kiwango cha hali ya juu na weledi, pia eneo la tija lilipewa kipaumbe. 

“Kwamba kwa kiwango gani, kila mfanyakazi anaweza kuchangia mafanikio ya shirika, kuanzia mfanyakazi wa chini hadi wa juu, tulihakikisha kwamba kila mmoja anakuwa na mchango katika shirika.” 

Pia amesema, waliangalia namna ya kuwaendeleza wafanyakazi wake, eneo lingine ni kuwekeza katika rasilimali watu. 

“Ili kuwapata wafanyakazi ilibidi kuwekeza kiasi kikubwa kwa wale wafanyakazi ambao tulikuwa nao, na kuongeza kama asilimia 25, lakini uwekezaji mkubwa tuliufanya kwa wale ambao walikuwepo awali kuhakikisha kwamba wanaleta tija,na weledi unaotakiwa.” 

Wakati huo huo, Dkt.Elirehema anasema kuwa,pia walihakikisha kwamba, kila mfanyakazi anakuja na ubunifu. 

“Ndiyo maana ukiangalia tangu mwaka 2019, kampuni yetu imekuwa na bunifu mbalimbali, na namna ya kuwahudumia wateja.” 

Pia, walipitia upya mpango mkakati wao ili kuhakisi huduma ambazo wanazitoa. 

“Kwa hiyo tulileta mabadiliko katika tafsri ya utendaji kazi, kwa kuangalia nafasi yetu ni ipi katika kutekeleza malengo yetu ya biashara, tulipitia upya misingi yetu, dhima, malengo,dhamira ili kuendana na uhalisia wa shughuli tunazozifanya. 

“Jambo la kwanza kuangalia vitu ambavyo vinatuletea faida, kwa hiyo yote yakabadilika na tukatengeneza mtazamo mpya, hivyo wafanyakazi tukataka waelewe mwelekeo wetu hii ni kampuni ya biashara.” 

Dkt.Elirehema pia amesema kuwa,NIC imefanya uwekezaji wa TEHAMA. Amesema, nyuma ya mwaka 1999 uendeshaji wao ulikuwa wa analojia, hivyo wakaona ni vema kuwekeza katika teknolojia ili kuongeza ufanisi. 

Miongoni mwa uwekezaji huo ni kupitia programu tumishi ambayo inamuwezesha mtumiaji kukata bima popote pale alipo, hivyo kuwawezesha kuongeza mapato. 

“Kwa sasa tumeamua kuachana na matumizi ya karatasi, tunatumia teknolojia, kwa sasa madai yako ukiwasilisha na nyaraka unalipwa ndani ya siku saba, haizidi siku saba, tofauti na huko nyuma hadi siku 30.” 

Akizungumzia katika eneo la kutengeneza utamaduni Dkt.Elirehema amesema, 

“Katika kampuni ambayo imepita safari ndefu za mabonde na mashimo, kunakuwa na utamaduni wake,kwa hiyo katika vitu ambavyo tulivifanya katika kuhakikisha kwamba tunajenga utamaduni, lakini pia mifumo tulihakikisha kuwa, katika utamaduni wetu, vitu vyetu vinatabirika, kwa maana ya mipangilio ambayo ipo wazi, yenye ubora inayostahili na inaweza kutoa ushaidi.” 

Pia, kuna masuala ya kuangalia muonekano wa shirika, ambalo kwa kurudi nyuma ya mwaka 2019, shirika lilionekana kuwa na taswira tofauti, kukosa ubunifu, hivyo kuonekana la kizamani. 

“Hivyo tukaangalia namna ya kufanya branding refresh, kubadili dhana potofu kuhusu shirika, tukaanza kutengeneza muonekano mpya wa shirika ambao uliwezesha sisi kupewa chata ya Superbrand ikiwa ni kampuni ya kwanza inayomilikiwa na Serikali.” 

Dkt.Elirehema amesema,katika uwekezaji kidigitali, kuna mapato ambayo yamepatikana zaidi ya asilimia 10 ya mapato. 

Mwaka 2019/2020, 2021/2022 mapato yamekuwa yakiongezeka zaidi ya asilimia 20. 

Pia, kwa upande wa matumizi yao wanahakikisha kiasi wanachotumia kinaenda katika madai, na kudhibiti matumizi ya kiundeshaji ili kuhakikisha shirika linasonga mbele. 

“Katika ulipaji wa madai, kwa sababu shirika lilikuwa katika kipindi kigumu muda mrefu, bima za maisha ni bima za muda mrefu. 

“Kwa hiyo tulichokifanya tuliamua kurudi nyuma kuanzia mwaka 1994, kuhakikisha kwamba kila mteja ambaye alikuwa anatudai tunamtafuta na tunamlipa. 

“Kwa ujasiri kabisa naweza kusimama mbele yenu kuthibitisha kwamba wadai katika kipindi hicho hakuna anayetudai.” 

Dkt.Elirehema amesema kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu wameweza kuwalipa wateja wao madai mbalimbali. 

“Hadi kufikia Juni 2022 tumelipa jumla ya shilingi bilioni 33.79 kwa bima za maisha. Na shilingi bilioni 40.18 kwa bima za mali na ajali.” 

Gawio 

Dkt.Elirehema amesema, shirika lilikuwa halijawahi kutoa gawio kwa Serikali kwa zaidi ya miaka 30. 

Aidha, amesema, Serikali imepewa shilingi Biloni 1.5 ikiwa ni gawio la kwanza lilitolewa kwa Serikali mwaka 2021. 

“Na mwaka 2022 tulitoa gawio la shilingi bilioni 2. Pia, niipongeze Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kuwa ofisi yenye maono makubwa zaidi, na kuyapokea maono ya Mheshimiwa Rais na kuyashusha kwetu.” 

Mbali na ubunifu wa bidhaa mbalimbali, Dkt.Elirehema amesema,upande wa ukuaji wamekuwa kwa asilimia 108. 

“Lakini umiliki wa soko kwa asilimia 16 mpaka mwezi wa 12, mwaka jana.Mali zimekuwa kwa asilimia 7, ukuaji wa mtaji kwa wanahisa umekuwa kwa asilimia 7.5. 

“Pia,tunahakikisha kwamba tunatekeleza mipango ya Serikali, sisi kama kampuni inayomilikiwa na Serikali tunahakikisha kwamba tunatekeleza mipango ya Serikali.” 

Pia,wamejipanga kubuni bidhaa ambazo ni za gharama nafuu kwa Watanzania ambao wana kipato cha chini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news